Thursday, 3 September 2015

LOWASSA APINGWA KWA MAANDAMANO






Yafanyika Dar es Salaam, Shinyanga na Mwanza
Ni baada ya Dk. Slaa kufichua uoza wa CHADEMA
Mbatia aomba watuhumiwa ufisadi wasamehewe

NA WAANDISHI WETU
WAFUASI wa CHADEMA katika maeneo mbalimbali nchini, wameanza kufanya maandamano ya kumng’oa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa.
Maandamano hayo kushinikiza Lowassa, ambaye amepewa nafasi ya kugombea urais na vigogo wa CHADEMA, yalianza jana katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga na Mwanza.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kufichua uozo, mchezo mchafu na usanii unaofanywa ndani ya chama hicho.
Dk. Slaa alitangaza namna Lowassa alivyoingia ndani ya CHADEMA katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika hoteli ya Serena, ikiwa ni karibu miezi miwili tangu aliposusia uteuzi wa mgombea urais wa CHADEMA.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Lowassa hastahili kuwa rais wa nchi kwa kuwa ni mchafu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ufisadi ambao mara nyingi alimkabili bayana na kumweleza msimamo wake.
Katika mikoa hiyo, mamia ya wafuasi wa CHADEMA wakiwa na mabango na bendera za chama hicho, waliandamana kupinga Lowassa kupewa nafasi hiyo na kutaka aondolewe haraka.
Aidha, wakati maandamano hayo yakianza kushika kasi, viongozi wa CHADEMA na UKAWA wameanza kuweweseka ambapo, jana, James Mbatia, aliibuka na kupendekeza watuhumiwa wa ufisadi wasamehewe.
Pia, alisema yuko tayari kushiriki kwenye mdahalo kwa niaba ya Lowassa na kujibu tuhuma za ufisadi, jambo ambalo linadhihirisha ahadi ya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kuanzisha Mahakama Maalumu itakayohusika na kesi za ufisadi na rushwa, imeanza kuwatisha.
Hata hivyo, wasomi na wanasiasa maarufu nchini wameonya kuwa kwa mambo yanavyokwenda CHADEMA inaelekea kujizika yenyewe.
Jijini Dar es Salaam, maandamano hayo yalianza saa 7:15 mchana katika eneo la Morocco, ambapo wanachama hao wakiwa na mabango na bendera waliandamana wakitaka kwenda Makao Makuu ya CHADEMA, Kinondoni.
Wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe wa kutaka Lowassa afukuzwe na Dk. Slaa arejeshwe ndani ya CHADEMA, wafuasi hao pia walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali.
Walisema hawawezi kukubali Dk. Slaa kuondoka kirahisi ndani ya chama alichokijenga kwa miaka mingi kwa sababu ya Lowassa, ambaye anatuhumiwa si msafi.
‘Tunataka CHADEMA ya Slaa na si CHADEMA ya wapiga dili’, Tunamtaka Slaa wetu hatumtaki fisadi wenu’, ‘Sumaye rudisha mashamba ya wanyonge’, ‘Damu ya Josephina itawatafuna’ na ‘Gwajima Jehanam inakuita,’ yalisomeka baadhi ya mabango hayo.
Aidha, wanachama hao walieleza kuwa wamesikitishwa na hatua ya baadhi ya viongozi wa CHADEMA kumkashifu Dk. Slaa, badala ya kukiri udhaifu na madudu waliyoyafanya.
Walisema misingi bora ya utawala na demokrasia iliyowekwa na Dk. Slaa sasa inabomolewa na watu wasio wasafi na makapi kutoka CCM, jambo ambalo linatia uchungu na halistahili kupewa nafasi.
Maria Moyo, alisema tangu kuingia kwa Lowassa chama hicho kimepoteza demokrasia na haki miongoni mwa wanachama huku tuhuma nyingi zikikiandama.
Naye Raphael Andrew, alisema kwa sasa CHADEMA imepoteza mwelekeo kwani hakuna sera za maana za kuwaeleza wananchi zaidi ya ubabaishaji na hilo limetokana na kuingizwa watu wenye makandokando.
Alionya kuwa ni jambo la kushangaza kwa mgombea kuomba ridhaa ya wananchi akipanga kuvunja sheria za nchi na kuingilia kazi za mihimili mingine.
Hivi karibuni, Lowassa aliwaeleza Watanzania kuwa akifanikiwa kuingia Ikulu atawatoa watuhumiwa wa ugaidi na mwanamuzi Nguvu Viking (Babu Seya) na wanawe wanaotumikia vifungo vya maisha kwa makosa ya ubakaji na ulawiti watoto.
"Leo unatuambia atamtoa Babu Seya gerezani, huko ni kuvunja sheria na tunachotaka ni sera nini atatufanyia watanzania… huyu hatumtaki na badala yake babu Slaa arejee kujenga demokrasia ya kweli," alisema.
Aliongeza kuwa Lowassa anakipa CHADEMA wakati mgumu katika kuomba kura hivyo, kwanza anatakiwa kujisafisha mwenyewe na makapi aliyohama nayo kutoka CCM ndipo aombe kura kwa watanzania.
Kabla ya maandamano hayo kufika mbali, polisi waliingilia kati na kuwataka kutawanyika ambapo, walikaidi hivyo polisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.
Hata hivyo, baada ya dakika 15 baadaye walirejea tena kuendeleza maandamano hayo kwenda Makao Makuu ya CHADEMA. Polisi waliongeza nguvu zaidi na kuwatawanya.

