Monday 7 September 2015

DIALLO AWATAKA WAFUASI WA CHADEMA KUDAI MGAWO KUTOKA KWA MBOWE





BLANDINA ARISTIDES, MWANZA
MWENYEKITI wa CCM mkoani hapa, Antony Dialo, amewataka wanachama wa CHADEMA kuomba gawio la fedha kutoka kwa viongozi wao waliokiuza chama hicho kwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, ili nao wafaidike.
Alisema hayo jana, wakati akizindua kampeni za chama wilayani Ilemela, ambapo alidai kuwa chama hicho kwa sasa si mali ya wanachama bali ni mali ya Lowassa  na washirika wake ambao ni makapi yaliyotemwa na CCM.
“Kuna watu watatu ambao ni wajanja kwenye siasa hao ni Mtei (Edwin), Mbowe (Freeman) na Ndesamburo (Phillimon), hawa ni wafanyabiashara na tayari wamemaliza hiki chama, hivyo wanachama wawaombe gawio la fedha ili nao wafaidi,” alisema Dialo na kushangiliwa na umati wa wananchi uliojitokeza.
“Tunapokwenda kanisani tuwaombe CHADEMA ili ujinga  uwatoke,  maana hata wakiambiwa hawaelewi, wanabaki kung’ang’ana na kupambana na CCM, eti waitoe madarakani na ukiwauliza sababu ya kuwaondoa CCM hawana jibu, wanasema lazima tuiondoe tu jambo ambalo haliwezekani” alisema.
Naye Katibu wa CCMma Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, alisema alitegemea upinzani ndio ujenge misingi ya kuleta maendeleo lakini umegeuka kuwa vyama vya usanii na ndio maana upinzani walikosa mgombea urais.
Mtaturu alisema  kutokana na sababu hiyo, waliamua kumchukua mgombea kutoka CCM, ambaye hivi sasa anawatesa.
 “CHADEMA ni sawa na kupe ambaye aking’ang’ania kwenye ng’ombe hatoki hata kama ng’ombe atachinjwa yupo tu, watu wamekalia peoples …! wakati chama kilishauzwa na pesa ilishaliwa kitambo,” alisema Mtaturu.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Ilemela, Anjelina Mabula, alisema atahakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM anaisimamia na kuitekeleza kwa asilimia 100.
Alivitaja vipaumbele vyake kuwa ni afya ya mama na mtoto, elimu na miundombinu.


Mwalusamba: Hata waovu
wanafanya uamuzi mgumu 

NA SHAABAN MDOE, ARUSHA

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Godfrey Mwalusamba, amewataka wakazi wa Jiji la Arusha, kupingana na kauli ya uamuzi mgumu wa kuikataa CCM.

Alisema mfano unaotolewa na wapinzi haustahili kufuatwa, kwani utawapotosha.

Aidha, amesema hakuna mgombea urais mwenye sifa kama Dk. John Magufuli,  kutokana na uadilifu na uchapakazi alionao na aliouonyesha katika miaka ishirini aliyokaa serikalini.

Mwalusamba aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge na madiwani wa Jimbo la Arusha ulioongozwa Dk. Mary Nagu.
 
Alisema wapo watu ambao wanaweza kukubalika pindi wanaposema watachukua uamuzi mgumu,  hata kwa kuwaangalia usoni, akiwemo Dk. Magufuli, lakini siyo Lowassa, ambaye tayari ana makandokando mengi, ikiwemo kashfa ya Richmond iliyomfanya ajiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu.

Aliongeza kuwa mbali na kashfa hiyo ya Richmond pia mgombea huyo anatia shaka kutokana na kuchangiwa fedha na wafanyabiashara, jambo ambalo limekuwa likihojiwa atalipa fadhila gani iwapo atashinda.

Mwalusamba aliwataka wananchi kukaa na kutafakari na kisha kumwuuliza atawadhibiti vipi matajiri hao pindi watakapofanya ufisadi kwa ujasiri kutokana na michango yao kwake katika safari yake hiyo.

