Tuesday 22 September 2015

SAMIA: ICHAGUENI CCM IWALETEE MAENDELEO




Na Khadija Mussa, Mkinga
WANANCHI wametakiwa kuendelea kuichagua CCM na kuachana na vyama ambavyo havijajipanga kwa ajili ya kuwaongoza na havina mfumo wa uongozi.
Hayo yalisemwa jana na mgombea mwenza wa urais wa CCM , Samia Suluhu Hassan, katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Duga wilayani hapa.
Samia alisema wananchi wamchague Dk John Magufuli kuwa rais ili waweze kupata maendeleo na wasithubutu kuchagua wapinzani wanaojiita UKAWA kwa kuwa hawajajipanga kuongoza nchi na hawana mfumo wa uongozi.
"Kwanza mgombea wao urais ni CCM maslahi, amekodi chama kwa pesa nyingi na hajapitia mchakato wowote, hivyo hajajipanga kuongoza nchi," alisema.
Samia aliongeza kuwa hakuna sababu ya kuichagua UKAWA kwani umoja huo haujasajiliwa sehemu yoyote, hivyo aliwaomba kuendelea kuichagua CCM kwa kuwa ndicho chama chenye kuwaletea maendeleo.
Naye Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu, aliwaomba wananchi hao kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kuchagua wagombea wa CCM.
Alisema wakimchagua Dk Magufuli, watamuwezesha Samia kuwa makamu wa rais, hivyo kuliwezesha taifa kusonga mbele kimaendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Tanga, Henry Shekifu, alisema CCM kazi yake kubwa ni kuwaletea maendeleo wananchi na kuboresha amani, hivyo aliomba wananchi waichague.
Awali, akiwa njiani kwenda Mkinga, Samia alilazimika kusimamisha msafara katika eneo la Mtimbwani wilayani hapa ili kuzungumza na wananchi waliozuia msafara wake.
Akizungumza na wananchi hao, alisema serikali ijayo itahakikisha umeme unapatikana katika vijiji vyote nchini katika muda wa miaka miwili, hivyo aliwaomba wamchague Dk. Magufuli kuwa rais.

No comments:

Post a Comment