MWANZA
Jijini Mwanza mamia ya vijana wa CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na ACT Wazalendo waliandamana na kuchoma bendera na kadi za CHADEMA.
Tukio hilo lilitokea jana mchana mbele ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, ambapo vijana wapatao 400 walikusanyika kutoka katika meneo mbalimbali ya jiji hilo wakiwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali wa kuwaponda viongozi wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Huku wakiimba “Mbowe kauza chama... hatukubali…tumejitambua” walidai hotuba ya Dk. Slaa imewatoa gizani, hivyo wanaibwaga CHADEMA na  mgombea wake Lowassa.
Vijana hao waliokusanya wananchi wengi kushuhudia, walikusanya kadi zao (nyingi zikiwa za Chadema) pamoja na bendera ya chama hicho na kuvichoma nakusema wanahamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kina mgombea bora, mchapa kazi na mwadilifu.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wenzao, Salim Yahaya, Juma Salum, Hamis Mashidonge, Happiness Kifula, Siajabu Mnaku (CHADEMA), Jackob Timbuta (ACT Wazalendo) na Mussa Ramadhan (CUF), walidai wamegundua vigogo wa UKAWAwamewauza, hivyo ni bora warudi CCM.
“Alichokifanya Mbowe kutuuza kwa fisadi Lowassa, hatukubali ndiyo maana tumekuja hapa na kuchoma bendera na kadi za vyama vyetu, kuanzia leo tunaliunga mkono Jembe na Tingatinga la CCM, Dk. Magufuli,” alidai Yahaya.
“Wenje nilikuwa nampenda sana lakini naya hafai, ni muongo na mnafiki alikuwa anatudanganya kuwa Dk Slaa yupo likizo atakuja kumbe walisha kula dili, tumechoka kutumiwa tunamuunga mkono Dk Slaa huyo ndiye alistahili kuwa Rais wetu, ana uchungu na watanzania,” alieleza Ramadhan na kudai pia anajiunga CCM.
Vijana hao waliripuka kumshangilia mgombea urais wa CCM Dk Magufuli, kabla ya kutawanyika na kurudi katika maeneo waliyotoka baada ya greda dogo la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kupita eneo hilo la nje ya ukumbi wa Ghand walipokuwa wamefurika.
“Jamani pisheni tingatinga kama Magufuli linapita,” alidai mmoja wao na vijana hao kuamsha wimbo ‘aliselema’ wakidai wanamtaka Tinga (Dk. Magufuli) kama hilo linalopita ang’oe ufisadi serikalini huku wakinyoosha juu mabango yao ambayo baadhi yalisomeka.
“Wenje ulitudanganya Dk Slaa yuko likizo kumbe kumbe mmepiga dili, Mbowe umezika chama chetu na wewe ni fisadi, Lowassa, Mbowe na Chadema wote choo,”

