Sunday 13 September 2015

NAPE AMPASUA PASUA LOWASSA




NA MWANDISHI WETU
KATIBU wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa ni mchafu na kamwe hafai kuwa rais.
Amesema mbali na Lowassa na wenzake ambao wamekimbia CCM baada ya kukatwa kutokana na kukosa uadilifu, hana sifa za kuwa kiongozi na hafanani na mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli.
Nape, alipasua kuwa katika wizara zote alizowahi kuziongoza, Lowassa alitia doa kwa kukosa uadilifu huku akijilimbikizia mali na kusababisha changamoto kubwa kwa Watanzania.
Nape, alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Uwanja wa Mnazi Mmoja, mjini Lindi.
Alisema kukatwa kwa Lowassa kwenye mbio za kuwania uteuzi ndani ya CCM,kulitokana na kuwa na makandokando mengi ikiwemo tuhuma za rushwa na ufisadi.
“Tulimuondoa Lowassa kwa sababu kila nafasi aliyopewa katika nchi hii alitumia vibaya madaraka yake, sasa huyo mtu anafaa kuwa rais?” Alihoji Nape.
Alisema Lowassa alianza kutumia vibaya madaraka alipokuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Mikutano cha Arusha, (AICC), Waziri wa Mifugo, Waziri wa Ardhi na hata alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, mambo yalikuwa yale yale hadi akalazimishwa kujiuzulu.
“Huyu akiwa Waziri wa Mifugo alihamisha ng’ombe katika ranchi za taifa na kujimilikisha kwa kuzihamishIa kwenye ranchi yake iliyoKo mkoani Tanga.
“Lowassa hafai, ana ranchi kubwa, kachukua ng’ombe wetu kawapeleka kwake na anawakagua kwa helikopta. Leo ndio anataka tumpe urais ili afanye nini,” alihoji Nape huku akishangiliwa na umati wa watu uliofurika kusikiliza sera za CCM.
Kuhusu mchakato wa kumpata mgombea urais, Nape alisema Lowassa asipotoshe umma kuwa hakujadiliwa.
Alisema Lowassa alijadiliwa na wajumbe walitumia muda mrefu kumjadili kabla ya kumuengua kwa kuwa hakuwa msafi na hafai kuwa rais wa nchi.
“Nasema kwa niaba ya CCM, Lowassa hafai hata kidogo kuwa rais kutokana na rekodi yake mbaya katika utendaji wa kazi. Nilimshangaa akichukua fomu wakati ni mchafu.
“Naomba huyu babu anayejipitisha kwenu kuwa anataka kwenda Ikulu, hafai hata kidogo na hata afya yake ina mgogoro, hata kunyanyua mguu mmoja kucheza muziki jukwaani kama Dk. Magufuli hawezi,” alisema Nape.
Nape alitumia fursa hiyo kuonya kuwa CCM itashughulika na vibaka wote walioandaliwa na UKAWA kufanya vurugu siku ya uchaguzi.
Huku akionekana kuchukizwa, Nape alisema wana taarifa kuwa UKAWA wamejipanga kuvamia vituo vya wapigakura na kwamba, CCM haitakubali hilo litokee, hivyo watakula sahani moja.
Pia, amemtaka Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, kuacha kuropoka katika majukwaa kwa kuisema vibaya serikali, vinginevyo ataanika uchafu wake kwa Watanzania.

No comments:

Post a Comment