Monday 7 September 2015

DK. MAGUFULI: MAFISADI WAMETUTIA UMASIKINI


 
 Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. John Pombe Magufuli akiwasili kwenye uwanja wa Jamhuri tayari kuhutubia wakazi wa Morogoro mjini kwenye mkutano wa kampeni za CCM
Wananchi wakimkaribisha Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wakifurahia ujio wa mgombea wa Urais wa CCM Dk.John Pombe Magufuli.
Mwenyekiti wa CCM ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa CCM Ndugu Innocent Kalogeresi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Alhaji Abdalla Bulembo kwenye mkutano wa kampeni za CCM  uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri.

NA SELINA WILSON, MIKUMI
MAFISADI wachache wanaomiliki fedha nyingi wanatajwa kuwa ndio chanzo kilichoifikisha nchi kwenye umasikini na kwamba, wameanza kudhibitiwa ili kukomesha kabisa vitendo hivyo.
Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, alisema hayo jana wakati akihutubia wananchi wa Kijiji cha Ruaha katika Jimbo la Mikumi mkoani Morogoro, wakati wa ziara yake ya kampeni za uchaguzi mkoani humo.
Dk. Magufuli alisema kuna watu wachache  wenye hela nyingi wakati kuna Watanzania wengi hawana hela hivyo akipata ridhaa ya wananchi atasimamia na kuhakikisha fedha zinashuka kwenda kwa wananchi.
Alisema mafisadi wamekuwa wakitumia fedha zao hovyo na kwamba hata kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu wametumia mabilioni kununua mabasi na kufanya kila jitihada ili wachaguliwe.
“Siwezi kuacha hali hii iendelee. Mtu mmoja ananunua mabasi 30 kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Nipeni urais ili nikawashughulikie. Jina langu Magufuli, nipeni kura nikawafunge magufuli yangu ili nikomeshe ufisadi,” alisema.
Alisema kiu ya Watanzania walio wengi ni kutaka mabadiliko, lakini alionya wasikubali mabadiliko ya jazba na badala yake washirikiane naye kuleta mabadiliko bora.

CHADEMA MBWA MWITU
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli akiwa katika maeneo ya Mkamba na Ruaha aliwaponda CHADEMA na kuwafananisha na mbwa mwitu waliojivika ngozi ya kondoo.
“Mchungaji unachunga kondoo, ghafla akatokea mbwa mwitu naye akajiunga na kundi la kondoo na kukawa hakuna tofauti, kondoo wapo wanaendelea na mambo yao kama hakuna kilichotokea.
“Kwa mchungaji ukiona kondoo hawashituki, ujuea uliokuwa ukiwachunga hawakuwa kondoo bali ni mbwa mwitu waliojivika ngozi ya kondoo na ndio maana hawashangai kwa kuwa yule mbwa mwitu ni mwenzao,” alisema.
Alisema CHADEMA wamekuwa wakipiga vita ufisadi kila uchao na kuisema CCM kwamba inakumbatia mafisadi sasa CCM imewaondoa wao ndio wamewakumbatia na kumteua mmoja wao kuwa mgombea wao wa urais.
Dk. Magufuli alisema kwa kitendo hicho CHADEMA ni mafisadi na wanakumbatia mafisadi hivyo wananchi wasiwapigie kura na badala yake waichague CCM ili ilete mabadiliko bora.
Aliwataka wananchi kumpa rungu la kuwashughulikia mafisadi na kutoa mfano wa kitanda kikiwa na kunguni unatakiwa kuwua kunguni ikibidi wachomwe kwa maji ya moto na kitanda kiendelee kutumika.
Mapema akizungumza kabla ya kumkaribisha Dk. Magufuli kuzungumza na wananchi, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi, Abdallah Bulembo, alisema CCM makada wake haikumteua  Edward Lowassa wala Fredrick Sumaye kwa sababu ya kashfa za ufisadi.
Alisema CCM imeleta kada makini ,Mwanasayansi Dk. Magufuli ambaye ni mwiba kwa wapiga dili na ndio maana walivyoona hivyo wakakimbilia UKAWA 
KERO YA WAKULIMA WA MIWA
Wakati huo huo nyingine Dk. Magufuli alisema anatambua kero kubwa ya uhusiano mbaya kati ya wakulima wadogo, wakubwa na wenye viwanda vya sukari.
Alisema akiwa Rais atashughulikia kero hiyo ili wakulima wapate haki yao badala ya kudhulumiwa na walanguzi wanaotaka kunufaika huku wakulima wakishindwa
“Nimesikia kuna NGO’S zinadhulumu wakulima wa miwa. Ushirika unawanufaisha wa watu wa juu. Kwenye serikali ya Magufuli tutazimaliza kero hizo kwa kuwa tunataka watu wanufaike na kazi wanazofanya,” alisema.

BEI YA SUKARI KUSHUSHWA
Akizungumzia kuhusu bei ya sukari, alisema akiingia Ikulu atasimamia bei ya sukari ishuke hususan kwa eneo la Ruaha, ambapo ndipo kiwanda kilipo kwa kuwa hakuna wananchi wauziwe bei juu.
“Haiwezekani kiwanda kipo hapa halafu bei ya sukari iwe sawa na Dar es Salaam. Kwa nini isiuzwe kwa bei ya kiwandani. Niacheni hilo nitalimaliza,” alisema Dk. Magufuli huku umati wa wananchi ukimshangilia.
Dk. Magufuli alisema hakuna sababu sukari iende Dar es Salaam halafu ndio irudi kwa wananchi na kuuzwa kwa bei ya juu, lazima wananchi wanufaike na uwepo wa kiwanda.
Hatua hiyo ya Dk. Magufuli kuzungumzia kero hiyo ilitokana na malalamiko ya wananchi kwamba wanauziwa sukari kwa bei juu ya sh. 2,000 ambalo ndio kuna kiwanda cha sukari cha Ilovo.
Juzi akizungumza Mjini Ifakara, Mgombea ubunge jimbo la Kilombero, Aboubakar Asenga, alimuomba Dk. Magufuli akiingia madarakani ashughulikie kero ya bei ya sukari.

No comments:

Post a Comment