Monday 7 September 2015

NCHI HAIWEZI KUKABIDHIWA KWA WAPIGADILI-MWIGULU





NA MWANDISHI WETU
MGOMBEA ubunge Jimbo la Singida Magharibi, Mwigulu Nchemba, amesema nchi haiwezi kukabidhiwa mikononi mwa 'wapigadili'
Amesena suala la kuanzishwa kwa Mahakama Maalumu ya kushughulikia mafisadi na wala rushwa si jambo la mzaha na kwamba, binafsi atakua mmoja wa wabunge watakaosimama kidete kuhakiki mahakama hiyo ianzishwe.
Aidha, amesema wagombea wa upinzani hususan CHADEMA wanalazimisha kuingia Ikulu ili kulipa fadhila kwa matajiri wanaowapa fedha na kuzitawanya kila kona ili wachaguliwe.
Akihutubia umati mkubwa wa wananchi wa Iringa katika uzinduzi wa kampeni Jimbo la Iringa Mjini, alisema wapigadili wanataka kuuza rasilimali za nchi kwa wanaowafadhili.
Alisema mgombea urais wa chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Edward Lowassa ameendelea kuusaka si kwa ajili ya maendeleo ya watanzania bali kwa lengo la kuziuza rasilimali za taifa kwa marafiki zao.
"Nchi hii hatuwezi kuiacha kwa watu wanaoishi kwa kupigadili bila kujali maslahi mapana ya taifa. "Tusitoe fursa hiyo kwani endapo tutafanya hivyo tutajuta milele," alisema.
Kwa mujibu wa Mwigulu, mgombea urais wa chadema amekuwa akitajwa kwa muda mrefu kuhusika na kashfa mbalimbali za ufisadi.
Akizungumzia mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za ufisadi, alisema hilo si jambo la mzaha.
Mwigulu alisema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli anafahamika kwa kusimamia mambo mbalimbali yenye maslahi kwa umma.
"Binafsi nitakua miongoni mwa watakaosimamia hoja hii kuhakikisha mahakama hiyo inaanzishwa na wale wanaoibeza huenda wakawa ni miongoni mwa watu wa mwanzo kuburuzwa kwenye mahakama hiyo," alisema.
Akimzungumzia mbunge aliyemaliza muda wake jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mwigulu alisema kwa muda wote aliokaa madarakani ameshindwa kufanya jambo lolote la maendeleo.
Alisema muda wote aliokuwa bungeni amekuwa akizungumza mambo mbalimbali yasiyo na uhusiano wa maendelep katika jimbo lake.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo hilo, Frederick Mwakalebela, alisema iwapo atachaguliwa atatenga asilimia 10 ya posho yake kwa ajili ya maendeleo ya jimbo hilo.
Pia, atashughulikia kero mbalimbali ambazo Mchungaji Msigwa alishindwa kuzitatua muda wote aliokaa madarakani.

No comments:

Post a Comment