Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu Hassan akishiriki kucheza ngoma, wakati kikundi cha kina mama kutoka Moshi Mjini kilipotumbuiza wakati wa mkutano huo |
Kamanda wa Umoja wa Vijana, Kinondoni Dar es Salaam, Angela Kairuki, akishauriana jambo na Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia, wakati wa mkutano huo wa kampeni |
Mama Samia, akimpongeza Devis Mosha kwa hotuba nzuri |
VIJANA wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, wameahidiwa kupatiwa pikipiki 30 za mkopo wa bei nafuu, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kujiongezea kipato.
Ahadi hiyo ilitokewa na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni wa Jimbo la Vunjo katika mji mdogo wa Marangu Mtoni.
Samia alitoa ahadi hiyo baada ya mgombea ubunge wa Vunjo (CCM), Meleck Shirima, kumweleza kuwa vijana wanahitaji mikopo, ikiwemo pikipiki kwa ajili ya kufanya biashara na kuinua vipato vyao.
Kutokana na mahitaji hayo, Shirima alimwomba mgombea mwenza kuwasaidia vijana hao ili waweze kukidhi kiu yao ya kuwa na maisha bora na kupunguza utegemezi.
Pia, aliiomba serikali kutoa sehemu ya fedha za mapato yatokanayo na Mlima Kilimanjaro kwa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ili izitumie kwa ajili ya maendeleo.
Akijibu ombi hilo, Samia alisema kwa kuanza anatoa pikipiki 30 ambazo zitatolewa kwa mkopo nafuu ili kuwawezesha vijana hao kufanya biashara ya kuendesha bodaboda.
Pia, alisema serikali ijayo ya CCM itahakikisha inakamilisha ujenzi wa Soko la Himo ili liweze kuwanufaisha wafanyabiashara wa Vunjo na mkoa kwa ujumla na kuwaunganisha na wenzao wa Kenya na Sudan Kusini.
“Soko hili liko katika mpango wa kujengwa ili liwe la kimataifa na watu wapate fursa ya kufanya biashara na wenzao wa Kenya na Sudan Kusini ambako kuna fursa kubwa ya biashara,” alisema.
Kero nyingine ambayo imekuwa kubwa kwa wakazi wa jimbo hilo, kwa mujibu wa Samia, ni maji katika maeneo ya tambarare.
Alisema kero hiyo itapatiwa ufumbuzi katika awamu ijayo na kwamba imewekwa katika mipango ya maendeleo kwenye Ilani ya CCM.
Ili kuhakikisha mambo hayo yanapatiwa ufumbuzi, aliwataka wananchi wa Vunjo kumchagua Shirima kuwa mbunge ili aweze kutoa msukumo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama.
“Chagueni Shirima ni kijana na mchapakazi tofauti na huyu aliyepo sasa (Augustine Mrema) ambaye kwa sasa hana nguvu za kufanya mambo kwa kasi. Huyu Shirima ni damu changa inayofanya kazi, mchagueni yeye na madiwani kutoka CCM,” alisisitiza.
UJENZI WA MABWENI MOSHI
Akiwa mjini Moshi, Samia alisema serikali ijayo ya awamu ya tano, itaweka mkazo mkubwa wa ujenzi wa mabweni katika Wilaya ya Moshi.
Samia alitoa kauli hiyo jana, katika mkutano wa kampeni wa Jimbo la Moshi Vijijini uliofanyika katika viwanja vya zahanati ya Manushi, mkoani hapa.
Alisema suala hilo ni moja ya mipango iliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hivyo litapatiwa ufumbuzi na hatimaye kuwalinda wanafunzi wa kike dhidi ya vishawishi na mimba za utotoni.
Samia alitoa kauli hiyo baada ya mgombea Ubunge wa Moshi Vijijini (CCM), Dk. Cyril Chami, kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa ya ujenzi wa shule ndani ya jimbo hilo, lakini changamoto kubwa kwa sasa ni mabweni.
Chami alisema ukoefu wa mabweni umewafanya wanafunzi wengi hasa watoto wa kike kutembea umbali mrefu na hata kukutana na changamoto nyingi za kitaaluma na kukatisha masomo kwa sababu ya kupata ujauzito.
Alisema jimbo la Moshi Vijijini kwa sasa lina shule za sekondari 50 katika kata 16, zikiwemo 29 za Kata.
Kutokana na changamoto hiyo, Samia alisema anatambua changamoto hiyo na kwa kuwa yeye ni mama anajua vikwazo anavyokutana navyo mtoto wa kike, hivyo atahakikisha inashughulikiwa ipasavyo.
Pia alisema barabara za Moshi Vijijini zitafanyiwa ukarabati ili kupitika mwaka mzima na kuondoa kero inayowasumbia wananchi hasa nyakati za mvua.
Ili kutekeleza yote hayo, aliwaomba wananchi kuichagua CCM katika nafasi za urais, ubunge na udiwani ili kutatua kero na kuleta maendeleo katika miaka mitano ijayo.
Alimsifu Dk. Chami kuwa ni msomi na mchapakazi ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, lakini aliamua kuwajibika kwa makosa ambayo hakuyatenda.
Alisema katika kipindi cha miaka 10 ambayo Moshi Vijijini imekuwa chini ya CCM, kuna maendeleo makubwa yamefanyika na yote hiyo ni kwa sababu ya CCM.
“Safari yetu ni ya maendeleo hivyo endeleeni kuipa kura CCM ili iweze kuwaletea maendeleo makubwa zaidi. Chami ndiye chaguo la kweli ndani ya ubunge. Ninamfahamu kwani tulikuwa wote mawaziri na ni mchapakazi hodari,” alisema.
No comments:
Post a Comment