WASOMI WACHAMBUA
Wasomi na wanasiasa mbalimbali wamesema CHADEMA inaelekea kujizika kisiasa.
Wamesema hivi sasa hakitakuwa na hoja ya kuikosoa CCM baada ya kukumbatia mafisadi waliokuwa wakiwanyooshea kidole kwa muda mrefu.
DK. LAWI OUT
Akizungumza na Uhuru jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Kitivo cha Sayansi, D.Lawi Yohana, alisema iwapo CHADEMA watashindwa kuwashawishi kuingia Ikulu kupitia uchaguzi huu nafasi yao katika jamii itakua finyu.
Dk. Lawi alisema kwa muda mrefu CHADEMA ilijijengea uaminifu mbele ya jamii hususan kwa kuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi,. lakini kutokana na hatua yake ya kumsimamisha kuwania urais mtu waliyemtuhumu kwa ufisadi kwa muda mrefu, hilo litawafanya wapotee.
"Endapo watashindwa uchaguzi wataweza kusimama mbele ya jamii na kunyoosha kidole kwa wengine kushutumu ufisadi.
"Ni wazi kwamba hakuna kiongozi yeyote wa CHADEMA atakayekuwa na ujasiri wa kufanya hivyo kwa kile walichokuwa wakikikemea ndicho walichokifanya," alisema.
Aidha, alimsifu na kumpongeza Dk. Slaa kwa ujasiri wake wa kukataa kuwa sehemu ya wababaishaji na kujipambanua mbele ya jamii.
Kwa mujibu wa Dk. Lawi, kwa muda mrefu Watanzania walitaka kumsikia Dk. Slaa kwa kuwa ni kiongozi anayekubalika na mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa.
Hata hivyo, alimuomba Dk. Slaa kuweka wazi ni mgombea gani wa urais kati ya wote waliojitokeza kwenye uchaguzi wa mwaka huu anaweza kuwa msaada na kiongozi bora kwa Watanzania.
PROFESA BENSON BANA
Kwa upande wake mchambuzi wa siasa ambaye pia ni mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chui Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana, alisema alichofanya Dk. Slaa ni ujasiri wa kuungwa mkono.
Profesa Bana alisema nchi haiwezi kuongozwa kwa siasa chafu wala hila bali inaongozwa kwa utaratibu na kiongozi mwenye uwezo wa kusimamia uamuzi kwenye kila nyanja.
Alisema Watanzania wanapaswa kutafakari na kufahamu kwamba,endapo wataamua kumuingiza mtu Ikulu kwa kigezo cha mafuriko pia nchi inawezakuondoka kwa mafuriko.
 “Ni kweli nchi inahitaji mabadiliko lakini je nani atuongoze katika mabadiliko hayo. Mabadiliko lazima yasimamiwe, yaasisiwe na yaongozwe kwa uzalendo. Tusiende tu kama bendera kufuata upepo kisha tutakuja,”alisema.
Aliongeza kuwa, Watanzania wapime aliyoyasema Dk. Slaa na kuyatafakari huku wakifuatilia historia yake katika upinzani watapata jibu sahihi kwa kuwa ni miongoni mwa viongozi

DK. MWAKYEMBE
Akizungumza kuhusu madai mbalimbali yanayotolewa na wafuasi wa CHADEMA hasa baada ya Dk. Slaa kufichua madudu yao, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe alisema wanachofanya wapinzani hao ni kutapatapa.
"CHADEMA wanaweweseka badala ya kujibu hoja za msingi zilizoelezwa na Dk. Slaa. Wanahangaika ooh alikula nini asubuhi, aliongozana na nani, alikutana na nai, alimwamkia nani, huku hoja za msingi zikiwekwa pembeni.
"Nikiwa Dar es Salaam karibu kila siku napita katika Hoeli ya Serena, ile ni hoteli si nyumbani kwa Dk. Slaa," alisema.

