WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amepiga marufuku
mawakala kutumika kununua mazao ya wakulima kwa niaba ya Hifadhi ya Taifa ya
Chakula (NFRA) kutokana na mawakala hao kubainika kununua mazao ya wakulima kwa
bei ya chini.
Imeelezwa kuwa mawakala hao wananunua mahindi
kwa wakulima kwa bei ya sh. 180, kisha kuyauza NFRA kwa sh. 500, hivyo
kusababisha wakulima kushindwa kunufaika na bei hiyo inayotumiwa na serikali
kununua mazao hayo.
Kufuatia uamuzi huo, Waziri Mkuu ameiagiza
NFRA kuweka vituo vya ununuzi wa mazao kwenye vijiji na kuhakikisha wanasambaza
magunia ya kuhifadhia mahindi kwa wakulima ili waweze kuuza mazao yao kwa bei
iliyopangwa na serikali.
Aidha, amesema serikali itaanda utaratibu
maalumu wa kusambaza pembejeo za kilimo, badala ya kuwatumia mawakala, ambao
wengi wao wamekuwa sio waaminifu na kusababisha malalamiko kutoka kwa wakulima.
Majaliwa alitoa agizo hilo juzi, wakati
akikagua kituo cha kuhifadhia chakula mkoani hapa, ambapo alisema serikali
haiwezi kuvumilia wakulima wakinyonywa na mawakala wenye kujali maslahi
binafsi.
Alisema wakulima waendelee kulima mazao yao,
hususan mahindi na serikali itayanunua kwa bei ya soko moja kwa moja pasipo
kutumia mawakala.
“Haiwezekani mkulima alime mahindi kwa shida halafu
wakala ayanunue kwa bei ya chini na kuyauza serikalini kwa sh. 500. Hii
haivumiliki, hivyo NFRA kwenye msimu huu wa kilimo lazima mfungue vituo vya
kununulia mahindi vijijini.
“Tunataka mkulima anufaike na bei iliyopangwa
na serikali na sio mawakala, kama mawakala wanataka kunufaika na bei hiyo ya
serikali nao watafute mashamba yao ya kulima,” alisisitiza.
Majaliwa alitoa agizo kwa wakuu wa mikoa
wanaotoa vibali kwa mawakala vya kununulia chakula kwa ajili ya kusambaza
kwenye maeneo yaliyokumbwa na upungufu wa chakula, kuhakikisha chakula hicho
kinafikishwa kwenye maeneo yaliyokusudiwa.
Aliongeza kuwa serikali itahakikisha hakuna
mwananchi atakayepoteza maisha kwa kukosa chakula kwa sababu chakula kipo cha
kutosha.
Awali, kabla ya Waziri Mkuu kutoa maagizo hayo,
mbunge wa Songea Mjini, Leonidas Gama na mbunge wa jimbo la Peramiho, Jenista
Mhagama, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge,
Ajira na Walemavu, walisema mawakala wamekuwa wakinufaika na bei ya mahindi
iliyopangwa na serikali huku wakulima wakiendelea kunyonywa.
Wabunge hao walisema mfumo unaotumika na NFRA
kununua mazao, hususan mahindi, haumnufaishi mkulima kwa sababu mawakala
wamekuwa wakinunua mahindi kwa wakulima kwa wastani wa bei ya sh. 180 hadi sh. 200
kwa kilo.
Waliongeza kuwa licha ya wakulima kujitahidi
kulima mahindi, bado hakuna soko la uhakika, hivyo waliiomba serikali kuweka
utaratibu kwa wakulima wadogo kuuza mahindi kwenye hifadhi hiyo ya chakula.
Baada ya Waziri Mkuu kutoa kauli hiyo,
wakulima wa mkoa wa Ruvuma waliipongeza serikali ya awamu ya tano kwa
kuzingatia maslahi ya wananchi.
Mkulima wa mahindi mkazi wa Peramiho, Ruth
Michael, alisema maamuzi hayo yamewafanya kupata nguvu zaidi ya kulima mahindi
kutokana na kupata uhakika wa soko la mazao yao.
“Waziri mkuu ametuongezea kasi ya kuendelea
kulima mahindi kwa kuwa mawakala waliokuwa wakituvunja moyo kwa kununua mahindi
kwa bei ya chini sasa mwisho wao umefika. Tutalima mahindi na kuyauza wenyewe
kwa bei iliyopangwa na serikali na sio ya mawakala,” alibainisha.
Alisema walikuwa wakiuza mahindi kupitia kwa
mawakala kwa bei ya chini kwa sababu walikuwa hawana sehemu nyingine ya kuuzia
mazao yao.
No comments:
Post a Comment