Tuesday 8 September 2015

VIJANA WAASWA KUWA MAKINI NA WAGOMBEA




NA WILLIAM SHECHAMBO
VIJANA wanaofuata mkumbo na ambao wanashabikia siasa katika siku za hivi karibuni hawana ufahamu wa elimu ya uraia, jambo linalotoa mwanya kwa wanasiasa uchwara kuwatumia kutimiza haja zao katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, imeelezwa.
Pia, baadhi ya vijana hao ambao kiuhalisia wako wengi na wanategemewa kushiriki kuchagua viongozi wa taifa, hawana utamaduni wa kusoma historia ya nchi ili kupata uwanja mpana wa kusikiliza, kujucha sera za wagombea zitakazokuwa na maslahi kwa taifa la Tanzania.
Hayo yalibainishwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni mojawapo nchini, ambapo alisema vijana wanapaswa kutambua kuwa walevi wa madaraka waliokuwepo mwaka 1995, wameongezeka.
Alisema hoja mojawapo inayotumiwa na baadhi ya vyama vya siasa kwenye kampeni zao mwaka huu, ni kuifufua Rasimu ya Katiba ya Warioba, ambayo ilisema lazima kuwe na serikali tatu ikiwemo ya Tanganyika, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema hoja hiyo ni ya kukataliwa kwa kuwa waasisi wa mataifa haya, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, waliwahi kukataa na kusema kuwa hakuna umuhimu wa kuwa na serikali ya tatu kwa sababu itaua hata hizi mbili zilizoko sasa.
Mhadhiri huyo alisema tangu mwaka 1964, kumekuwa na serikali mbili ambazo mpaka sasa zina kero zake, hivyo hata ikiongezeka ya tatu kero husika zitaongezeka.
Alisema vijana wangekuwa na utamaduni wa kusoma kitabu cha Mwalimu Nyerere kiitwacho Uongozi wetu na hatma ya Tanzania, ni mwongozo mzuri wa kufanya maamuzi kwenye uchaguzi.
Alisema mfano mzuri ni darasa analolifundisha UDSM, ambalo wanafunzi wa mwaka wa pili katika kozi ya sayansi za siasa, hawajui kirefu cha TANU wala kumjua Samora Machel, hali inayoonyesha dalili za vijana kuchukua maamuzi bila kujali mwafaka wa taifa kwa siku zijazo.
Katika kipindi hicho kilichoongozwa na mwandishi mkongwe, Makwaiya Kuhenga, vijana walitakiwa kuacha ushabiki wa vyama kwa kuwa endapo Tanganyika itafufuliwa, hakutakuwa na utaifa wa Tanzania na Watanzania watalaumiwa kwa kuibomoa nchi kwa mikono yao.

No comments:

Post a Comment