Tuesday 22 September 2015

KISHIMBA AAHIDI KUSIMAMIA RASILIMALI




MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jumanne Kishimba, amewataka wananchi kumuunga mkono ili aweze kusimamia kikamilifu rasilimali zilizopo wilayani humo na pia kuharakisha maendeleo.
Kishimba, amesema licha ya kuwa na rasilimali nyingi, bado jimbo hilo liko nyuma kimaendeleo na kwamba, dhamira yake ya kuwania nafasi hiyo ni kuwainua wananchi.
Alikuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi mjini hapa, ambapo alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Kishimba alisema wapinzani wamejipanga kuwarubuni wakati hawana sera wala dhamira ya kweli ya kuwatumikia.
Awali, akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Kishimba alisema kuna mambo mengi yaliyofanyika katika kuleta maendeleo kwa wananchi na kwamba, serikali imejipanga kuyaendeleza kikamilifu.
Alisema atahakikisha tatizo la umeme kukatika mara kwa mara linapungua kama wananchi watampa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo, kwani linazidi kurudisha nyuma shughuli za maendeleo.
“Mimi kama mgombea ubunge wa jimbo hili kupitia CCM, nawaomba wananchi kunipa ridhaa ya kuliongoza ili tuweze kushirikiana kwa pamoja  katika kulinda raslimali zetu tulizonazo, ikiwemo migodi ya dhahabu kama vile Buzwagi, Bulyanhulu na viwanda mbalimbali, vikiwemo vya pamba, tumbaku pamoja na kuleta mikopo kwa vijana ili waweze kuendelea kujiajili wenyewe,”alisema Kishimba.

No comments:

Post a Comment