Wednesday 23 September 2015

DK: MAGUFULI NGANGARI, AMSHANGAA LOWASSA




MGOMBEA Urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema kitendo cha mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, kuahidi kuwaruhusu wafanyabiashara kuuza kahawa Uganda hakina maana wala tija kwa wakulima nchini.
Aidha, Dk. Magufuli jana alidhihirisha kuwa ni mzee wa kazi na yuko ngangari idara zote, pale alipopanda jukwaani na kuanza kupiga ‘push up’.
Tukio hilo lililoamsha shangwe kila kona ya uwanja wa Kayanga, wilayani Karagwe, Dk. Magufuli aliwaomba wananchi wamchague kwa sababu ana nguvu za kuendesha serikali makini na hata kiafya yuko imara tofauti na wengine.
Akizungumzia zao la kahawa akiwa wilayani Misenyi, katika Jimbo la Nkenge, Dk.  Magufuli alisema kuuza kahawa nje ni kushindwa kuimarisha uchumi wa ndani.
Alisema ili kuhakikisha bei ya kahawa inaongezeka, atapunguza kodi ambazo ziko 26.
Alisema kodi hizo ndizo zinazofanya bei ya kahawa kuwa chini, na anamini ikiwa juu, hata wafanyabiashara wa Uganda watafuata bidhaa hiyo Tanzania.
Kuhusu suala la vizuizi vilivyopo ofisi ya Mamlaka ya Mapato Misenyi, mgombea urais alisema atalitafutia ufumbuzi ili vikwazo hivyo viishe.

Fidia kwa wananchi
Kuhusu fidia kwa wananchi waliobomolewa nyumba kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege Misenyi, Dk Magufuli alisema atahakikisha wanaostahili kulipwa wanapata haki yao kwa mujibu wa sheria ya ardhi.
Aidha, alisema mgogoro wa ranchi unaendelea kufanyiwa kazi na Mkuu wa Mkoa, John Mongella na ana imani kubwa ufumbuzi wa haraka utapatikana na hakuna anayeonewa.
Aliahidi kujenga barabara kutoka Karagwe mpaka Benako yenye urefu wa kilomita 100.
Lakini, mgombea huyo aliwaomba wananchi wa Karagwe wamchague Innocent Bashungwa awe mbunge wa Karagwe.
Aliwataka wale wa Jimbo la Nkenge, wampe kura za kutosha Diodurus Kamara ili awe mbunge.
Aliendelea kuwakumbusha wananchi wa maeneo mbalimbali ya Kagera, kutowachagua viongozi wasio na kumbukumbu na wasio na uchungu na nchi.
Alisema hata shule za Kata zimejengwa na serikali ya CCM, lakini inashangaza kuona baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakizipinga kwenye majukwaa.
Mbali ya kufanya mikutano katika majimbo ya Karagwe na Misenyi, Dk. Magufuli alihutubia Kyerwa, ambako alimuombea kura mgombea ubunge, Innocent Bilakwate.
Dk Magufuli, amemaliza majimbo tisa ya mkoa wa Kagera. Mengine ni Bukoba Mjini, Vijijini, Muleba Kusini na Muleba Kaskazini.

MSUKUMA AFUNGUKA TENA
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku, maarufu kama Msukuma, amemponda Lowassa akiwataka wananchi kutomchagua kwa kuwa hana sifa za uongozi.
Aidha, alifichua kuwa hata mikutano yake ya kampeni ambayo amekuwa akiihutubia, hutanguliza fedha kwa ajili ya kuwaandaa wananchi.
"Naomba niwaambie, mimi ndiye najua siri kubwa za Lowassa… huwa wanatanguliza fedha kabla ya kuanza kuhutubia,” alisema Msukuma.
Aliwataka wananchi kuendelea kuchukua fedha za mgombea huyo kwa kuwa ni sehemu ya zile zilizoporwa na mafisadi, hivyo hawana sababu ya kuziacha.
Hata hivyo, aliomba wananchi kufanya uamuzi sahihi kwa kumchagua Dk. Magufuli kwani, ndiye anastahili kuwa kiongozi wa nchi kutokana na uchapakazi wake.
Pia, aliwaponda wenyeviti wa zamani wa CCM, Mgana Msindai (Singida) na Khamis Mgeja (Shinyanga) kuwa ni makapi yasiyostahili kusikilizwa bali kupuuzwa.
Alimtaja Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha kuwa naye ni mzigo na hana uwezo kwenye siasa.

No comments:

Post a Comment