NA SELINA WILSON, MTWARA
MGOMBEA wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema akichaguliwa kuwa Rais, serikali
itaongeza makusanyo ya kutoka sh. bilioni 900 hadi mara mbili zaidi.
Amesema serikali ya awamu
ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, ilipoingia madarakani ilikuwa inakusanya
sh. bilioni 300 kwa mwaka na sasa imefikia sh. bilioni 900, hivyo ataongeza
mara mbili zaidi.
Dk Magufuli alisema hayo
jana mjini Mtwara mbele ya umati wa wananchi waliofurika ndani na nje ya Uwanja
wa Mashujaa.
Alisema anajua makusanyo
yapo, lakini baadhi ya watendaji wanahujumu, hivyo atahakikisha anasimamia
vizuri na kudhibiti uvujaji wa mapato kwa kuwa na uzoefu wa miaka 20 serikalini
na anajua kila kona.
Aliwataka wakazi wa Mtwara
kumchagua awe Rais wa awamu ya tano kwa kuwa ana malengo ya kuleta maendeleo
kwa kutumia wawekezaji wa ndani na nje kwa kujenga viwanda na kumaliza tatizo
la ajira kwa asilimia 40.
Pia, Dk. Magufuli alisema
wazawa watashirikishwa kikamilifu katika kuendeleza rasilimali za gesi, mafuta
na madini ili nao wafanye biashara bila kubaguliwa.
Alisema serikali yake
itajenga mtandao wa reli ya kisasa kutoka Mtwara/Songea mpaka Mbamba Bay na
itaunganishwa na Liganga na Mchuchuma ili watu wafanye biashara na atapanua Bandari
ya Mtwara ili mizigo ya Malawi na Zambia itumie bandari hiyo na kusafirishwa
kwa reli hiyo bila kupitia Dar es Salaam.
MABADILIKO
YASIYO NA MPANGO
Katika hatua nyingine, Dk.
Magufuli aliwataka wananchi wasikubali kurubuniwa na matapeli wa kisiasa ambao
wamekuwa wakiongopa kwamba wanaweza kuleta maendeleo kwa siku moja.
Aliwafananisha wanasiasa
hao sawa na wanaume wanaowarubuni wasichana kwamba wakikubali kuchukuliwa nao
watapata kila kitu wakati hata kitanda hana.
Dk. Mafuguli alisema
wamekuwa wakisema kuwa CCM imechoka ing`olewe ili wao walete mabadiliko jambo
ambalo si sahihi kwa kuwa mabadiliko bora yanaweza kupatikana ndani ya CCM.
Aliwataka wananchi
wasikubali kutupa kitanda chenye kunguni na badala yake wasafishe kwa kuwaua
kunguni na kuendelea kulalia kitanda.
“Ndugu zangu mimi ndio
kiboko yao. Nimegombea ili nisafishe kunguni. Mimi ndio maji ya moto kwa ajili
ya kuwaua kunguni wote kwenye kitanda CCM, Msikubali mabadiliko yasiyo na
mpango,” alisema.
Alisema Tanzania inahitaji
mabadiliko na mabadiliko hayo yataletwa na yeye na ndio maana alipoteuliwa tu,
mafisadi wanaochafua chama wameanza kukimbia wenyewe.
Dk. Magufuli ambaye
alipanda jukwaani saa 10:12 jioni, alisema hatasahau mapokezi hayo na anaamini
kwamba umati huo unaonyesha dalili kwamba wanataka mabadiliko na yeye amegombea
urais kwa ajili ya kuleta mabadiliko bora.
Kwa upande wa majeshi, alisema
anakerwa na uvamizi kwenye vituo na kuhoji majambazi na kuhoji mbona hawavamii
kambi za JWTZ wala Ukonga FFU.
Dk. Magufuli alisema anajua
wanaogopa cha moto, hivyo alisisitiza kwamba kwenye serikali yake anataka
kujenga nidhamu ya jeshi la polisi.
Pia, alisema serikali yake
itaangalia walemavu wa aina zote ili
kuhakikisha wanapata haki zao na kuendesha maisha yao.
LUKUVU ASEMA ALIPITA MCHUJO
HALALI
Awali, Mjumbe wa Kamati
Kuu, William Lukuvi aliwapongeza wananchi wa Mtwara kwa kufurika kwa wingi
katika Uwanja wa Mashujaa kumpokea na kumsikiliza mgombea wa CCM Dk. Magufuli.
Akimtambulisha Dk.
Magufuli, Lukuvi alisema ni kada aliyepita kwenye mchujo wa machakato halali wa
uchaguzi wa ndani ya CCM na kupitishwa kwa kura nyingi.
Aliwataka wananchi wa
Mtwara wahoji, wagombea wengine walipita kwenye mchujo gani na waeleze katika
mchakato walikuwa wangapi mpaka akateuliwa mmoja.
Lukuvi alitoa mfano wa kada
wa CCM aliyekatwa na kutimkia UKAWA kwamba aligombea nafasi hiyo kwa kushindana
na nani na kwenye mchujo walikuwa wangapi.
