Monday 7 September 2015

TINGATINGA LABOMOA NGOME YA CHADEMA





NA SELINA WILSON, KILOSA
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli maarufu Tingatinga, amebomoa ngome ya CHADEMA wilayani Kilosa mkoani Morogoro kwa kumchukua Mwenyekiti wa Wilaya wa chama hicho, Selemani Simba.
Dk. Magufuli alimpokea mwenyekiti huyo pamoja na timu ya wananchama wa CHADEMA zaidi ya 50 akiwemo Katibu Mwenezi wa  Kilosa Kati, Mussa Ngongi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Kilosa, Simba alisema ameamua kujitoa CHADEMA, baada ya kuchoshwa na siasa za upinzani.
“Nimeamua kutoka CHADEMA baada ya kuona amepatikana mzalendo wa kweli Dk. Magufuli ambaye anatosha kuwa Rais wa Tanzania. CHADEMA hawana uzalendo wamesimamisha fisadi kuwa mgombea urais,” alisema.
Kwa upande wake Musa Ngongi aliyekuwa Katibu wa Jimbo la Kilosa wa CHADEMA, alisema amejiunga na CCM ili akafanye siasa safi na za kizalendo.
“Nitapinga nini wakati Dk. Magufuli ni mzalendo na ndio mgombea wa CCM, sioni sababu ya kuendelea kuwa mpinzani sioni cha kupinga,” alisema.
Alisema CHADEMA wameungana na Lowassa ambaye wakati wa safari za matumaini, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliwahi kusema kwamba anashangaa majambazi wanachomwa moto lakini Lowassa anachwa anatamba wakati yeye ni miongoni mwa mafisadi papa.
Ngongi alisema alisema kutokana na kitendo hicho amepoteza ujasiri wa kuendelea kubaki ndani ya CHADEMA hivyo, ameamua kujiunga na CCM kwa ajili ya kumpigania Dk. Magufuli na madiwani na wabunge wake.
Kwa upande wake aliyekuwa mpambanaji wa CHADEMA, Oliva Mollel, alisema amemua kuhama kwa kuwa hakuna matumaini kwenye chama hicho.
“Nilikuwa CHADEMA kiherehere. Tulikuwa tunapiga vita ufisadi lakini sasa kumekuwa na ufisadi ndani ya CHADEMA, nimeamua kutoka na sasa na naomba vijana wenzangu tupambane na ufisadi kwa nguvu zote tumchague Dk. Magufuli,” alisema.
Dk. Magufuli alifanya mikutano ya kampeni katika maenei ya Kimamba,Melela na  Sanganga  njia pande ya kwenda Mzumbe, ambapo aliwataka wananchi kuichagua CCM ili ifanye kazi ya kudhibiti mafisadi.
Alisema atahakikisha sekta za elimu, afya, maji, barabara zinaboreshwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

No comments:

Post a Comment