Tuesday 8 September 2015

MASSABURI: HATUHITAJI MABADILIKO YA DHARULA




NA MARIAM MZIWANDA
MGOMBEA Ubunge wa CCM katika Jimbo la Ubungo, Dk. Didas Massaburi, amesema Watanzania hawahitaji mabadiliko ya dharura bali mabadiliko endelevu ambayo yatatokana na viongozi wa CCM.
Amesema umefika wakati wananchi kuamka na kudharau wote wanaowarubuni na kuwahadaa kuwa watawaletea maendeleo wakati ukweli ni kuwa, wanatafuta njia ya kukidhi njaa zao.
Aliyasema hayo juzi jioni wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa wakazi wa Kimara na kusisitiza atahakikisha wananchi wa Ubungo wananufaika na uwakilishi wake kupitia Ilani ya CCM na serikali ya awamu ya tano.
Alisema akipata ridhaa ya wananchi hao, atapigania uboreshaji wa miundombinu yenye tija, ambayo itatoa ajira nyingi kwa vijana.
Alisema Ilani ya CCM imeweka vipaumbele vingi katika huduma muhimu hivyo barabara ya Kimara Kilungule, Ubungo External zitakamilika na kujengwa kwa kiwango cha lami, sambamba na barabara ya Kimara hadi Changanyikeni.
Alisema mbali na uwezeshaji kuiuchumi uliopewa kipaumbele katika Ilani ya CCM, atahakikisha anatenga sh. milioni 10 katika kila kata kupanua wigo wa mikopo kwa vijana na wanawake.
Dk. Massaburi alisema anatambua kiu ya wananchi hao ni huduma bora za afya, elimu, maji na huduma zote muhimu, hivyo serikali ya CCM itasimamia ipasavyo na kuondoa sheria za halmashauri zinazokandamiza walala hoi.
Katika mkutano huo, Massaburi alipokea wanachama wapya kutoka vyama mbalimbali, akiwemo Katibu wa Uhamasishaji ACT, Mohamed Issa na Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Rungwe, Richard Mugogo.
Kwa upande wake, Mugogo alisema hakuna haja ya wanachama wa CHADEMA kuendelea kupoteza muda kushabikia chama cha wababishaji, kwa kuwa chama hicho si cha siasa tena bali ni kijiwe cha biashara na wajanja ndio wanaopiga dili.
Alisema Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe amepoteza mwelekeo wa chama na kwa wanasiasa makini, hawawezi kumlaumu kwa kuwa Mbowe hana sifa ya uongozi.
“Cha kujiuliza Mbowe ana CV gani zaidi ya kuwa DJ maarufu? Hivi mtu kama huyo ukiona anaongoza dili la biashara utashangaa nini na ndio maana hajutii unafiki wake kwa Lowassa pale alipomwita fisadi,” alisema.
Aliongeza kuwa kama Mbowe ana sifa za uongozi na kama hakuna maslahi kumleta Edward Lowassa CHADEMA, aeleze sababu za msingi za yeye kumpokea Lowassa na kuendelea kumpigania awe rais huku akijua hana sifa.

No comments:

Post a Comment