Alisema Dk. Magufuli ni
kiongozi aliyefanya kazi ndani ya serikali na kazi yake imeonekana nchi nzima
na ndio maana CCM imemsimamisha baada ya kushinda kwa vigezo mbalimbali ndani
ya Chama.
MAGUFULI
MWADILIFU – MPANGU
Kada wa CCM na Katibu Mkuu wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu
Tanzania, Amon Mpanju, amesema Tanzania inahitaji Rais makini, muadilifu na
mwenye kuchukia ufisadi.
Mpanju akihutubia mamia ya
wananchi wa Mtwara Mjini, alisema vijana wasikubali kupotoshwa wakachagua Rais
fisadi ambaye ameghubikwa na kashfa.
Alisema wakitoa fursa kwa
mtu wa aina hiyo watatengeneza serikali itakayoongozwa na genge la mafisadi, hivyo
chaguo sahihi ni Dk. Magufuli wa CCM.
Katika hatua nyingine, alimpongeza
aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kwa kuwa mzalendo wa kweli
na kuzungumza hadharani juu ya ufisadi wa mgombea urais wa wa UKAWA, Edward
Lowassa.
Alisema kitendo cha Dk.
Slaa kueleza kujitenga na siasa kutokana na CHADEMA kumsimamisha mtu
anayetuhumiwa kwa ufisadi kuwania urais ni kitendo cha kishujaa na kizalendo.
Katika hatua nyingine, Mpanju
alivionya vyombo vya habari vinavyotuhumiwa kununuliwa na wanasiasa ambavyo
vimekuwa vikiandika habari za upendeleo kwa baadhi ya wagombea na wakati
mwingine kupotosha wananchi.
MURJI ATAMBA KERO SASA BASI
Akizungumza katika mkutano
huo, mgombea ubunge wa Mtwara Mjini, Hasnein
Murji, alisema kero kubwa za wana Mtwara ni ajira kwa kuwa baadhi ya
wenye viwanda hawatoi ajira na badala yake wanakwenda na watu wao.
Murji alisema baadhi ya watu
wanaoporwa ardhi yao na wawekezaji bila kulipwa chochote jambo ambalo limekuwa
kero kubwa.
Alisema ana amini chini ya
utawala wa Dk. Magufuli ambaye hana kashfa ya ufisadi, anajua changamoto zote
zitapatiwa majibu na wananchi watanufaika na rasilimali zao.
Akijibu kero hiyo, Dk.
Magufuli alisema sheria za ardhi zipo wazi, hakuna mwekezaji au serikali
inayoruhusu kuchukua ardhi ya mtu bila kulipwa fidia. Alisema suala hilo
amelichukua na atalifanyia kazi.
Pia, Dk. Magufuli
aliwapokea wanachama 51 kutoka CHADEMA wakiongozwa na aliyekuwa Katibu
Mwenezi wa Wilaya ya Mtwara, George Makota.
Akizungumza kwa niaba ya
wenzake, Makota alisema wameamua kuondoka CHADEMA baada ya kuona hakuna
maendeleo na maendeleo ya kweli yapo ndani ya CCM.
APAGAWISHA NA YAMOTO BAND, CHEGE
Dk. Magufuli katika
kujinadi kwa wana Mtwara aliwapagawisha pale alipopanda jukwaani na kuanza
kucheza sambasamba na vijana wanaounda kundi la Bendi ya Yamoto .
Aliamsha kelele za shangwe
pale alipopanda jukwaani kwa mara ya pili na kucheza wimbo wa Mkono Mmoja wa
nyota wa kundi la Wanaume Family, Juma Said (Chege).
Huku akionyesha kuendana na
midundo na mziki uliokuwa ukiimbwa na kusababisha wanananchi waliofurika katika
Uwanja wa Mashujaa kumshangilia vilivyo.
Yamoto Bendi ilianza kutumbuiza
wakati Dk. Magufuli akiingia uwanjani hapo na ghafla alipanda jukwaani na
kuanza kuimba na kucheza wimbo wa Baba Huyoooo.
Wimbo huo ambao ulikuwa
ukiimbwa na msanii wa kundi hilo, Maromboso umeingizwa maneno yanayomtaja Dk.
Magufuli na kuisifia CCM.
Kutokana na mvuto wa wimbo
huo na kitendo cha Dk. Magufuli kucheza, wananchi waliofurika uwanjani hapo
wazee kwa vijana walionekana wakicheza na kushangilia.
Akicheza wimbo wa Chege,
Dk. Magufuli aligeuza kofia yake na kuanza kucheza huku akiweka mkono mmoja juu
ili kwenda pamoja na mashairi ya wimbo huo.
Awali akizungumza katika
mkutano huo, Dk.Magufuli alisema atadhibiti wizi wa kazi za wasanii na uonevu
wa kila aina dhidi yao.
Dk. Magufuli alisema
atanzisha mfuko kusaidia wasanii ili waweze kunufaika na kazi wanazofanya.
No comments:
Post a Comment