Wednesday 23 September 2015

WAFANYABIASHARA WA MBOWE WANAJIFICHA NINI?





Na Doto Magori
AKIZUNGUMZA Jumanne kwenye hafla ya taasisi ya Twaweza, kutangaza matokeo ya utafiti wake kuhusu hali ya kisiasa nchini juzi, jijini Dar es Salaam, mwanaharakati Maria Sarungi katika tathmini yake, alisema jina la mgombea wa CCM wa urais, Dk John Magufuli, linafahamika sana kutokana na kujitangaza zaidi.
Alisema misuli ya kifedha iliyonayo CCM ndiyo inafanya kuweza kujitangaza zaidi kupitia mabango na vyombo mbalimbali vya habari, kwa maana ya magazeti, redio na televisheni.
“Ukienda sehemu mbalimbali nchini na hasa vijijini, hukosi kukuta mabango ya Magufuli na hivyo ukimhoji mtu nani unadhani anafaa kuwa Rais na hata kama hujamtajia majina, atamtaja Magufuli…lakini hata hivyo matokeo haya si utabiri wa matokeo ya uchaguzi,” alisema Maria.
Kauli yake ilitokana na ya Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, kwamba katika swali la unadhani nani anafaa kuwa Rais, hakukuwa na jina lililotajwa, ila kura zilikwenda kwa Magufuli na Edward Lowassa, anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ni kweli kuwa CCM ina misuli kuliko Ukawa, licha ya umoja huo kushirikisha vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, huku vitatu vya mwanzo vikipata ruzuku ya serikali kutokana na kuwa na wabunge.
CCM ina miradi mingi ambayo ni vyanzo vyake vya fedha, ingawa hilo halikatazi vyama vingine kuwa na miradi kama hiyo, pamoja na ndani ya vyama vya siasa kuwapo viashiria vya ulaji, huku tukisikia malalamiko kuwa baadhi ya viongozi wanapokea fedha za ruzuku na misaada mingine kutoka nje na kuishia mifukoni wao.
Bila shaka Ukawa baada ya kubaini kuwa hali yake ya kifedha ni hoi na kwamba huenda ikasuasua katika kukamilisha kampeni kabla ya upigaji kura Oktoba 25, mwaka huu, ikaamua kuitisha harambee iliyofanyika Dar es Salaam, ambapo taarifa zilisema ilihudhuriwa na watu 800.
Harambee hiyo ilikusanya jumla ya Sh milioni 97, kwa mchanganuo kuwa Sh milioni 67, zikiwa ni ahadi ndani ya ukumbi, Sh milioni 20, zikichangwa kwa njia ya simu na Sh milioni 10, zikikusanywa papo hapo ukumbini chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Ukawa na Chadema, Freeman Mbowe.
Mbowe akiongoza harambee hiyo, aliwajulisha washiriki kuwa tangu waanze kampeni, Ukawa wamekuwa wakisaidiwa na Watanzania mbalimbali wenye nafasi zao (kiuchumi), baadhi wakijitolea magari kwa ajili ya usafiri wa kampeni.
Alichoshangaza ni kutangaza kuwa kuna wafanyabiashara watano wenye uwezo mkubwa ambao hawakutaka watajwe majina, ambao wamekubali kuisaidia Ukawa kwenye kampeni zake kwa siku zilizosalia, lakini akasema hawakutaka kutajwa majina yao, kwa sababu eti wanaogopa kufuatiliwa.
“Wakati tunaendelea na uchangiaji hapa, nimepokea simu kutoka kwa rafiki zangu watano wenye uwezo mkubwa kiuchumi. Wameahidi kuchangia harambee, lakini wanaogopa kujulikana kwa kuhofia mkono wa Serikali,” alisema Mbowe.
Akaendelea huku akisikitika: “Inasikitisha Mtanzania mwenye uhuru ndani ya Taifa lake anahofia kuchangia safari ya mabadiliko kwa sababu ya kuogopa serikali, wakati serikali iliyopo imejaa mafisadi wakubwa.”
Kama alichokisema Mbowe si danganya toto, basi kuna tatizo miongoni mwa wafanyabiashara wanaoogopa kuichangia Ukawa, lakini pia na viongozi wetu, kwa sababu inawezekana kuogopa kumchangia jambazi au muuaji akafanye uhalifu kuliko kuchangia watu wema. Je, Ukawa ni miongoni mwa majambazi hao?
Hii ina maana kuwa wafanyabiashara hao wakichangia Ukawa, itasababisha matatizo katika nchi, hiyo bila shaka ndiyo imani waliyonayo nao wakajulikana kuwa wamechangia, la sivyo kwa nini wanajificha kwa madai kuwa Serikali itawabana? Inashangaza na kuacha maswali ya Ukawa inashirikiana na wafanyabiashara gani?
Umoja ambao unajumuisha mawaziri wakuu wawili wa zamani ndio sasa unashirikiana na wafanyabiashara watano wanaoogopa kujulikana kuwa wametoa mchango kusaidia umoja wa vyama vya siasa? Ni wapi pameandikwa kuwa wanakatazwa? Kwa nini wanajihisi hivyo na viongozi hao akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Upinzani Bungeni?
Naunga mkono kauli na hoja ya mwanaharakati wa mtandao wa TGNP, Gemma Akilimali, ambaye alipohojiwa alishangaa kauli ya Mbowe na kuhoji mbona mfanyabiashara Mustafa Sabodo amekuwa akiichangia Chadema na kujitangaza bila  matatizo na hakupata kufuatwa na serikali?
“Sabodo ni mfanyabiashara mkubwa tu na amekuwa akiwachangia Chadema na CCM waziwazi bila kificho na hatujaona lolote likimtokea. Hivyo hofu zao zinaweza kutujengea maswali katika uwazi wa shughuli zao,” alitanabaisha Akilimali.
Ni dhahiri kuwa kujificha katika harambee inamaanisha fedha walizonazo wafanyabiashara hao ni haramu na wanaogopa kuulizwa walizipata vipi na wapi na pengine hata kodi wamekuwa hawalipi. Je, ndio wale waliokuwa wakimchangia Lowassa na kupeleka makanisani akitaja kuwa ni “za marafiki zangu”?
Kuna watu wenye uwezo wao huenda katika nyumba za ibada na kutoa sadaka za mamilioni ya fedha, lakini hatujasikia hata siku moja Serikali ikiwafuata na kuwahoji sababu za kufanya hivyo, iweje leo wafanyabiashara hao wakubaliane kwa pamoja kwamba watachangia, lakini hawatataka kutangazwa.
Hapa kuna fumbo tata, pengine hawapo na kama wapo ni wezi au fedha hizo zinatoka kwingine hata nje ya nchi, lakini wanasingiziwa wafanyabiashara hewa ili kuzihalalisha. Ni vizuri pia hata kiasi cha fedha kingetajwa kwa sababu ni ahadi tayari kuliko kuficha, kwani wana Ukawa huenda wasijue ziliingia lini na kutumikaje.
Angalau hilo ni tatizo sugu lililoko ndani ya Chadema. Waliokikimbia chama hicho wanajua na waliomo wanajua, lakini wanachelea kulisema, kwa sababu wanajua pia nini kiliwakuta waliolijua wakalisema hadharani.

No comments:

Post a Comment