Tuesday 8 September 2015

SHAKA: ICHAGUENI CCM KUWAENZI NYERERE NA KARUME




Na Mwandishi Wetu

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema kutoichagua CCM iliyotokana na vyama vyama vya ukombozi vya TANU na ASP ni kusaliti juhudi na fikra za waasisi wa Taifa hili, marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema hayo jana wakati akizungumza na wanachama wa CCM na jumuia zake  katika kijiji cha Lusinza, kata ya mtitu, wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Alisema wananchi wazalendo wa Tanzania Bara na Zanzibar, wana deni lisilolipika la kuendeleza jukumu  la kuthamini michango iliyotolewa na wapigania uhuru hao waliopambana na wakoloni hadi kupatikana uhuru mwaka 1961 na Mapinduzi mwaka 1964.

"Pamoja na serikali ya CCM kutekeleza Ilani ya uchaguzi, kusimamia malengo ya maendeleo kisiasa, kijamii na kiuchumi, wananchi wa Bara na Zanzibar wana dhima ya kuwaenzi Mwalimu Nyerere na Mzee Karume kwa kuichagua CCM," alisema Shaka.

Aliwaeleza wanachama hao  kuwa juhudi, bidii na ushupavu uliofanywa na waasisi hao kupitia TANU na ASP, ndiyo uliowakomboa wananchi wa pande mbili za Muungano na kuwapatia hadhi, heshima na thamani ya utu wao.

Shaka alisema wanasiasa  wa upinzani wanaopita sasa nchini na kusema wanapigania mabadiliko na ukombozi, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa ufisadi, Edward Lowassa, wanahitaji kupuuzwa kwa madai hawajui wanachokitafuta na kukipigania.

"Ikiwa Lowassa na Sumaye wamekwenda  CHADEMA kupigania maslahi binafsi na dhambi walizowatendea watanzania, hilo suala jingine, ukombozi wa waafrika na uhuru wao umeletwa na vyama vya TATU na ASP," alisema Shaka.

Kaimu huyo Katibu Mkuu wa UVCCM aliwataka wanachama wa  CCM kumpuuza Lowassa kwa madai anayoyatoa kwamba alihama CCM baada ya taratibu za kumpata mgombea urais kukiukwa huku  akisema madai hayo hayana misingi na mashiko.
Shaka alisema Lowassa ameteuliwa kuwa mgombea wa
urais bila kuthibitishwa na kupitishwa na mkutano mkuu wa CHADEMA na kuongeza kuwa, kupitishwa kwake kuligubikwa na harufu ya mizengwe na uchakachuaji wa demokrasia.

"Kama anasema vikao vya CCM vilibaka matakwa ya
demokrasia kumpata mgombea urais, CHADEMA walichakachua misingi na dhana kamili ya demokrasia. Dunia ijue  CCM haikuwa tayari kupitisha
mgombea mwenye makandokando mbele ya jamii,”  alieleza huku akishangiliwa na wananchi.

Akizungumzia Sumaye, alisema mwanasiasa huyo kukaa kwake miaka 10 akiwa waziri mkuu, ilikuwa ni hisani na huruma ya Rais Benjamin  Mkapa, lakini akasema hakuwa na vigezo , uhodari wala viwango vya kushika wadhifa huo.

Aidha, Shaka  aliwataka wananchi wa Kilolo kumpigia kura za urais mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli kutokana historia yake ya utumishi wa umma kuwa ya uaminifu, uadilifu na uchapakazi.

Pia, aliwataka wamchaguae mgombea ubunge, Venance  Mwamoto  wa CCM kuwa mbunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment