![]() |
Asumpta Mshana |
![]() |
Angella Kairuki |
NA EPSON LUHWAGO, MPWAPWA
WAZIRI Mkuu wa zamani na mgombea urais
wa CHADEMA, Edward Lowassa, amezidi kushambuliwa na safari hii ameelezwa kuwa
ni mtu asiyejua sheria.
Wakati mwanasiasa huyo akichambuliwa
hivyo, mbunge wa zamani wa Nkenge, Asumpta Mshama, amesema anajiandaa
kumfikisha Lowassa mahakamani kumtaka aeleze alipo aliyekuwa Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) Dk. Daudi Ballali.
Naye Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM,
Samia Suluhu Hassan, alisema wapinzani wanafanya mchezo wa kuigiza kwani
walichokifanya kwa kumsimamisha Lowassa kuwa mgombea ni sawa na kumsilimisha
mtu asubuhi na jioni kumteua kuwa sheikh wakati hajui hata aya moja ya Kurani.
Akizungumza juzi wakati wa mkutano wa
kampeni wa mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika wilayani
Mpwapwa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Angellah Kairuki,
alisema mwanasiasa huyo ameonyesha kuwa ‘mbumbumbu’ wa sheria.
Alisema hayo kutokana na kauli
aliyoitoa Lowassa hivi karibuni kwamba akichaguliwa kuwa Rais atahakikisha
anamtoa gerezani mwanamuziki maarufu, Nguza Viking, anayetumikia kifungo cha
maisha kutokana na makosa ya kulawiti.
“Huyu ni mtu anayetaka kuwa Rais wa
Tanzania, lakini hajui sheria. Anasema atamtoa Babu Seya (Nguza) iwapo ataingia
Ikulu, ina maana kuwa ataingia kuvunja sheria na kuingilia mihimili mingine ya
dola. Hafai kabisa kuwa Rais,” alisema.
Alisema Tanzania inaongozwa na utawala
wa sheria, lakini inashangaza mtu anayetaka kuwa kiongozi wa nchi kutoheshimu
utawala bora.
Kwa mujibu wa Angellah, Watanzania
wanapaswa kuwa macho na wanasiasa ambao wana uchu wa madaraka na wanaanza kutoa
vitisho kuwa wakiingia Ikulu, watavunja sheria.
“Kila wizara aliyoongoza alisababisha
matatizo na migogoro mingi. Hatuna muda wa kuyazungumza mabaya yake lakini
niseme inatosha kwani hata Wizara ya Ardhi ambako mimi ni Naibu Waziri alifanya
madudu kibao,” alisema.
Angellah alisema Watanzania wanapaswa
kuichagua CCM kwa kuwa ina mipango na malengo mazuri kwa ajili ya kuwaletea
Watanzania maendeleo, tofauti na wapinzani ambao wanasema sera yao kubwa ni
kuitoa CCM madarakani.
“Hivi leo mahitaji ya Watanzania ni
kuing’oa CCM madarakani? Wananchi wanahitaji maji, umeme, afya na barabara
ambavyo ni ahadi na mipango ya CCM. Chagueni CCM ndiyo mpango mzima,”
alisisitiza.
ASUMPTA ACHARUKA
Wakati Angellah akimwonyesha Lowassa
hajui sheria, Asumpta Mshama alisema anajiandaa kumfikisha mahakamani kwa kauli
zake za utatanishi kuwa atamleta Ballali Tanzania.
“Sisi tunajua kuwa Ballali alishakufa,
lakini inashangaza kuona kuwa mtu anasema atamleta. Hii ina maana kwamba
Ballali yuko hai, hivyo tunataka atueleze aliko.
“Huwezi kusema kitu kama hiki kama huna
uhakika. Inaonekana mwenzetu anajua aliko, sasa amlete na asipomleta nitakwenda
mahakamani kumtaka afanye hivyo. Natafuta mwanasheria ili kufungua kesi,”
alisema katika mikutano iliyofanyika juzi na jana Mpwapwa na Kibakwe.
Sambamba na hilo, Asumpta alisema
Watanzania wanapaswa kuichagua CCM kwa kuwa haina ukanda wala udugu tofauti na
CHADEMA ambacho ni chama cha kifamilia.
Kwa mujibu wa Asumpta, CHADEMA
ilianzishwa kama chama cha kufa na kuzikana kwenye ukoo wa Mzee Edwin Mtei, lakini
baadaye alikigeuza kuwa chama cha siasa.
“Alipoamua kustaafu alimwachia Freeman
Mbowe ambaye ni mkwe wake. Mzee Ndesamburo ana mtoto, Lucy Owenya, ambaye ni
mbunge na Grace Kiwelu pia ni mke wa mtoto wa Ndesamburo.
“Kama haitoshi, viongozi wengi wa
CHADEMA wanatoka kaskazini. Hata waliohamia juzi (Lowassa na Waziri Mkuu wa
zamani Frederick Sumaye) ni wa kutoka kaskazini. (Lawrence) Masha naye ambaye
amejiunga na chama hicho mke wake ni wa kutoka Kilimanjaro. Watanzania hatutaki
masuala ya ukanda kwani sote ni wamoja,” alisema.
No comments:
Post a Comment