PROFESA SAFARI AKIRI
Akijibu maelezo yaliyuotolewa na Dk. Slaa juzi kwamba alipokea barua yake ya kuomba kujiuzulu, Mmoja wa wanasiasa waandamizi wa CHADEMA Profesa Abdallah Safari alisema aliamua kufanya hivyo baada ya kuona barua hiyo imeandikwa kwa dharura katika Hoteli ya Bahari Beach walikokuwa wakifanyia vikao.
Profesa Safari alidai barua hiyo aliiandika kwenye vijitabu vinavyotolewa hotelini hapo hususan kwa wale wanaohudhia mikutano mbalimbali.
"Ni kweli nilipokea barua yake na nikaitia mfukoni tena sikuichana kama alivyosema hata kesho ukitaka nikuletee ndugu mwandishi ili uipige picha na kuiweka katika gazeti lako, nitafanya hivyo.
"Niliamua kuichana kwa kuwa niuliona haikufuata utaratibu wa kisheria," alisema.

POLEPOLE  AWALIPUA TENA
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Humprey Polepole, amesema Ukawa haipaswi kuchaguliwa kwa sababu kiongozi   waliyempa dhamani ya kuwania urais ana alama ya tuhuma za ubadhirifu.
Alisema kufuatia hali hiyo, imewafanya Ukawa kutoizungumzia ajenda ya kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kwenye majukwaa ya kisiasa.
Akizungumza juzi, kwenye kipindi cha 360, kinachorushwa na Clauds TV, Polepole alisema, CCM imefanikiwa kulidhibiti genge lililokuwa likikichafua.
Alisema, baada ya kukamilika kwa mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM, chama kimedhihirisha uwezo wake wa kukabiliana na genge la wahuni.
Polepole alisema, Watanzania wanapaswa kumchagua kiongozi atakayekuwa akiibeba ajenda ya uadilifu na kupambana na ufisadi.
Alisema, Ukawa imepotoka na kwenda kinyume na misingi yake ya awali kama ilivyokuwa katika kipindi cha mchakato wa Katiba mpya.
“Ukawa imepotoka katika misingi yake, mtu akiwa na tuhuma za ufisadi hapaswi kuongoza taifa letu, watu wa Ukawa wamefanya uamuzi usio sahihi” alisema.
Alisema, Magufuli ni mgombea aliyepitia misingi ya Mwalimu Nyerere kwa sababu hasukumwi na nguvu ya pesa.
Aliongeza kuwa, mgombea huyo wa CCM, ni mchapakazi na anauwezo wa kudhibiti vitendo vya rushwa.
ASKOFU IKONGO ALONGA
Mkuu wa Kanisa la Act of God, Askofu Pius Ikongo, amesema maaskofu wanaopinga tuhuma zilizotolewa na Dk Slaa kuwa baadhi yao wamepewa rushwa hawako sahihi.
Alisema, maaskofu hao wamechukua hatua zipi tangu kutolewa kwa ripoti ya kashfa ya Esrow iliyowataja maaskofu waliopokea fedha hizo.
Kauli hiyo aliitoa jana, wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Kilimanjaro Kempsky, kuwa alipotoa pendekezo la kuwawajibisha maaskofu waliopewa fedha hizo baadhi ya viongozi  walimpinga.
Alisema, askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ni mwanasiasa aliyejificha kwenye mwamvuli wa dini.
Katika kulithibitisha hilo, inashangaza kwa kiongozi huyo wa dini kuhudhuria vikao vya juu vya Chadema.
Alisema, Gwajima alihusika kuwasafirisha baadhi ya maaskofu kuhudhuria mkutano wa Lowassa uliofanyika Arusha.
Alisema, katika mkutano huo, gari la Gwajima lilitumika kuwasafirisha maaskofu hao wakilipwa fedha za chakula.
“Inashangaza maaskofu kuhudhuria mikutano ya kisiasa, ingekuwa wanakwenda kuhubiri neno la mungu ni sawa lakini sio katika mikutano ya kisiasa” alisema
Alidai kuwa, Gwajima ameligawa Baraza la kidini la CPCT kwa kumdanganya Katibu Mkuu wa baraza hilo, Askofu David Mwasota.
Alisema, ameligawa kwa kutumia fedha ili kuanzisha baraza jingine na anatumika kisiasa.
Alimpongeza Dk Slaa kwa kuzungumza ukweli na kumtaka kutovunjika moyo kwa kuwa mungu yupo naye.
Alisema, idadi kubwa ya Watanzania wanamuunga mkono kwa kuwawezesha kuwafungua macho kuhusiana na matendo maovu yanayotendeka.
Askofu Ikongo alisema, katika kongamano la viongozi wa dini kanda ya Ziwa, walibainisha kuwepo kwa viashiria kwa baadhi ya viongozi wa dini kujihusisha na ushabiki wa kisiasa nje ya mipaka ya kidini.
Katika azimio hilo, hawakukubaliana na viongozi wa dini wanaoeneza matendo hayo kwa kuwataka, kutojihusha na ushabiki wa kisiasa kwa sababu nyumba za ibada ni mahala patakatifu.
Alisema, wanasiasa hawapaswi kufanya kampeni katika nyumba za ibada au viongozi wa dini kwenda kwenye majukwaa ya kisiasa kuwanadi wagombea.
Aliwataka viongozi wa kidini, kusimama katika kazi ya kuliombea taifa ili uchaguzi umalizike kwa amani na utulivu.

WANANCHI WATOA YAO
Kwa upande wao wananchi mbalimbali walitoa Dk. Slaa ni kiongozi wa mfano anayestahili kuigwa na wana-CHADEMA na UKAWA wote.
Sylvester Matthew mkazi wa Dar ews Salaa,, alisema hotuba hiyo imekuja wakati mwafaka na kuwataka Watanzania kutoipuuza.
Alisema wananchi wanapaswa kuachukua ushabiki na kufuata mkumbo, badala yake wajitafakari na kuchagua kiongozi atakayewafaa na si mafisadi.
Kwa upande wake Ally Rashidi, mkazi wa Kariakoo, alisema iwapo Dk. Slaa asingeweka wazi yale aliyoyazungumza, angekuwa hajawatendea haki Watanzania, kwani wengi wamekuwa wakidanganyika kuwa Lowassa ni msafi na anaonewa tu kwa tuhuma za Richmond.
“Angalau sasa baada ya hotuba ya jana, wengi wamegeuka na kuipuuza ukaw, baadhi yao wanasema ni bora kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) au kutopiga kura na kubaki bila chama chochote,” alisema.
Miriam Samuel Mkazi wa Upanga, alisema anaona Dk. Slaa amechelewa kujitokeza na kuzungumza kile alichokiita ni ukweli kwani tayari kuna wananchi wameshadanganyika na hawapo tayari kuchanganua ukweli.
“Nawashauri watu hao kuwa wanapaswa kubadilika na kuchanganua vutu, mambo anayozungumza Dk. Slaa, kama alivyosema si uzushi na anavyo vielelezo vyote,” alisema.
Humphrey Joseph, mkazi wa Kawe, aliwataka watanzania kuondokana na dhana kuwa Dk. Slaa anatumiwa na CCM, ni siasa za propaganda ya ukawa tu ambao wameishiwa hoja  madhubuti.
“Namfahamu Dk. Slaa kama mtu makini, alichokizungumza jana, alishazungumza miaka 8 iliyopita, hajatunga lolote, nawasisitiza kuwa watajuta kumweka madarakani mtu asiyetosheka na mali, hakuna dhamira ya kuboresha maisha ya Watanzania kwa mtu huyu hata kidogo,” alisema. 
Juzi mchana, Dk. Slaa, alihutubia wananchi kupitia vituo mbalimbali vya televisheni na redio, katika mkutano na waandishi wa habari, ambapo alitangaza rasmi kukiacha  Chadema na kuahidi kuendelea kuwatumikia Watanzania nje ya siasa.
Alieleza jinsi ambavyo chadema kilimkaribisha mgombea wake wa urais, Edward Lowassa, kinyume cha taratibu.
Vile vile, Dk. Slaa alimchambua Lowassa, jinsi ambavyo hafai kuwa kiongozi kutokana na kashfa nyingi za ufisadi.
Hata hivyo, Dk. Slaa alimshangaa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Simaye, kwa kumsafisha Lowassa kwa Watanzania ambapo alishatoa kauli nyingi za kumtuhumu na kuapa kutokaa naye meza moja.
Alisema, Sumaye mwenyewe si msafi kwani yeye mwenyewe Alishawahi kumshutumu Bungeni kutokana na kumiliki shamba kubwa la Kibaigwa, mkoani Dodoma huku akiwaachanwananchi hawana ardhi.
