Thursday, 3 September 2015

SAMIA AKERWA NA UCHAFU DAR, AAHIDI KUVALIA NJUGA TATIZO HILO



NA WAANDISHI WETU
 MGOMBEA  mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, amesema
anakerwa na uchafu wa jiji la Dar es Salaam, hivyo kuahidi kuvalia
njuga tatizo hilo baada ya kuingia madarakani.
Alisema katika kuhakikisha hilo linatekelezwa, serikali ijayo
itawabana wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa  katika jiji  la Dar
es Salaam na  kwamba watakaoshindwa kusimamia hilo, wataondolewa
kwenye nafasi zao mara moja.
“Mimi ni mwanamke ambaye ni mzazi wa watoto wanne. Ninakerwa sana na
ninapata uchungu kuona watoto wadogo wakichakura jalalani, tena wakiwa
pekupeku. Sipendi hali hiyo na nitahakikisha hilo nalisimamia
ipasavyo.
“Najua wananchi wanatozwa ada za kuzoa taka, lakini hazitolewi kwa
wakati. Hata kule kwangu Kijitonyama kuna kampuni ya kuzoa takataka,
lakini kazi yake inafanya kwa kusuasua. Hili hatutakubaliana nalo hata
kidogo,” alisema katika mkutano wa kampeni za CCM, kwenye viwanja vya
Buza, wilayani Temeke.
Sambamba na hilo, aliwataka mgambo wa jiji ambao wamekuwa kero kwa
wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo, kama mama lishe na
wamachinga, kuacha kuwabugudhi, ili  wafanye shughuli zao kwa amani.
Alisema serikali ya CCM haipendi kuona wananchi wake wakipata adha ya
kusumbuliwa na wamachinga kila kukicha na hata kunyang’anywa mali zao,
hivyo watakaoendelea na tabia hiyo watakiona cha mtema kuni.
Katika hatua nyingine, alitangaza neema kwa wajasiriamali kwamba
watanufaika na mikopo ya riba nafuu kutoka katika taasisi za fedha.

MMANDA AMMWAGIA SIFA

Akimnadi mgombea mwenza katika viwanja vya Mbagala Charambe, Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Evod Mmanda, alisema Samia ni
mwanamke shupavu na mchapakazi, hivyo anatosha kuwa Makamu wa Rais.
Mmanda alisema Samia anastahili kuwa katika nafasi hiyo si kwa sababu
ni mwanamke tu, bali pia ni msomi na mtu mwenye uzoefu mkubwa katika
medani ya uongozi.
Alisema historia na rekodi yake katika uongozi ni sifa kubwa za
kumfanya ateuliwe kuwa mgombea mwenza. Alisema Samia alikiwa Waziri wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa miaka 10 na miaka mitano
serikali ya Muungano.
“Alikuwa anaongoza wizara ya Wanawake, Jinsia na Watoto na baadaye
Wizara ya Utalii na Uwekezaji Zanzibar. Pia amekuwa waziri wa masuala
ya Muungano. Kwa uzoefu huo ndiye mtu anayejua kwa undani matatizo
yahusuyo na wanawake watoto.
“Uchumi wa Zanzibar umepanda na kwa kiasi kikubwa na mchango mkubwa
katika hilo kutokana na utalii, sekta aliyokuwa akiiongoza. Zaidi ya
hapo kulikuwa na kero nyingi za Muungano na hivi tunavyozungumza
zimebaki mbili tu, nazo zinashughulikiwa. Yote hiyo ni kazi ya Samia
Suluhu Hassan,” alisema.
Kutokana na sifa hizo, Mmanda alisema Samia ameandaliwa vya kutosha
katika nafasi hiyo na hilo halina hata chembe ya ubishi, hivyo
Watanzania hawana budi kumchagua Dk. John Magufuli kuw kuongoza
Tanzania, ili Samia awe makamu wake.

UMMY AONYA

Kwa upande wake, Mjuumbe wa Kamati ya Taifa ya Kampeni ya CCM, Ummy
Mwalimu, alisema wananchi wa Temeke watafanya kosa iwapo watachagua
wapinzani katika urais, ubunge na udiwani.
Alisema Watanzania hawataki mabadiliko eti kwa sababu ya kuiondoa CCM
madarakani, bali hoja kubwa ni maendeleo ambayo yataletwa na CCM
pekee.

“Mmeshajiuliza wapinzani walishafanya kitu gani tangu vyama vingi
vilipoanzishwa? Mambo yote haya yamefanywa na CCM, hivyo ichagueni
tena, ili iendelee kuleta maendeleo,” alisema.
Alitumia nafasi hiyo kumnanga mgombea urais wa CHADEMA, Edward
Lowassa, kwa kusema hakuifanyia kitu chochote Temeke alipokuwa waziri
mkuu.
Alisema hivi sasa Jimbo la Temeke lina matatizo makubwa ya maji na
tatizo hilo lilichangiwa na Lowassa kwa kuwa alipokuwa katika wizara
hiyo aliisahau Temeke.
Kwa mujibu wa Ummy, matatizo ya maji na kero zingine zinazoikabili
Temeke zitashughulikiwa na CCM kwa kuwa imeyaweka bayana katika ilani
yake ya uchaguzi.

No comments:

Post a Comment