NA MOHAMMED ISSA
MGOMBEA mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassani,
leo anatarajiwa kupata mapokezi makubwa katika wilaya za Ilala, Temeke na
Kinondoni mkoani Dar es Salaam, ambapo atakuwa na mikutano kwa siku tatu.
Samia atawasili mkoani hapa akitokea Dodoma ambapo atafanya
mikutano ya hadhara kwenye majimbo 10 na kata 102.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Mkoa wa Dar es Salaam,
Juma Simba ‘Gadafi’ alisema jana kuwa Samia atafanya mikutano ya hadhara kwenye
majimbo na kata ikiwa ni pamoja na kuwanadi wagombea ubunge na udiwani.
Alisema mgombea mwenza ataanza ziara yake katika jimbo la
Kigamboni ambapo atakuwa na mkutano mkubwa wa hadhara katika Kata ya Somangira.
Gadafi alisema katika mkutano huo, Samia atamtambulisha
mgombea ubunge wa jimbo hilo na madiwani wa Kigamboni ambapo pia atawakabidhi
Ilani ya Uchaguzi ya Chama.
Alisema baada ya kumalizika kwa mkutano huo, mgombea mwenza
atakuwa na mkutano mwengine mkubwa katika uwanja wa Ninja uliopo Mbangala Charambe.
Gadafi alisema saa 10, Samia atafanya mkutano mwingine
mkubwa jimbo la Temeke Kata ya Buza, ambapo atamnadi mgombea ubunge wa Temeke
na madiwani wa jimbo hilo.
Alisema kesho, Samia ataendelea na ziara yake katika Wilaya
ya Kinondoni ambapo ataanzia jimbo la Kibamba na kwamba atamnadi mgombea ubunge
na madiwani wa jimbo hilo na kuzungumza na wananchi.
Gadafi alisema baada ya mkutano huo, mgombea mwenza atakuwa
na mkutano mwingine mkubwa katika Uwanja wa Barafu Mburahati ambapo atamnadi
mgombea ubunge wa jimbo la Ubungo na madiwani wake.
Alisema baada ya mkutano huo kumalizika, Samia atafanya
mkutano mwingine Mwananyamala kwa Kopa na kumalizia jimbo la Kawe ambapo
mkutano mkubwa wa hadhara utafanyika Msasani.
Gadafi alisema kesho kutwa, Samia atatembelea Wilaya ya
Ilala ambapo atakuwa na mkutano wa hadhara katika viwanja vya Posta Amana na
baadaye atafanya mkutano jimbo la Segerea na kuhitimisha mkutano wake katika
jimbo la Ukonga Kata ya Majoe.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano
hiyo ili kusikiliza sera mzuri za Chama.
Gadafi aliwahakikishia wanancchi na wana-CCM kwa ujumla
kuwa Chama kitafanya kampeni za kistarabu na kwamba kitapata ushindi mkubwa
katika uchaguzi mkuu wa 0ktoba 25, mwaka huu.
Alisema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, wabunge,
wawakilishi na madiwani watapata ushindi wa kutisha.
No comments:
Post a Comment