Monday 9 November 2015

RAIS MAGUFULI AVUNJA BODI YA MUHIMBILI, AMTIMUA MKURUGENZI WA ZAMANI, AMTEUA MPYA


Na Waandishi Wetu
RAIS Dk. John Magufuli ametangaza kuvunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambayo ilishamaliza muda wake.
Aidha, Rais Magufuli amemteua Profesa Lawrence Mseru, kukaimu nafasi ya mkurugenzi mkuu wa Muhimbili kuanzia leo.
Kufuatia uamuzi huo, Dk. Hussein Kidanto, aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo, amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine.

Uamuzi huo wa Magufuli umekuja saa chache baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo na kujionea hali halisi ya utoaji wa huduma za afya.
Taarifa  iliyotolewa jana jioni na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilimkariri Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, akisema:
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli , leo (jana) mchana amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukutana na hali ya kusikitisha.

“ Rais  amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini. Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika Hospitali za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko”.  
Balozi Sefue pia amesema,   Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo.
Tayari Wizara ya Fedha imetoa sh. bilioni tatu kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote.
Balozi Sefue pia ametumia nafasi hiyo kuwaagiza watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.
“Hakutakuwa na huruma kwa watumishi wa Umma wasiojali wananchi na mahitaji yao,” alisisitiza Balozi Sefue.
Mapema, katika ziara  hiyo ya kushtukiza, Rais Magufuli pia alitembelea Taasisi ya Mifupa na Tiba ya Mfumo wa Fahamu (MOI) na kuvuta hisia za wananchi wengi.
Akiwa hospitalini hapo wagonjwa na wananchi wanaouguza wagonjwa wao walimiminika kumuona huku wakimshangilia na kusema huyu ndiye kiongozi anayetakiwa.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza kwenye taasisi za serikali. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Magufuli alifanya ziara kama hiyo katika Wizara ya Fedha na kujionea namna ya utendaji kazi wa wizara na kuwasisitizia watumishi wake usimamiaji mzuri wa ukusanyaji kodi.
Rais Dk. Magufuli, ambaye alitembelea wodi ya Mwaisela namba mbili na Sewahaji namba 17 na 18, kwa lengo la kujionea hali halisi ya utoaji wa huduma za afya, alitoa motisha ya soda kwa wafanyakazi na wagonjwa.
Baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo walisema wamefurahishwa na ziara hiyo kwa sababu itawezesha kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili wao na wagonjwa.
Miongoni mwa changamoto zinazoikabili Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ni pamoja na ubovu na ukosefu wa vipimo muhimu kama CT-Scan na MRI kwa muda mrefu.
Wafanyakazi hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe kwa kuwa si wasemaji, walisema ukosefu wa vipimo hivyo unasababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa.
Walisema kukosekana kwa vipimo hivyo kunasababisha baadhi ya wagonjwa kushindwa kufanyiwa upasuaji, hivyo wanaamini ziara hiyo itakuwa mwarobaini wa tatizo hilo.
Walisema gharama ya vipimo hivyo katika hospitali binafsi ni kubwa, hivyo kuwawia vigumu wananchi wa hali ya chini na zinaongezeka zaidi kwa mgonjwa aliyelazwa Muhimbili, kwani anatakiwa akodi gari la wagonjwa kumpeleka katika vipimo.
Kwa upande wao, wananchi ambao wanauguza wagonjwa wao, walifikisha kilio chao cha ubovu wa vipimo hospitalini hapo, ambapo Rais Magufuli aliahidi kulishughulikia suala hilo.
Wananchi hao, ambao walikuwa wakimshangilia Rais  Magufuli muda wote aliokuwepo hospitalini hapo, walisema wana imani kubwa kwamba atazipatia  ufumbuzi changamoto zote zinazoikabili kwa kuwa amejionea mwenywe hali halisi.
Mara baada ya Rais Magufuli kuondoka hospitalini hapo, baadhi ya wafanyakazi walijikusanya katika makundi, wakijadili namna ambavyo wanatakiwa kufanyakazi ili kuendana na kasi yake.
Wafanyakazi hao pia walibadili salamu zao za kawaida wanapokutana na kuanza kusalimiana kwa kutumia kaulimbiu ya Rais Magufuli ya ‘Hapa kazi tu’.
Awali, Rais Magufuli alifanya ziara katika Hospitali ya Aga Khan na kuwajulia hali Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo-Bisimba na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Beatrice Shelukindo.

No comments:

Post a Comment