Sunday, 11 October 2015
DK SHEIN AVUNJA NGOME YA MAALIM SEIF PEMBA
Na Hamis Shimye, Mtambwe, Pemba
MGOMBEA urais wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amevunja ngome ya mpinzani wake, Maalim Seif Sharif Hamad katika kijiji cha Mtambwe, ambacho ndiko alikozaliwa kiongozi huyo, ambaye pia ni mgombea wa urais kupitia CUF na kuwaeleza wananchi wa eneo hilo kuwa maendeleo wanayoyaona kijijini hapo yameletwa na CCM.
Pia, amesema endapo wakimchagua na kuwa rais, atahakikisha anaendelea kuwapa kipaumbele wananchi wa eneo hilo, ambao wengi wao ni wavuvi na wakulima wa mazao mbalimbali ikiwemo larafuu, ambalo tayari ameshalipandisha bei.
Dk. Shein aliyasema hayo jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Makoongeni, uliopo wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba na kuhudhuria na mamia ya wananchi, ambao walimuahidi watampa kura nyingi za kishindo.
Abdallah Twahili Issa ni mmoja wa wananchi, aliyekuwa kivutio kikubwa katika uwanja huo, ambaye alibeba bango aliloliandika 'Kuhama Chama sio kuritadi', akiwa na maana kuwa kubadilisha chama sio kubadili dini.
Kitendo hicho kiliungwa mkono na wananchi wengi, ambao kila mmoja alianza kupiga yowe huku wakiimba kuwa hawaogopi chochote na ndio mwisho wa jeuri ya Maalim Seif katika kijiji hicho, ambako ndiko liliko jimbo la Mtambwe.
UHURU ilielezwa kabla ya Dk. Shein kufika kijijini hapo kuwa, wananchi hao walikuwa wanatishwa pamoja na kuchapwa bakora endapo watakwenda kwenye mikutano ya CCM au wakikutwa wamevaa nguo za Chama.
Twahili alisema Dk. Shein ni mkombozi wao na ndio maana wamekuja kwa wingi licha ya kuwepo kwa vitisho.
Alidai chini ya utawala wa Dk. Shein, kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 45, wanaiona barabara ya lami yenye kiwango cha juu.
Alisema Maalim alishawahi kuwa Waziri Kiongozi na hakufanya jambo lolote lile, na bado anawatisha na kuwaeleza CUF ndio chama chenye maendeleo wakati sio kweli, bali kimejaa ghiriba, ubabe na vitisho vya mara kwa mara.
Furaha ya wananchi hao ilionekana kumkuna Dk. Shein, ambaye muda mwingi alionekana akitabasamu na kusema amefurahishwa mno na wingi wa watu hao ambao aliwataka wasiogope na waende kupiga kura kwa wingi.
"Nawaomba nipeni kura nyingi mimi pamoja na mbunge, mwakilishi na diwani ndani ya jimbo hili tuweze kuleta maendeleo mengi zaidi ya haya," alisema.
Dk. Shein alisema kutokana na mwitikio huo kuwa mkubwa, amewaahidi kuwa endapo atachaguliwa tena, ataongeza bei ya karafuu kutoka 25,000 na kuwa juu zaidi kwa kuwa lengo lake ni kuhakikisha mkulima ndiye anayenufaika zaidi.
Alisema mbali ya kuinua zao hilo, pia atamalizia usambazaji wa nishati ya umeme ili kuhakikisha eneo nzima la Mtambwe linakuwa na umeme wa uhakika, ambao utawasaidia wananchi kufanya shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alisema wingi wa watu hao utamchanganya Maalim Seif
Balozi Idd, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kampeni wa CCM Zanzibar, alisema Maalim Seif alidai kuwa Dk. Shein hawezi kufika Mtambwe kwa kuwa ni ngome yake, lakini sasa amejidanganya na anaweweseka.
"Nimepewa taarifa za kuweweseka kwa Maalim Seif. Sasa namweleza kuwa hatukuja kutembea bali tumekuja kuchukua kura nyingi hapa kwao na wananchi wametueleza dhahiri kuwa hawampigii," alisema na kuamsha shangwe kwa mamia ya wananchi hao.
Alisema Maalim Seif hana huruma na matatizo ya wananchi wa Mtambwe, ndio maana hata yeye mwenyewe hakutaka kujenga nyumba nyumbani kwao ya kuishi kama walivyo viongozi wenzake.
"Eti anadai ataleta maendeleo hapa, mbona kashindwa kipindi alipokuwa Waziri Kiongozi? Na ataletaje maendeleo wakati hata nyumba ya kuishi yeye mwenyewe huku hana je, ataweza kweli kuwakumbuka? Yule ni mpita njia tu huku na mpeni kura nyingi Dk. Shein,"alisema.
Alisema watu wa Mtambwe na eneo zima la Pemba, waanze kubadilika na kuanza kukipigia kura Chama cha Mapinduzi kwa kuwa ndicho Chama sahihi chenye kuleta maendeleo ya kweli Zanzibar.
Alisema CCM ndiyo iliyoondoa michango yote ya shule na hivi sasa wanafunzi wanasoma bure hadi sekondari huku kina mama nao wakitibiwa bure.
"CUF wanajua wameshashindwa Zanzibar na ndio maana wanafanya mbinu mbalimbali ikiwemo kununua shahada, hivyo nawaambia mara hii hawatoki,"alisema.
Balozi Idd aliwataka wananchi wa eneo hilo wasiogope chochote, waende kupigakura na hakuna chochote watakachofanyiwa kwa kuwa serikali ipo na itawachukulia hatua wote wanaofanya fujo kipindi cha kupigakura visiwani humo.
Zomeazomea haipigi kura
Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Mohamed Abood, amesema uchaguzi ni sayansi na sio vurugu na anawashangaa CUF muda mwingi kutumia kuhamasisha kufanya fujo na sio kupigakura.
Alisema anataka kuwaeleza kuwa Pemba nzima ina asilimia 30 ya wapiga huku Unguja ikiwa na asilimia 70, hivyo alitamba kwa takwimu hizo na nguvu aliyekuwa nayo Dk. Shein na CCM, wanauwezo wa kupata kura zaidi ya asilimia 60.
Aliwataka wanaCCM wajitokeze kwa wingi kumpigia kura Dk. Shein pamoja na viongozi wengine wote walioomba kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa Unguja na Pemba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment