Tuesday, 5 January 2016

DK. SHEIN AWATAKA WATUMISHI WA AFYA KUZINGATIA MAADILI




RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amesema wakati serikali inatekeleza kwa kasi mpango wake wa kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya, watumishi wa sekta hiyo watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia miiko ya taaluma zao.
Akizungumza jana, katika hafla ya kuweka mawe ya msingi ya majengo mawili ya huduma za wazazi na watoto katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Dk. Shein alisema katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya uongozi wa serikali ya awamu ya saba, kasi ya uimarishaji wa sekta ya afya imeongezeka na kuifanya Zanzibar kupiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya.
Dk. Shein alisema azma ya kuipandisha hadhi Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja na Abdalla Mzee, Pemba pamoja na hospitali za Unguja na Pemba, kuwa za wilaya, imetekelezwa kwa kiwango kikubwa na wananchi hawana budi kujivunia mafanikio hayo.
Alisema azma ya serikali ya kuiwezesha hospitali ya Mnazi Mmoja kutoa huduma za upasuaji wa moyo iko pale pale na kuongeza kuwa utekelezaji wake utaanza wakati wowote.
Dk. Shein alisema Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kuweka mtandao wa miundombinu ya afya na utoaji wa huduma hizo pamoja na kuwa ziko changamoto kadhaa katika kufikia ubora na malengo yaliyowekwa.
Alisema hatua zilizochukuliwa kuzipandisha hadhi hospitali hizo ni pamoja na kuzipatia vifaa bora na vya kisasa na wataalam wanaotakiwa, japokuwa kumekuwa na upungufu wa majengo, ambao serikali imekuwa ikikabiliana nao hatua kwa hatua.
Majengo yaliyowekewa mawe ya msingi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ni jengo la wazazi na watoto wachanga, ambalo litakuwa na wodi ya kinamama, vyumba vya upasuaji, vyumba vya kujifungulia vya kisasa, sehemu ya huduma za dharura na huduma nyingine muhimu za kitabibu.
Jengo lingine ni la watoto wadogo litakalokuwa na wodi ya vitanda 100, kati yake 32 ni kwa watoto wenye magonjwa ya kuambukiza, 54 ya watoto wasiokuwa na magonjwa ya kuambukiza na 10 kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji huduma za kusafisha figo.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya Uholanzi kupitia shirika la ORIO, ambayo kwa kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inagharamia ujenzi wa jengo la wazazi na watoto na vifaa vyake kwa gharama ya Euro milioni 9.9.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Mahmoud Thabit Kombo, alisema wizara hiyo inafarijika na mchango mkubwa unaotolewa na Dk. Shein katika kuimarisha sekta ya afya.

No comments:

Post a Comment