Na Mwandishi Wetu, Geita
MWENYEKITI wa CCM Mkoa
wa Geita, Joseph Musukuma, amesema ataziweka hadharani siri zote za mgombea
urais wa CHADEMA, Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward
Lowassa.
Amesema ana ufahamu uozo
mwingi wa Lowassa, kwani alikuwa miongoni mwa washauri wake 10, muhimu wakati
akitafuta wadhamini ndani ya chama na kwamba mgombea huyo hana sifa na hafai
kuongoza nchi.
Mbali na hilo,
amewashukia waliokuwa wenyeviti wa chama wa mikoa, Mgana Msindai (Singida) na
Hamis Mgeja (Shinyanga), kwamba anawafahamu vilivyo na wanasumbuliwa na
maslahi binafsi na si ya Watanzania.
Musukuma alisema hayo
katika mkutano wa hadhara, wakati akimnadi mgombea ubunge Jimbo la Geita,
Costantine Kanyasu (CCM), kwenye ufunguzi wa kampeni uliofanyika katika uwanja
wa Nyankumbu, mjini hapa.
“Napenda niwaeleze
Watanzania, hasa wale waliokuwa hawajui, nilikuwa miongoni mwa washauri 10
muhimu wa Lowassa wakati akitafuta wadhamini ndani ya chama ili ateuliwe kuwa mgombea urais, namjua na siri
zake zote nazijua, wala hakuna kitu ambacho anaweza kukificha,” alisema huku akishangiliwa na umati mkubwa wa
wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Alisema miongoni mwa
siri anazotarajia kuzitoa hadharani ni pamoja na mpango mkakati uliokuwepo
baada ya chama kukata jina la Lowassa kuwa ni kuhakikisha Balozi Amina Salum
Ali, anapitishwa kuwa mgombea urais wa CCM.
Msukuma alisema mkakati
huo ulipangwa, ili Lowassa ashinde kirahisi akiwa CHADEMA.
“Ni kweli wafuasi wa
Lowassa walikuwa wakinihusisha kuwa ni miongoni mwa wenyeviti wa mikoa wa CCM
waliotarajiwa kuhama kwenda CHADEMA, najua hata wao walijua mie ningehama
kwenda huko, lakini nimewaambia sihami
CCM.
‘’Kwa sababu namfahamu
vilivyo Lowassa, hivyo nawasubiri wafuasi wake waropoke, ili niweke siri zake
zote hadharani kwa Watanzania wasiojua ukweli, kwani nimekuwa nikihudhuria
vikao vyote muhimu vya kimkakati nyumbani kwake kabla hajahama kwenda huko
aliko,’’ alisema.
Alisema kiu ya
Watanzania katika uchaguzi wa mwaka huu ni kumpata mgombea wa CCM ambaye ni Dk.
John Magufuli na kwamba muda wa wapinzani kupewa ridhaa ya kuongoza dola
haujafika.
Akizungumzia makada
waliohama chama na kujiunga na CHADEMA, Musukuma, ambaye pia ni mgombea ubunge Jimbo
la Geita Vijijini, alisema anawasubiri kwa hamu Msindai na Mgeja wafike Geita
kuwalaghai wananchi.
Musukuma alisema
atajitolea kurusha helikopta angani na kuueleza umma namna Msindai alivyokuwa
mzigo ndani ya chama.
“Huyu bwana ni mzigo
kweli kweli, wala asiwadanganye Watanzania na kisa cha Mgeja kuhama ni kuwa
baada ya binti yake kukosa ubunge, huku akiwa ametumia zaidi ya sh. milioni 30,
alizotoa kama rushwa kwa wajumbe”, alisisitiza.
Alisema ana vielelezo
vyote, ikiwemo ujumbe mfupi wa maneno aliokuwa akitumiwa na Mgeja na baadhi ya
nyaraka zingine muhimu alizokuwa akitumia kuwarekodi pasipo wao kujua.
“Ninazo sms alizokuwa
akinitumia na pia ushahidi niliokuwa nawarekodi bila wao kujua,” alisema.
