Thursday, 21 January 2016

DK. MAGUFULI, SAMIA WASHIRIKI KUMUAGA LETICIA NYERERE








RAIS Dk. John Magufuli, jana, aliwaongoza waombolezaji kuuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Leticia Nyerere.
Shughuli ya kuuaga mwili huo, zilifanyika nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msasani, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na na mamia ya wananchi.
Viongozi wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan,  Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Rais  mstaafu Jakaya Kikwete, mke wake Mama Salma, Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal, mawaziri wakuu wastaafu, Joseph  Warioba na Mizengo Pinda.
Katibu Mkuu  Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,  Spika wa Bunge mstaafu Anna Makinda, Katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha Rose Migiro, Mwenyekiti wa  chama cha UDP, John Cheyo na wabunge mbalimbali.
Baada ya Rais Magufuli kuwasili, alitoa pole kwa mjane wa Baba  wa Taifa, Mama Maria Nyerere na familia yake, kisha aliwaongoza waombolezaji kuuaga mwili huo.
Baadhi ya viongozi  walimuelezea marehemu Leticia kuwa alikuwa mbunge machachari, aliyesimama katika msimamo  thabiti kwenye maamuzi yake.
Pinda alisema: “Letecia ni mmoja wa wabunge ambao walikuwa hawawezi kuruhusu  vikao vya bunge viishe bila kuchangia.
“Alikuwa na uwezo wa kujenga hoja na zilizolenga katika kutetea maslahi ya taifa. Tumempoteza mtu makini, ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika taifa na bado mchango huo ulihitajika.”
Anna Makinda alisema: “Nikiwa Spika wa Bunge, Leticia alikuwa mmoja wa wabunge  waliokuwa wajenga hoja wazuri. Siku zote  alizungumza kwa kujiamini na hakuyumba katika msimamo wake.”
Anna alisema Leticia alikuwa mtulivu na mfano bora kwa wabunge wengine wanawake na kwamba alipenda kujiendeleza kielimu.
Wasifu
Akisoma wasifu wa marehemu, Jaji Asha Makongoro, alisema Leticia alizaliwa Machi Mosi, 1959, katika kijiji cha Kitunga wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Alisema alifunga ndoa na Madaraka Nyerere, Agosti 15, 1987, katika Kanisa la St. Peters, Dar es Salaam na walipata watoto  wanne na walio hai ni Julius, Juliana na Helena.
Elimu
Alipata elimu  nje na ndani ya nchi katika vyuo na shule mbalimbali, ambapo  1966 hadi 1973, alisoma katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Mwaka 1974 hadi 1975, alisoma katika Shule ya Wasichana Jangwani na mwaka 1975 hadi 1976 alisoma katika Shule ya Wasichana Masasi.
Mwaka 1976 hadi 1978, alisoma Shule ya  Sekondari Arusha-Meru na mwaka 1979 hadi 1982, alihitimu Chuo cha Orel College of State Bank cha Russia na kutunikiwa diploma ya  masuala ya fedha.
Mwaka 2001 hadi 2002, alihitimu diploma ya masuala ya Uhusiano wa Kimataifa kutoka chuo cha Strayer cha Marekani na mwaka 2005 hadi 2008, alihitimu shahada ya masuala ya fedha  katika Chuo Kikuu cha Corlins cha Marekani na mwaka 2008 hadi 2011, alihitimu shahada ya uzamili (MA-In Finance) kutoka Chuo Kikuu cha Corline cha Marekani.
Leticia alianza kuugua  Oktoba, mwaka jana, na kupata matibabu katika hospitali mbalimbali huko India, Uingereza na Marekani.
Akiwa Marekani katika Hospitali ya  Community Doctors, iliyoko Lan Ham, Maryland, hali yake ilibadilika na hatimaye umauti ukamkuta Januari 10, mwaka huu.
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya familia ya Baba wa Taifa, Rose Nyerere, aliwamshukuru Rais Dk. Magufuli, viongozi wote, Bunge na wananchi kwa kushiriki kikamilifu katika msiba huo.
Mwili wa Letecia utasafirishwa hadi Butiama mkoani Mara, nyumbani kwa Baba wa Taifa kwa ajili ya maziko, yatakayofanyika leo.

No comments:

Post a Comment