Alisema Dk. Magufuli hana deni na mtu yoyote aliyemchangia katika safari yake ya urais na kwamba mgombea wa CCM yupo na watu masikini, walio na mategemeo makubwa toka kwake.

Aliwataka wakazi wa Jimbo la Arusha kumchagua mgombea wa ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Philemon Mollel pamoja na madiwani wake, kwakuwa mgombea huyo ana uwezo wa kuwatumikia wananchi.

Dk. Mary aliwataka wananchi kutokubali kudanganywa tena na kumchagua mbunge wa upinzani, ambaye hajawasaidia lolote, zaidi ya yeye na familia yake.

Kwa upande wake, Mollel alisema iwapo atachaguliwa atahakikisha anajenga masoko yote, ambayo yatakuwa ya ghorofa ili wafanyabiashara wote wapate maeneo.

Alisema atahakikisha vikundi vya akina mama anavikopesha zana za kilimo na biashara alizonazo, ili ziwawezeshe kujikwamua kiuchumi.



Mabula azidi kutisha,
Wenje maji ya shingo

NA PETER KATULANDA, MWANZA 
ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Ezekia Wenje (CHADEMA), juzi aliandamana na wafuasi wake ,kitendo ambacho kimetafsiriwa kuwa alikuwa akiwaaga rasmi wananchi wa jimbo hilo, kutokana na mambo kuonekana kumeendea kombo.
Wenje aliandamana kabla ya kuzindua kampeni kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mbugani, baada ya kuahirisha uzinduzi huo mara tatu, akihofia kukosa watu  kama waliohudhuria mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM, zilizofanyika kwenye uwanja huo, mwishoni mwa mwezi uliopita.
Kama kawaida ya CHADEMA kukodi na kusomba watu kutoka wilaya na mikoa jirani, mkutano huo pia ulijaa watu kutoka nje ya Mwanza na kuhudhuriwa na vigogo wanane wa chama hicho.
Hata hivyo, wakati Wenje akizindua kampeni zake katika Kata ya Mbugani, mgombea ubunge wa CCM, Stanslaus Mabula, alimfungia kazi kwa mkutano mkubwa uliofanyika katika Kata ya Mabatini, ambapo  maelfu ya watu walifurika kwenye uwanja wa Kabengwe Hill, kusikiliza sera za CCM.  
Baada ya mkutano huo ulioanza saa 9:00 mchana hadi saa 12:00 jioni, maelfu ya wananchi na wana CCM walijibu maandamano ya Wenje kwa kuandamana kutoka Kabengwe Hill hadi kwenye ofisi za CCM, Wilaya ya Nyamagana na kusabaisha barabara kuu ya Mwanza-Musoma isipitike kirahisi kwa muda wa saa nzima.
Kufuatia hali hiyo, wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakirudi maeneo waliyotoka, roho ziliwauma kutokana na Wenje kuwatangazia kuwa Mabula ameahirisha mkutano wake baada ya kuambulia watu 16.
Wafuasi hao waliingilia kuvuruga maandamano hayo, wakiwatukana, kuzomea na kuwashambulia baadhi ya akina mama wanachama wa CCM, hali iliyosabisha vurugu za hapa na pale, ambazo zilidhibitiwa na polisi na kuwatia mbaroni baadhi ya vijana walioanzisha vurugu hizo.
Wenje akitumia muda mwingi kuwashambulia Mabula na Katibu wa UVCCM wa Wilaya ya Nyamagana, Hussein Khim.
Vigogo wa CHADEMA waliohudhuria mkutano huo ili kumsitiri Wenje ni pamoja na wagombea James Lembeli (Kahama), Suzan Lyimo (Viti Maalum), Ester Bulaya (Bunda), Vicent Nyerere (Musoma Mjini), Patrobas  Katambi (Shinyanga Mjini) na John Heche (Tarime Vijijini). 
Wengine pamoja na wagombea wa majimbo ya Misungwi ni Hamis Mgawo (Sengerema), Kalwinze Ngongoseke (Magu), Yusuph Kazi, Ester Matiko (Tarime Mjini) na Highness Kiwia (Ilemela).



No comments:

Post a Comment