Thursday, 6 October 2016

ATCL YATANGAZA NAULI MPYA ZA BOMBADIER


NA WILLIAM SHECHAMBO

SHIRIKA la Ndege la Air Tanzania (ATCL), limetangaza gharama za tiketi kwa ndege zake aina ya Bombadier, kwenye mikoa minne ya awali ya Tanzania Bara na  Zanzibar.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni wiki chache tangu Rais Dk. John Magufuli, azindue ndege mbili mpya za shirika hilo, aina ya Bombadier Q-400, zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja.

Taarifa iliyonaswa na Uhuru jana, kwenye ukurasa rasmi wa mtandao wa Instagram wa Shirika hilo (www.instagram.com/airtanzania_atcl),
zilionyesha kuwa ndege hizo zitaanza kutoa huduma mikoa mitatu ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mikoa hiyo ni Mwanza, Arusha na Kigoma na baadaye visiwa vya Zanzibar, ambapo gharama za tiketi zimeelezwa kuwa ni sh. 180,000 kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha na sh. 360,000 kwenda na kurudi.

Kwa mkoa wa Mwanza kutoka Dar es Salaam, tiketi itakuwa ikiuzwa sh. 160,000 kwenda na sh. 320,000 kwenda na kurudi, bei ambayo ni nafuu na ilivyo kwenye mashirika mengine binafsi ya ndege.

Mkoa wa Kigoma, tiketi kutoka Dar es Salaam itauzwa sh. 395,000 kwenda na sh. 610,000 kwenda na kurudi, huku Zanzibar kutoka Dar es Salaam itauzwa kwa sh. 123,000 kwenda na sh. 246,000 kwenda na kurudi.

Tiketi ya moja kwa moja kutoka Arusha kwenda Zanzibar itakuwa sh. 249,000, pekee, ambapo wadau wa usafiri wa anga wakiwemo abiria waliojibu kwenye ukurasa huo, walisema shirika hilo litakuwa na msaada mkubwa kwa Watanzania kutokana na unafuu wake.

No comments:

Post a Comment