MGOMO wa wafanyakazi
wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL),
umechukua sura mpya baada ya kuiomba serikali kuwafukuza viongozi wa kampuni
hiyo.
Aidha, wameiomba
serikali kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji kutokana na uongozi uliopo
kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Wafanyakazi wa kampuni
hiyo wamedai uongozi huo umeisababishia hasara kubwa kampuni na kwamba
inajiendesha bila kupata faida huku ikishindwa kuboresha hali ya maisha ya
wafanyakazi.
Naibu Katibu wa Chama
cha Wafanyakazi wa Reli Taifa (TRAWU), Boaz Nyakelele, alisema juzi kuwa, uongozi
uliopo umechoka na kwamba hauna ubunifu wa kuendesha kampuni hiyo kibiashara na
umeshindwa kulipa malimbikizo ya madai ya wafanyakazi.
Alisema uongozi huo
umeshindwa kulipa madai ya wafanyakazi, yakiwemo fedha za makato ya mifuko ya
jamii na mifuko ya bima ya afya zaidi ya sh. bilioni mbili.
“Hatujalipwa madai
yetu ya fedha za malimbikizo kuanzia Julai hadi Novemba, 2014. Mkurugenzi
Mtendaji wa TRL alimuahidi Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati wa ziara yake
kuwa atahakikisha analipa madai hayo Desemba 31, mwaka jana, lakini hadi sasa
hajafanya hivyo,” alisema.
Alisema uongozi wa TRL
umekaidi ahadi ya kulipa madeni ya
wafanyakazi, badala yake umetumia kigezo cha kubana matumizi kutowalipa kwa
kusitisha kufanyakazi saa za ziada.
Nyakelele alisema
uongozi wa kampuni hiyo umesitisha saa za ziada za kufanyakazi, lakini umewaajiri
vibarua maarufu kwa jina la ‘viarusi’, ambao wanafanyakazi kwenye treni za
kusafirisha abiria, ikiwemo treni inayotoa huduma katikati ya jiji, maarufu
kama ‘Treni ya Mwakyembe’.
“Uongozi umeshindwa
kabisa kuboresha maslahi ya wafanyakazi, ikiwemo mkataba wa hali bora, ambao ni
chachu ya kufanyakazi katika kampuni hii na hivi sasa wafanyakazi wengi
tumekata tamaa,” alisema.
Kwa upande wake,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk.Leonard Chamuliho, alisema serikali
imesikia kilio cha wafanyakazi hao na kwamba, kuna mambo yanafanyiwa kazi,
ikiwemo masuala ya kisheria kuhusu madudu ya waliohujumu mabehewa ‘feki; na
mengineyo ya utendajikazi.
“Najua mnahamu ya
kutaka kufahamu hatima ya wabadhirifu hao, lakini naahidi kuwa nitawapa
mrejesho hivi karibuni,” alisema.
Dk. Chamuliho alisema
mambo ya kisheria yataendelea kisheria ili kutoleta sintofahamu kuhusu tuhuma
hizo na kwamba hali hiyo itakwisha hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment