Na Hamis Shimye, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohamed Shein, amesema ujenzi wa bandari mpya eneo la Mpigaduri, Unguja,
utaanza mapema mwakani.
Amesema fedha za ujenzi wa
bandari hiyo ziko mbioni kupatikana kutoka Benki ya Exim ya China, ambayo
imeonyesha nia ya kuikopesha serikali dola milioni 222 (takriban sh. bilioni
490).
Mbali na kuanzwa kujengwa
kwa bandari hiyo, Dk. Shein pia amesema atajenga bandari ya Wete, Pemba na
kuiboresha bandari ya Mkoani iliyoko pia kisiwani humo.
Dk. Shein aliyasema hayo
kwenye uwekaji wa jiwe la msingi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan
Karume. Uwanja huo unajengwa na Serikali
ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa mkopo kutoka China.
Alisema serikali yake
imepanga mambo mbalimbali kuhakikisha inaboresha miundombinu kwa kuwa bila
miundombinu imara hakuna maendeleo bora.
"Ujenzi wa bandari
hiyo si suala la jana au leo, bali lilianza toka kwa Mzee wetu Dk. Salmin Amour
ambaye alitaka kujenga bandari eneo hilo. Sasa ndoto hiyo imekamilika na ujenzi
utaanza mwakani,''alisema.
Alisema alipokutana na
Rais wa China, Xi Jinping, alimwomba kujenga bandari hiyo na kukubali na tayari
kuna kampuni ilishafanya upembuzi yakinifu.
Dk. Shein alisema anaamini
bandari hiyo itakapokamilika itasaidia kuongeza mapato ya Zanzibar kwa kuwa
itakuwa na uwezo mkubwa wa kubeba watu na itaendana na ushindani wa kimataifa.
"Tumenuia pia kujenga
bandari ya Wete kupitia mwekezaji wa ndani, ambaye tayari ameshapatikana na
muda ukifika ataanza ujenzi huo huku pia bandari ya Mkoani nayo ikiendelea
kuboreshwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Shein, ujenzi
wa bandari hiyo unatokana na bandari iliyoko Malindi kuwa ndogo na kunahitajika
kujengwa kubwa yenye uwezo wa kupokea na kusafirisha wageni pamoja na mizigo.
Usafiri wa ndege Pemba
sasa kufanyika pia usiku
WANANCHI wa Pemba na
Unguja wataanza kusafiri kwa ndege usiku katika kiwanja cha ndege cha Pemba,
baada ya miezi miwili kukamilika kwa uwekaji wa taa kwenye kiwanja hicho.
Pia uwanja huo ndani ya
muda mfupi utajengwa zaidi na kuwa wa kisasa kwa kuboresha na kupanua njia za kurukia
ndege na utuaji ili kusaidia ndege nyingi kutua kwa wakati.
Ahadi hiyo ilitolewa jana
na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, ambaye pia ni mgombea wa Urais wa
CCM Zanzibar, ambapo alisema amenuia kukoboresha kiwanja hicho na kuwa na cha
kisasa.
Alisema hivi sasa ndege
nyingi haziwezi kutua usiku kwenye kiwanja hicho, hivyo ukarabati na uwekaji wa
taa umeshaanza na kuahidi kuwa ndani ya
miezi miwili kila kitu kitakuwa vizuri.
"Nawaambia ndugu
zangu wa Pemba na Unguja, sasa mtaweza kutua na kusafiri kwa ndege hata usiku
kwenye kiwanja chetu cha ndege cha Pemba
kwa kuwa ujenzi wake unakaribia kwisha,” alisema.
Dk. Shein alisema licha ya
kuweka kwa taa hizo kwenye kiwanja hicho, pia ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha
ndege cha Pemba nao utafanyika.
No comments:
Post a Comment