RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti, Zanzibar |
WANANCHI wakimshangilia Dk. Shein alipowahutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti |
Shein: Hatuna sababu ya kushindwa
Amchana Maalim Seif na Ukawa yakeUtekelezaji wa Ilani unaipa ushindi CCM kihalali
NA SULEIMAN JONGO, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema upinzani utaendelea kuisoma namba katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Amesema ushindi kwa CCM ni jambo lisilozuilika na kwamba, Watanzania na Wazanzibari wajipange kupiga kura kwa uhuru na amani.
Mbali na hilo amesema hakuna sababu ya kutishana kama wanavyofanya baadhi ya wagombea hususan kutoka upinzani kwa kuwa CCM ni Chama cha waungwana wanaoheshimu taratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, Dk. Shein ambaye pia ni mgombea urais wa CCM Zanzibar, alisema kwa namna CCM ilivyotekeleza ahadi zake ilizozitoa kupitia Ilani yake ya uchaguzi ya 2010, ni wazi kwamba Watanzania na Wazanzibari kwa namna ya pekee wataendelea kuiamini.
Alisema hakuna sababu kwa CCM kushindwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuwa imetekeleza ahadi zake na bado kupitia ilani ya mwaka huu, itaendelea kuahidi mambo ambayo inauhakika itayatekeleza.
"Ninachowahakikishia Wazanzibari mwaka huu ni kwamba, wapinzani wataisoma namba. Tutaendelea kushinda kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi uliopita," alisema.
Alisema ana uhakika wa ushindi kwa CCM utakaotokana na misingi ya ukweli, haki na amani si kwa hila kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Kwa mujibu wa Dk. Shein, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali yake imejitahidi kutekeleza mambo mbalimbali iliyoyaahidi kwa wananchi ambao ndio wapigakura.
Alisema shutuma za upinzani hususan makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwamba kuna matatizo kwenye tume ya uchaguzi, huo ni woga wa kisiasa unaotokana na kutokuwa na uhakika wa kushinda kwenye kila uchaguzi.
"Nawaomba wana-CCM endeleeni kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Kila mwenye haki ya kupiga kura atapata fursa ya kufanya hivyo bila bughudha.
"Sisi tutashinda tu kwa kuwa si mara ya kwanza. Tutashinda kihalali kwa kupigiwa kura na wananchi. Wanaolalamika kuibiwa kura wanazungumza mitaani bila kuonyesha ushahidi wa kisayansi.
"Sijaridhika na kauli za uongo zinazotolewa kwamba CCM tunaiba kura. Tutaenelea kulifanyia kazi. Kwenye vituo vya kupigia kura kuna wawakilishi wa vyama vyote, sijui huo wizi wa kura unafanyika vipi.
"Kauli hizi si za kidemokrasia hususan kutoka kwa kiongozi aliyebobea, ni kauli zinazolenga kuleta vurugu na kuchochea uvunjifu wa amani," alisema.
Alisema mwenye dhamana ya kulinda kura ni vyombo husika, si mwanasiasa wala chama chochote cha kisiasa.
Dk. Shein alisema kwa muda mrefu wana-CCM wamekaa kimya huku wanasiasa wengine wakiongea mambo mbalimbali, ikiwemo kutoa vitisho, lakini CCM haioni sababu ya vitisho hivyo.
Alisema Tanzania ni kisiwa cha amani na kila mmoja anatimiza wajibu wake kwa uhuru.
Rais Dk. Shein alisema kutokana na ukweli huo, ndio maana CCM haioni sababu ya kutoa vitisho kwa kuwa nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria.
Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, Dk. Shein alichukua fomu za kuwania urais katika uchaguzi mkuu huo.
Shughuli ya uchukuaji fomu hizo ilifanyika katika ukumbi wa hoteli hiyo, ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, alimkabidhi fomu hiyo.
No comments:
Post a Comment