NA
MWANDISHI WETU, IRINGA
KAIMU
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, amesema
Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye na mwenzake aliyejiuzulu kwa kashfa ya
Richmond, Edward Lowassa, walikuwa mizigo ndani ya CCM na serikali yake.
Amesema
muda mfupi ujao, CHADEMA itajutia kuwakaribisha ndani ya chama hicho kwa kuwa
wanasiasa hao ni mizigo isiyobebeka.
Shaka
alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea ubunge wa Jimbo
la Isimani kwa tiketi ya CCM, William Lukuvi, uliofanyika kwenye kijiji cha
Kihorogota kilichoko jimboni humo.
Alisema uamuzi wa chama hicho kuwakaribisha viongozi hao haukufanyika kwa umakini kwa kutazama faida na hasara zinazoweza kusababishwa na wanasiasa hao, hususan kwenye nyanja ya kisiasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa Shaka, viongozi hao wamepoteza haiba na mvuto mbele ya jamii kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi na kujimilikisha ardhi bila kujali maslahi ya wanyonge.
"Nawapa pole sana viongozi wa CHADEMA na UKAWA kwa kukukubali kupokea viongozi mizigo, tena mizito kuliko lumbesa, hawabebeki na wamepoteza haiba na heshima mbele ya Watanzania," alisema.
Shaka alisema uongozi wa nchi unamhitaji mtu mwadilifu, mwenye hofu ya Mungu na anayeweza kusimamia maslahi ya wengi.
“Kiongozi
tunamyemhitaji lazima awe mwaminifu, mtiifu na mzalendo ambaye hana
shutuma wala tuhuma za ufisadi au ubadhirifu wa mali za umma,” alisema.
Alisema kuwa CCM inashukuru baada ya wawili hao kuhama na kujiunga na CHADEMA, chama ambacho kwa zaidi ya miaka saba kilikuwa kikiwanadi na kuwashitaki kwa wananchi kwamba ni mafisadi na hawastahili kupewa jukumu la kuongoza nchi kwa nafasi yoyote yenye maslahi ya umma.
Alisema
wanasiasa hao waliowahi kuaminiwa na kushika nyadhifa mbalimbali za juu katika
uongozi wa nchi, walikuwa wakikitia madoa chama na kwamba endapo wangeendelea
kubaki CCM, ingekuwa kazi ngumu kukinadi mbele ya jamii.
Aidha, Shaka aliwataka wananchi wa Isimani kutopoteza muda kwa kukishabikia chama cha siasa kama CHADEMA, ambacho hakina sera, malengo, dira, wala mipango na mikakati ya kushika hatamu za utawala wa dola na kusimamia maslahi ya umma.
Katika
hatua nyingine, Shaka aliponda sera ya majimbo inayotangazwa na CHADEMA na
kusema sera hiyo ni hatari kwa mustakabali wa amani ya nchi, umoja wa kitaifa
na utulivu kwa kuwa inaweza kuibua ubaguzi na ukabila ndani ya jamii.
“Ikataaeni CHADEMA na wagombea wake kwa sababu chama hicho kina sera ya majimbo inayoweza kuligawa taifa na kulijengea matabaka ya ukabila, ukanda na kuweka misingi isiyoheshimu utu, demokrasia, usawa na haki,” alisema Shaka.
Alisema katika Bara la Afrika lenye nchi 54 ni nchi sita tu ambazo zinatumia sera na mfumo wa majimbo, ambazo ni Nigeria, Afrika Kusini, Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na Comoro.
Shaka alisema kuna athari nyingi zinazoweza kuingia nchini kutokana na mfumo huo, ikiwemo mapigano ya wenyewe, ukabila ubaguzi na udini kama ilivyo kwenye baadhi ya nchi hizo.
Pia
aliwahimiza wananchi wa Isimani kumwuunga mkono na kumchagua mgombea urais wa
CCM, Dk. John Magufuli, ambaye ni kiongozi anayekubalika, kuheshimika na
kuaminika katika utendaji na usimamiaji wa majukumu aliouonyesha kwenye nafasi
mbalimbali alizoshika.
Shaka
aliwataka wana Isimani kuendelea kumchagua Lukuvi kwa kuwa ni kiongozi hodari,
mchapakazi, jasiri anayependa kuwajali watu , kuwathamini na kuwatumikia.
Mbali na kuwanadi Magufuli na Lukuvi, pia aliwaomba wakazi wa Kata Kihorogoto, kumchagua mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia CCM, Ponsiano Kalage kwa kuwa kufanya hivyo kutakamilisha dhana ya mafiga matatu, inayomaanisha rais, mbunge na diwani katika kila eneo la uchaguzi.
Shaka na msafara wake wako mkoani Iringa kwa ziara rasmi ya kampeni, ambapo anatarajiwa kuzunguka kwenye majimbo mbalimbali ya mkoa huo kabla ya kwenda mkoani Njombe kuendelea na ziara hiyo.
No comments:
Post a Comment