WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amewaagiza wamiliki wa viwanda hapa nchini kuhakikisha wanatoa mikataba kwa wafanyakazi wao na kuwalipa kwa wakati ili kuondoa migogoro isiyo na tija.
Mwijage alitoa agizo hilo jana, wakati wa ziara ya kikazi mkoani Kagara, ambapo alitembelea viwanda vya Vic Fish na Kagera Fish, ambavyo vinajihusisha na kuchakata minofu ya samaki, vilivyoko katika wilaya ya Bukoba.
Waziri huyo pia alitembelea shamba la chai la
Bushumba, lililoko wilayani Muleba na Kiwanda cha Tanica cha kusindika kahawa
ya unga na cha Amir Hamza cha kukoboa na kusaga kahawa, vilivyoko Manispaa
ya Bukoba.
Katika ziara hiyo, Waziri Mwijage alikutana na
wakulima wa chai na wafanyakazi wa viwanda hivyo, ambao walielezea changamoto zinazowakabili
na kuiomba serikali kuzitafutia ufumbuzi.
Baadhi ya wafanyakazi waliwalalamikia waajiri wao
kwa kutowapatia mikataba ya kazi na wakati mwingine kutowalipa stahiki zao kwa
wakati, jambo linalozua migogoro mahali pa kazi kati ya mwajiri na wafanyakazi.
Kufuatia malalamiko hayo, Mwijage alisema maelekezo
ya serikali ni kuona viwanda vyote nchini vinafanyakazi.
"Ninachotaka ni kuona idara ya biashara, viwanda
na uwekezaji inashamiri, kwa hiyo naagiza wawekezaji wote wenye viwanda
kuhakiisha mnafuata sheria inavyosema kwamba, kila mfanyakazi hata awe wa muda
mfupi au wa kudumu, lazima apewe mkataba na stahiki zake zipatikane kwa wakati,
ikiwemo mishahara na kupelekewa stahiki zake kwenye mifuko ya hifadhi ya
jamii,” alisema.
Aliwataka wawekezaji kuboresha mashamba na viwanda
pamoja na kuwapa mikataba wafanyakazi ili waweze kupata haki zao kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment