Monday, 12 June 2017

BULEMBO AMALIZA ZIARA KATIKA WILAYA 47 ZA MIKOA SABA, JOTO LAKE LASABABISHA CHADEMA 376 KUTIMKIA CCM






Na Bashir Nkoromo

Hatimaye Mjumbe wa kamati Kuu ya CCM, Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi na Mbunge wa Kuteulia na Rais Alhaj Abdallah Bulembo, amemaliza ziara yake ya Kichama akiwa amefanikiwa kutembelea mikoa saba na jumla ya Wilaya 47 za mikoa hiyo.


Katika ziara hiyo ambayo alianza May 26, 2017, aliihitimisha jana, Juni 10, 2017 katika mkoa wa Geita, ziara ikiwa imechukua zaidi ya wiki mbili, ambapo mkoa wa kwanza kufanya ziara hizo uliuwa Dar es Salam na badaye kuendelea katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Tabora, Kigoma, Kagera na Geita ambao ndio mkoa aliomalizia.


Alhaj Bulembo katika ziara hiyo ambayo haikuhusu Jumuia yake ya Wazazi Tanzania, bali ya Kichama zaidi ilikuwa mahsusi kwa kuagizwa na Bosi wake, Mwenyekiti wa CCM Rais John Magufuli, kwa lengo la kutoa shukrani kwa wana CCM kufuatia kura nyingi walizompa hadi kukipatia Chama Cha Mapinduzi kura nyingi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 2015.


Hata hivyo Bulembo anasema, Shukrani hizo, ni za awali kwa kuwa Mwenyekiti Mwenyewe Rais Dk. John Magufuli atafanya ziara rasmi kutoa shukrani.


Katika ziara hiyo, Alhaj Bulembo pia pamoja na mambo mengine ya kuhimiza ujenzi na uimarishaji Chama na Jumuia zake, alikuwa na ajenda za kufafanua kuhusu mabadiliko yaliyowaacha nje badhi ya waliokuwa Mabalozi na pia kufafanua kwa kina umuhimu wa Mabalozi wapya waliopatikana sasa na wale waliobaki kutokana na mabadiliko hayo ndani ya Chama.


Alhaj Bulembo kwenye vikao vya ndani kwenye ziara hiyo alipata fursa za kuwapiga msasa, kwa kuwapa darasa zito Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM katika Wilaya husika, Wajumbe wa Mabaraza ya Jumuia zote za Chama, Mabalozi na Watendaji wote wa serikali.


Mara kadhaa alisisitiza umuhimu wa madiwani kuwa karibu na viongozi wa Chama hasa mabalozi, ikiwa ni pamoja na kuwatambua kwa karibu hadi kwa majina na kujenga mahusiano ya kawaida kwa lengo la kukuza ukaribu baina yao na viongozi hao, siyo tu wa kichama bali hadi wa kifamilia.


Katika hali ambayo haikuwa ikitarajiwa,  katika wilaya karibu zote alizofika, ilionekana dhahiri kwamba madiwani karibu wote walikuwa hawana mahusiano ya kawaida na mabalozi, hali hii ilijidhihirisha pale Alhaj Bulembo alipokuwa akiwasimamisha madiwani na kumuuliza kila mmoja alivyoshiriki kwenye uchaguzi wa mabalozi, idadi ya mashina na majina ya mabalozi katika kata zao.


Madiwani wengi walijikuta wengine hawajui hata idadiya mashina katika kata zao, na pia walishindwa kutaja idadi ya mabalozi kwenye eneo lao, na kutaja majina ya mabalozi ndiyo ilikuwa kazi kubwa. Diwani alijikuta akitaja balozi mmoja au wawili tu, kata nzima.


“Mnajua lengo la mahusiano haya, ni kukirahisisha Chama kupata kura kwa urahisi wakati wa uchaguzi, kwa sababu ninyi madiwani mkiwa mmeshajenga mahusiano na Wenyeviti wenu wa mitaa na mabalozi hakutakuwa na kazi ngumu ya kutafuta kura, na lazima mtambue kuwa Mabalozi ndiyo siri kubwa ambayo hufanikisha ushindi wa CCM katika chaguzi”, anasema Bulembo kwa nyakati tofauti.


Mbali na darasa alilokuwa akitoa kwenye vikao hivyo, katika ziara hiyo amewesha CCM kujizolea wanachama wapya 376 ambao walikihama chama cha Chadema na kujiunga na CCM, wakiwemo waliokuwa viongozi wa Chadema katika vitongoji na Vijiji na aliyekuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita.

No comments:

Post a Comment