Thursday, 27 August 2015

MAGUFULI ACHOTA NONDO KWA PINDA


NA SELINA WILSON, SUMBAWANGA
KATIKA kuthamini busara za viongozi waliomtangulia, mgombea Urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema atachota busara kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na atazingatia ushauri wake katika kuongoza nchi.
Amesema Pinda ni mwalimu wake, amemfundisha kazi kwa miaka 20 katika utendaji wa serikali kwenye wizara mbalimbali, hivyo atakuwa karibu naye ili aweze kuchota busara.
Dk. Magufuli aliyasema hayo juzi, wakati alipotembelea na kuzungumza na wananchi wa Kata ya Kibaoni, ambako ni nyumbani alikotoka Waziri Mkuu Pinda.
Alisema akiwa rais atahakikisha anaendelea kutoa mchango wake kwenye uongozi wa nchi na kwamba serikali itamtunza wakati wote wa maisha yake.
“Waziri Mkuu huyu amenifundisha kazi, kwa hiyo nitahakikisha naendelea kuchota busara zake. Tulikuwa wote kwenye mchakato, hakuna aliyejua nani atapata fursa ya kuteuliwa, lakini ananiunga mkono na mimi sitamuangusha,”alisema.
Aliwaomba wananchi waichague CCM ili waunganishe nguvu zao katika kuleta maendeleo ya haraka na kwamba yatapatikana kwa kusogeza huduma karibu na wananchi.
Dk. Magufuli alisema barabara za lami zinazounganisha wilaya na mikoa ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi kwa maana ya wakulima kuweza kufikisha mazao yao kwenye masoko.
STAILI YA KUOMBA KURA GUMZO
STAILI ya kuomba kura ya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, imeonekana kuwavutia wananchi wengi kiasi cha kusababisha umati wa maelfu ya watu wanaojitokeza kumsikiliza kulipuka kwa shangwe.
Dk. Magufuli amekuwa akijitambulisha kwa majina yake manne na kusisitiza kuwa wananchi wasisahau kumpigia kura Oktoba 25, mwaka huu.
“Mimi naitwa John Pombe Joseph Magufuli, mimi ndiye niliyekabidhiwa na CCM ridhaa ya kupeperusha bendera yake kwenye urais. Nakuomba mwananchi uwe CHADEMA, CUF, TLP na wana CCM wote, mnipigie kura ili niwe rais.
Ukisahau majina yangu, kumbuka Pombe basi ndiyo mie, ukisahau Pombe, basi kumbuka Magufuli, mwenye jina hilo nipo peke yangu. Jina langu baya, lakini mimi ndiye ninayefaa kuwa rais na kuwaletea mabadiliko ya kimaendeleo,”alisema.
“Yaani siku ya Oktoba 25, ukienda kupiga kura kumbuka Pombe tu ndiyo utakuwa umenichagua na umenipata ‘Rais Special’,” akimaanisha rais bora mwenye uwezo wa kuwatumikia wananchi,
Staili hiyo ambayo ameitumia katika mikutano mbalimbali ya kampeni juzi, ilisababisha umati wa maelfu ya wananchi waliofurika kushangilia huku wengine wakiimba ‘Jembe , Jembe, Jembe’ wakimaanisha kwamba Dk. Magufuli ni mchapa kazi.
Dk. Magufuli katika mikutano yake alikuwa akikonga nyoyo za wananchi kwa staili yake ya kutoa salamu kwa lugha za makabila mbalimbali ikiwemo, kifipa, kinyakuyusa, kisukuma, kiha,kichaga,kihaya, kisafa na zingine, hali ambayo ilikuwa ikiwafanya wananchi kushangilia huku wengine wakiitikia kwa lugha hizo.
Katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Nelson Mandela, Mjini Sumbawanga, Dk Magufuli pia aliwataka wananchi kudumisha upendo na mshikamano ili kuleta maendeleo ya Tanzania mpya.
Wagombea wafundwa
WAGOMBEA ubunge wa majimbo mbalimbali wametakiwa kushirikiana na walioshindwa kwenye kura za maoni na kuwaunganisha wananchi ili CCM ipate ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu na kwamba atawapatia kazi za kufanya walioshindwa kura za maoni.
Wagombea hao ni wa Kalambo, Josephat Kandege, Dk. Lucas Siyame (Momba), Aeshi Hilary (Sumbawanga Mjini) na Ignas Malocha wa jimbo la Kwela.
Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, alitoa ahadi juzi na jana, katika mikutano ya hadhara na kila alipowasalimia wananchi waliofunga barabara kwa lengo la kutaka kumlaki.
Pia aliwaombea msamaha wagombea hao kwa wananchi kwa mambo mbalimbali waliyowakosea huku akisisitiza kwamba hakuna malaika kwenye uongozi, kinachotakiwa ni kuwasamehe ili waendelee kushirikiana kuleta maendeleo.
Akifafanunua juu ya walioshindwa kura za maoni, alisema kwenye uchaguzi ni lazima apatikane mmoja, hivyo aliwaomba kuvunja makundi na kwamba baada ya uchaguzi atawapa kazi za kufanya kwa kuwa walikuwa na nia ya kuwatumikia wananchi.
“Nikiwa rais wenu, sitakosa kazi ya kuwapa mfanye. Naomba wabunge mkishashinda , mje nao kwangu mimi nitawapa kazi. Kwenye serikali kuna kazi nyingi za kufanya na rais hawezi kushindwa kumpa mtu kazi,”alisema.
Aliwataka wananchi bila kujali itikadi zao, wawachague wabunge hao pamoja na madiwani wa CCM ili kujenga safu bora ya utendaji kazi.
“Najua zipo changamoto nyingi, wengine wamekasirika baada ya kura za maoni, lakini ninachowaahidi ni kwamba sitawaangusha, nitashirikiana nanyi na nyie naomba mshirikiane kutafuta ushindi wa CCM,” alisema.
Dk. Magufuli alisema wakati wa kumpata mgombea urais wa CCM, walikuwa 38, lakini vikao vilifanya kazi na kura zikapigwa, yeye akibuka na kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM, hivyo na kwa wabunge na madiwani ni hivyo, kwa maana hiyo ni lazima apatikanane mmoja kuwakilisha wengine.
“Hapa Momba najua uchaguzi uliopita mlipoteza mkachagua upinzani, mmepata shida, hata fedha za mfuko wa jimbo hamjaziona, sasa mchagueni Dk. Siyame, ninamfahamu ni mchapa kazi, ndiye aliyenisukuma kujenga barabara ya lami ya Sumbawanga/Tunduma,” alisema.
Akiwa njiani kuelekea Tunduma, msafara wa Dk. Magufuli ulisimamishwa katika vijiji mbalimbali, ambako wana CCM walilazimika kuunganisha bendera na kufunga barabara ili kumshawishi asimame na kuzungumza nao.

No comments:

Post a Comment