Katika hatua nyingine, Meneja
kampeni wa mgombea ubunge jimbo hilo, Ahmed Mbarak, alisema Dk. Wilbroad Slaa
ni mcha Mungu anayesimamia ukweli kutokana na hatua yake ya kuamua kujitenga na
mafisadi.
Akizungumza katika
mkutano huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, wilayani Geita, ambaye
alitangaza rasmi kuhama chama hicho kupitia mkutano huo, Bashiru Ally,alisema
vyama vya upinzani hapa nchini, ni mfano wa kampuni za watu binafsi, kwa
kuwa Lowassa amevamia kichaka asichokijua.
Kwa upande wake, mgombea
ubunge jimbo hilo, Constantine Kanyasu, akiomba kura, alisema anazijua kero
nyingi zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, ikiwemo maji na shida wanazopata
wachimbaji wadogo wa dhahabu na kwamba baadhi ameanza kuzishughulikia.
Njau
amdadavua Sumaye
KADA wa
CCM, Victor Njau, ameshangazwa na kitendo cha Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick
Sumaye, kuungana na Edward Lowassa, wakati alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha
Lowasa haingii Ikulu kwa njia yoyote ile.
Amesema
Sumaye alimtafuta mara kadhaa akitaka kukutana naye ili wapange mpango mkakati
wa kuhakikisha Lowassa hafanikiwi katika harakati zake za urais na baada ya
mazungumzo ya muda mrefu walikubaliana kukutana jijini Arusha
Njau
alitoa kauli hiyo jana katika uzinduzi wa kampeni za Jimbo la Arusha Mjini,
zilizofanyika katika viwanja vya Soko Kuu, jijini hapa.
Alisema
Sumaye alifunga safari kutoka Dar es Salaam na kuja Arusha kwa ajili ya kuonana
naye pamoja na watu wengine ambao hakuwataja.
Kwa
mujibu wa Njau, mapema mwaka huu, walikutana na Sumaye katika hoteli ya kitalii
ya Naura Spring, iliyopo jijini hapa, chumba namba 206, kupanga mpango mkakati
wa kuhakikisha Lowassa haingii Ikulu, lakini cha kushangaza hivi sasa
anamkumbatia na kumpamba kwa kila sifa kuwa ni kiongozi anayefaa kuwaongoza
Watanzania.
“Nina
ushahidi wa kutosha wa maandishi na sauti niliyomrekodi Sumaye akisistiza mambo
kadhaa tutakayoyafanya na wenzangu, ili kukamilisha mpango huu kwa namana yoyote
ile, lakini leo hii anaambatana naye. Hivi kweli huyu ni mzima au anataka
kucheza na akili za Watanzania?” alihoji.
Alisema
mara kadhaa Sumaye amekuwa akikaririwa na vyombo vya habari kuwa endapo CCM,
ingemteua Lowassa kugombea urais, angehama kwa sababu si msafi na ana tuhuma
nyingi.
Njau
ambaye ni mwanasheria wa kujitegemea, aliwataka Watanzania kutodanganywa na
mafisadi wala rushwa, wenye uroho wa kwenda Ikulu, kwani wakiwachagua watajutia
na kuwataka wananchi kumchagua Dk. John Magufuli kuwa rais wa awamu ya tano.
“Ndugu
zangu, tusimchague Lowassa, ana uroho wa madaraka… tumchague Dk. Magufuli kwa
kuwa ni mchapa kazi na kazi zake alizozifanya zinaonekana kwa macho. Mafisadi
wala rushwa wenye uchu wa madaraka tusiwape nafasi ya kwenda Ikulu kwa kuwa
hatujui lengo lao nini,” alisema.
Kuhusu
Godbless Lema, aliwataka wananchi wa Arusha kutomchagua kwa kuwa ni tapeli na
anatafuta nafasi hiyo kwa ajili ya maslahi binafsi.
Alisema
aliahidi kujenga machinga Complex, lakini mpaka sasa hakujenga wala hakuna hata
kiwanja alichonunua kwa ajili ya ujenzi huo.
Njau
alisema watamwuunga mkono mgombea wa CCM, watafanya kampeni kila kona usiku na
mchana, kuhakikisha mgombea huyo anapata ushindi mkubwa.
No comments:
Post a Comment