Sunday, 11 October 2015
KAZI IMEANZA
Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameunda jopo la wataalamu wa fani na sekta mbalimbali kwa ajili ya kufanya mabadiliko makubwa serikalini, kuanzia siku ya kwanza atakayoapishwa kuwa rais, imefahamika.
Jopo hilo linaundwa na wataalamu wa ndani ya nchi na linahusisha wataalamu huru na magwiji wazalendo wa uchumi, biashara, utawala na sheria, kutoka kwenye taasisi za elimu ya juu, asasi zisizo za kiraia na sekta binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba, alisema Dk. Magufuli amefanya hivyo ili kuhakikisha kwamba anaanza kazi kwa juhudi kubwa, lakini pia kwa kutumia maarifa mapya.
Makamba alisema Dk. Magufuli amepanga kufanya mabadiliko ya kweli wakati wa utawala wake na kwamba njia ya kwanza ni kuhakikisha kila kitu kinakuwa kimewekwa vizuri tayari kwa maamuzi yake kama kiongozi mkuu.
Kwa mujibu wa Makamba, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, jopo hilo limepewa majukumu kumi ya msingi yanayotakiwa kufanyiwa uchambuzi na mapendekezo kuwa tayari kabla Dk. Magufuli hajaapishwa ili akiwa rais aanze kuyafanyia kazi haraka.
Mbunge huyo wa Bumbuli anayemaliza muda wake, aliyataja majukumu hayo kuwa ni: “Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo serikali itabana matumizi, ikiwemo manunuzi ya umma, posho za vikao na matumizi ya magari, ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.
“Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo serikali itaongeza mapato mara moja bila hatua za kibajeti kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.
“Kuchunguza na kupendekeza maboresho makubwa katika mfumo wa utendaji na utumishi na ufanisi katika serikali.
“Kupitia kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wa ngazi zote, wakulima, wafugaji na wavuvi iwapo unaweza kurekebishwa bila kuathiri bajeti ya serikali inayotekelezwa sasa,” alisema Makamba.
Katika maeneo hayo ya awali, Magufuli inaonekana anataka kuongeza mapato ya serikali ili iweze kutoa huduma zaidi kwa wananchi na pia kupunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima ili kutunisha mfuko wa serikali.
Masuala mengine ambayo jopo hilo la wataalamu litayaangalia kwa kina ni: “Kupitia sheria zote za nchi na kuorodhesha sheria ambazo zinapaswa kubadilishwa haraka ili kuharakisha mabadiliko ya kweli na ya haraka ambayo ameyaahidi kwa Watanzania.
“Kupitia na kuorodhesha masuala yote na kero zote zinazosubiri maamuzi ya serikali ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.
“Kupendekeza miundo na idadi ya wizara na kutengeneza rasimu za mikataba ya kazi kwa mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine wakuu atakaowateua mara baada ya kuapishwa.
“Kupendekeza njia za haraka za kumaliza kero za watumishi wa umma, hasa walimu, askari, madaktari na wauguzi, ili aanze nao kazi wakiwa na ari na morali ya kusukuma mabadiliko ya kweli.
“Kutengeneza rasimu ya mpango-kazi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi alizozitoa kwenye kampeni, hasa upatikanaji wa ajira kwa haraka na umeme wa uhakika.
“Kupendekeza muundo wa kitaasisi na utaratibu muafaka wa kutekeleza ahadi ya kutoa sh. milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa nchini,” alisema Makamba.
Kwa kutazama hadidu hizo za rejea kwa jopo alilounda Magufuli, inaonekana kuwa mgombea huyo wa CCM ana lengo la kupunguza ukubwa wa baraza lake la mawaziri kama anavyoahidi katika wakati huu wa kampeni.
Hadidu hizo za rejea kwa jopo zinaonyesha kuwa Magufuli pia anataka kuwa na suluhisho la kudumu la matatizo ya ajira nchini pamoja na suala la matatizo ya umeme yanayogubika Taifa hivi sasa.
Katika historia ya siasa za Tanzania, Magufuli atakuwa mgombea wa kwanza wa nafasi ya urais, ambaye ataingia madarakani wakati tayari akiwa na picha ya nini anatakiwa kufanya kuibadilisha nchi kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa ndani.
Baadhi ya wasomi kama Profesa Issa Shivji wamekuwa wakilaumu kwamba baadhi ya mipango ya kuikwamua Tanzania kutoka ilipo imekuwa haifanikiwi kwa sababu imekuwa ikiandaliwa na wataalamu kutoka nje ya nchi ambao hawajui maslahi ya taifa wala mazingira yake.
Wakati huohuo, Makamba jana alisema kwamba mgombea urais huyo wa CCM anazidi kukubalika kwa wapigakura hapa nchini kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele na kwamba chama chake kinajiandaa na ushindi.
Akitoa tathmini ya jumla ya kampeni, Makamba alisema hadi kufikia jana, Dk. Magufuli alikuwa ametembelea mikoa 22 na majimbo 203, huku akiwa amefanya mikutano mikubwa rasmi 240 na mikutano 865 ya kusimamishwa na wananchi njiani, hasa wananchi wa vijijini.
Pia, alisema Dk. Magufuli amekuwa akitumia usafiri wa barabarani, ambapo hadi jana alikuwa ametembea jumla ya kilomita 31,467 kwa barabara kuu, barabara za mikoa, barabara za wilaya, barabara za mlisho (feeder roads) na barabara za mijini na vijijini.
“Watu wengi wamekuwa wanajitokeza kwenye mikutano yetu. Lakini la muhimu zaidi ni hamasa na matumaini wanayopata baada ya kumuona jukwaani na kumsikiliza Dk. Magufuli.
“Wananchi wanapoondoka kwenye mikutano yetu ya kampeni wanakuwa wamepata fursa ya kumsikia mgombea wetu kwa kitambo kinachotosheleza, wamemuelewa, wameelewa sera za CCM na wameshawishika kukipigia kura CCM,” alisema.
Wakati zikiwa zimebaki takribani siku 13 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Makamba alisema CCM haitalewa na mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, badala yake imeongeza nguvu ya kukampeni ili kuongeza kura kwa Magufuli na wagombea wengine wa nafasi ya ubunge na udiwani kupitia chama hicho.
“Tunaingia katika ngwe ya mwisho ya kampeni zetu.Tangu kampeni zianze hadi sasa, ushindi wa CCM unajidhihirisha. Hata hivyo, katika kujihakikishia ushindi na kuongeza kiwango cha ushindi, katika ngwe hii ya mwisho, tumeanza kampeni nzito.
“Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ameanza ziara ya kampeni katika majimbo 64. Vilevile, viongozi wengine wa CCM, akiwemo Rais na Mwenyekiti wa CCM mstaafu Mzee Benjamin William Mkapa, nao wataanza safari za kuzunguka nchi nzima kumuongezea kura Dk. Magufuli na wagombea wetu wa ubunge na udiwani.
“Tutatumia helikopta nne kwa ajili ya shughuli hii. Dk. Magufuli na Samia wataendelea kutumia usafiri wa gari hadi mwisho wa kampeni, isipokuwa pale tu itakapokuwa hakuna budi,” alisema Makamba
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment