Na Nathaniel Limu, Mkalama
WANASIASA wa upinzani wameonywa
kuacha kutumia hotuba za Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa
lengo la kujinuifaisha kisiasa.
Badala yake wametakiwa kutumia
hotuba hizo kujikosoa kutokana na kufanya mambo kinyume na kuliweka taifa
kwenye hatari ya kuingia kwenye machafuko.
Onyo hilo limetolewa juzi jioni
na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, wakati akizindua kampeni za kuwania
ubunge na madiwani katika Jimbo la Mkalama mkoani Singida.
Alisema hivi karibuni kumekuwa
na wimbi la baadhi ya wagombea wakiwemo wanaowania urais, kutumia baadhi ya
hotuba za Mwalimu Nyerere wakilenga kuwaaminisha wananchi wawachague kwa madai
watafuata nyayo zake.
“Wengi wa viongozi hawa wanajaribu
kuwahadaa wananchi na kuwa kuhama CCM kimezingatia maneno ya Mwalimu Nyerere kuwa,
mabadiliko usipoyapata ndani ya CCM, unaweza kuyapata nje ya CCM,” alisema.
Mwigulu, ambaye anatetea nafasi
hiyo alisema mabadiliko ya kweli aliyoyazungumza Mwalimu Nyerere sio ya kuhama
vyama kusaka nafasi za uongozi bali ni ya kiutendaji ambayo yatafanyika ndani
ya CCM na si kwa kukimbilia upinzani.
Alisema itapendeza zaidi iwapo
wanasiasa hao mabingwa watazungumzia pia kauli za Mwalimu Nyerere kuwa, 'anayekimbilia
Ikulu kwa kutumia fedha hafai na atazirejeshaje'.
"Kama wao ni mabingwa wazungumzie
maneno ya Mwalimu Nyerere kuwa 'Ikulu ni mahali patakatifu na kuna nini hadi
mtu apakimbilie’. Mwalimu alisema hawa watu wanatoa wapi fedha za kuhonga,”
alisema Mwigulu.
Aidha, Mwigulu aliwataka wana
CCM waliohama baada ya kushindwa katika kura za maoni huko walikokimbilia
kutimiza tamaa zao za kutaka uongozi, wasipopata wanaweza kurejea CCM iwapo watakaribishwa tena.
"Wewe fikiria mtu kama
Lowassa (Edward) amelelewa na CCM zaidi
ya miaka 40 sasa, kichwa chake chote hakina kitu kingine kimejaa CCM. Mambo
ambayo atataka kuyaanzisha kwenye UKAWA yatakuwa na harufu kubwa ya CCM tu. Kwa
hiyo, huko walikokimbilia kusaka uongozi kwa gharama yoyote ikiwemo ya matumizi
makubwa ya fedha hakuna cha ziada,” alisema.
Alisema upinzani katika uchaguzi
mkuu mwaka huu haupo kabisa bali kilichopo ni CCM (A) na CCM (B) ndizo zinazochuana.
Mwigulu aliwaeleza wananchi hao
kuwa chaguo la Watanzania kwa urais ni Dk. John Magufuli, ambaye ni kiongozi
safi na asiye na kashfa.
No comments:
Post a Comment