NA EPSON LUHWAGO, MTERA
SERIKALI ijayo ya CCM inakusudia kuanzisha halmashauri
katika jimbo la Mtera mkoani Dodoma ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na
kupeleka madaraka karibu na wananchi.
Sambamba na halmashauri, pia kiwanda cha kutengeneza mvinyo
kitajengwa ili kuongeza thamani ya zabibu zinazozalishwa katika jimbo hilo.
Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan,
alisema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika Kijiji cha Mlowa
Barabarani.
Samia alitoa ahadi hiyo kutokana na ombi la Mbunge wa
Mtera, Livingstone Lusinde, aliyesema Wilaya ya Chilonwa ni kubwa jambo
linalokwamisha maendeleo kwa kuwa kuna halmashauri moja tu ya wilaya.
Pia, alisema wananchi wa Mtera ni wakulima wazuri wa zabibu,
lakini wanaziuza kwa hasara kutokana na
kutokuwa na kiwanda cha kutengeneza mvinyo.
Akijibu maombi hayo, mgombea mwenza alisema serikali ijayo
inatarajia kufanya hayo yote ili kuwezesha utoaji wa huduma. Alisema suala la
kiwanda cha kutengeneza mvinyo liko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka huu.
“Hili suala la kiwanda halina mjadala kwa sababu Ilani ya
Uchaguzi inalizungumzia. Tutahakikisha kiwanda cha mvinyo kinajengwa ili
kuongeza thamani ya zao la zabibu. Kiwanda hiki kitawezesha kuwepo kwa soko la
uhakika la zabibu zenu,” alisema.
No comments:
Post a Comment