Wednesday 23 September 2015

MALECELA: WACHAFU WAMEONDOKA CCM, CHAMA KIMEBAKI IMARA




NA WAANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti Mstaafu wa CCM,  John Malecela, amesema makada wachache wachafu waliokuwa wakikitia doa Chama na kujali maslahi yao binafsi, wameondoka.
Amesema hatua hiyo ni nzuri kwa kuwa CCM sasa kitabaki na wanachama makini, waaminifu na wenye sifa, baada ya makapi kukimbilia upinzani kuendeleza wimbi la kusaka maslahi binafsi na kukata kiu ya uroho wa madaraka.
Aidha, amesema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ndiye chaguo sahihi la Watanzania kwa sasa kwani, ni mchapakazi na atayeleta mabadiliko ya kweli na ambayo Watanzania wanayahitaji na si porojo za wapinzani.
Amesema ana imani kubwa Dk. Magufuli atapata ushindi wa kishindo dhidi ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, anayegombea kupitia CHADEMA.
Mzee Malecela, ambaye kwa muda mrefu alikuwa kimya, aliyasema hayo jana nyumbani kwake Dar es Salaam, alipozungumza na UHURU katika mahojiano maalumu.
Alisema huu ni wakati muhimu kwa Watanzania na kuwaasa kuhakikisha wanachagua kiongozi bora na asiye na uchu wa madaraka kwa kuwa kuna wengine wanalazimisha kuingia Ikulu kwa nguvu wakati hawana uwezo na sifa.
“Kuna viongozi waliopoteza utu wao kwa kuhama CCM na kuingia kwenye genge ambalo halina sera wala dhamira ya kuwatumikia Watanzania zaidi ya kuangalia matumbo yao. Hawa ni wa kuogopwa na kukataliwa hadharani kabisa bila kificho.
“Sina shaka na Dk. Magufuli na Chama kimechagua mtu ambaye alikuwa akihitajika kwa maendeleo ya Tanzania. Ninamfahamu na ninamwamini,” alisema.
Alisema Dk. Magufuli ameitumikia serikali kwa miaka 20, anafahamu matatizo ya Watanzania wanyonge kwani, licha ya kuwa waziri miaka yote hiyo hakuwa mtu wa kujikweza wala kuishi maisha ya kifahari.

HOFU YA VURUGU
Hata hivyo, Mzee Malecela alionyesha hofu kuwa genge la UKAWA huenda likaanzisha vurugu kutokana na dalili za mgombea wao kushindwa kuonekana mapema.
Amesema Lowassa hana ubavu wa kupambana na Dk. Magufuli kwa kuwa tayari ana kashfa na haonekani kuwa imara kiafya, tofauti na mwenzake ambaye anakubalika kila kona.
Pia, amesema njia nyingine ambayo huenda ikatumiwa na UKAWA ni kupanga mikakati ya kuahirishwa kwa uchaguzi.
“Hawa tayari wameshikwa pabaya…mgombea wao hana sifa za kumshinda Dk. Magufuli na wenyewe kwa wenyewe ni vurugu humo ndani wakigombea madaraka.
“Wameshindwa kufikia malengo waliyojiwekea katika hatua za mwanzo tu, sasa ikitokea wakapewa nchi si watapigana wakitaka kugawana vyumba vya kulala Ikulu,” alisema.

No comments:

Post a Comment