‘Leo Sumaye anasema Lowassa msafi, dhambi haiwezi kuhalalishwa na dhambi nyingine, kama mnakumbuka watanzania waliwahi kumwita Sumaye ‘ziro’,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa, aliifananisha Chadema kuwa sawa na choo kwa kujitia ujasiri wa kupakua uchafu wa chooni na kuuleta chumba cha kulala kwa kuwa kitakuwa choo, tena kinachonuka kuliko choo halisi.
Alisema, Chadema imebaki haina hoja ya kukemea uchafu kwa chama tawala kuwa uchafu huo wote umehamia kwake.
MBATIA ATAKA MAFISADI WASAMEHE
Ahadi ya mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli ya kuunda mahakama maalumu ya kuwashughulikia  mafisadi na wala rushwa, imeendelea kuitesa kundi la Ukawa baada ya Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kutaka mafisadi wasamehewe.
Pia, hofu ya uwezo mdogo wa mgombea wa urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, kushiriki kwenye mdahalo na kujibu tuhuma dhidi ya ufisadi umedhihirika wazi baada ya Mbatia kutaka  ashiriki kwenye mdahalo kwa niaba ya Lowassa.
Kauli hiyo ya Mbatia ambaye ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, imekuja kufuatia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa, kuanika hadharani tuhuma za ufisadi dhidi ya Lowassa ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na kujiuzuru kwa kashfa ya Kampuni ya kufua umeme ya Richmond.
Katika tuhuma hizo Slaa alisema, Ukawa wanajengaje maadili kwa kutumia watu waliohusika na uchafu wakati Scotland Yard iliwahi kutaka  kufanyika kwa uchunguzi kuhusu uhalali wa dola milioni 400 za Lowassa.
Akizungumza Dar es Salaam, jana, Mbatia alisema kunahaja ya kuundwa kwa tume ya malidhiano ili mafisadi na wala rushwa wasamehewe.
Alisema, Watanzania ambao walioathirika na matukio ya aina hiyo pia  ni vyema wakajenga moyo wa kusamehe.
“Hata ndani ya Ukawa, endapo tukishika madaraka basi tutaunda tume ya maridhiano ili mafisadi waweze kusamehewa na Watanzania wajenge moyo wa kusamehe” alisisitiza.
Alisema, mafisadi watapaswa kuwaomba radhi wananchi na kisha Watanzania wajenge moyo wa kusamehe.
Mbatia ambaye wakati wote alipokuwa akizungumza, alionekana kushindwa kujenga hoja kwa kile alichokuwa akizungumza na wananchi zaidi ya kuwatuhumu baadhi ya viongozi kwa masuala mbalimbali na kudai atawataja hadharani.
Katika hali ya kushangaza, Mbatia hata alipotakiwa na waandishi habari kutaja orodha ya majina ya viongozi hao alishindwa kuyataja.
Mbatia alisema, Ukawa hawawezi kumsumbua, Lowassa kushiriki kwenye mdahalo kwa kuwa wanaotaka kufanyika kwa mdahalo huo sio hadhi yake.
Badala yake, Mbatia alitaka ashiriki yeye katika mdahalo huo badala ya Lowassa.
0000

No comments:

Post a Comment