Tuesday, 27 October 2015

CCM YAZOA MAJIMBO YOTE MWANZA NA GEITA




NA PETER KATULANDA, GEITA
WAGOMBEA ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majimbo ya mkoa wa Geita, wameligaragaza kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo hayo, Ali Kidwaka, katika jimbo la Geita Vijijini, Mwenyekiti wa CCM mkoani Geita, Joseph Kasheku, maarufu kama Msukuma, ameibuka mshindi baada ya kupata kura 44,313, sawa na asilimia 68.
Msukuma amewapiga wapinzani wake Mangilima Augustine (CHADEMA), aliyepata kura 18,909 huku mgombea wa CUF, Malugu Magese akiambulia kura 1,786.
Katika jimboni Busanda, Lolesia Bukwimba (CCM), aliyezoa kura 63,043, ametetea kiti chake kwa kuwabwaga Mawazo Chemu wa CHADEMA, aliyejivuta na kupata kura 45,019, akifuatiwa na Ngofuma Msafiri aliyeambulia kura 1,532.
Jimbo la Geita Mjini, Costantine Kanyasu (CCM), alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura 34,653, sawa na asilimia 55.1, akifuatiwa na mgombea wa CHADEMA, Rojas Luhega aliyepata kura 26,303, sawa na asilimia 41.5 na Peter Malebo wa CUF aliyepata kura 625.
Katika jimbo Mbogwe, Augustine Masele (CCM) ameshinda kwa kura 32,921 na kumuacha mbali mpinzani wake wa karibu, Nicodemas Maganga wa CHADEMA, aliyepigiwa kura 13,975 na Andrew Mnuke wa ACT Wazalendo alijipatia kura 5,464.
Jimbo la Nyang’wale, CCM iliibuka kidedea baada mgombea wake Hussein Amar kupigiwa kura za kishindo 36,249 na kuwagaragaza vibaya wagombea Fortunatus Malya wa CHADEMA aliyepata kura  9,886 huku mgombea wa ACT Wazalendo akipata kura kiduchu 350.
MWANZA
Mkoani Mwanza majimbo ya Ilemela, Nyamagana na Ukerewe yaliyokuwa yakikaliwa na CHADEMA, yote yamerejeshwa CCM na kuyafanya majimbo yote ya mkoa huo yawe chini ya CCM.
Nyamagana, Ezekia Wenje aliangukia pua baada ya kugaragazwa na Stanslaus Mabula (CCM), aliyepata kura 81,012. Wenje ambaye awali aligomea matokeo hayo na kusababisha yatangazwe saa 7 usiku, alipata kura 79,280 akifuatiwa na mgombea wa CUF aliyepata kura 1,005.
Angelina Mabula (CCM) naye aliibuka kidedea kwa kura 85,424 jimboni Ilemela baada ya kumg’oa Highness Kiwia wa CHADEMA aliyepata kura 51,679, akifuatiwa na mgombea wa ACT Wazalendo aliyepata kura 3,910.
Shanif Mansoor (CCM) wa jimbo la Kwimba, amemfanyia mauaji mgombea wa CHADEMA, Shilogila  Babila aliyepewa kura 7,338 huku Mansoor alimwagiwa kura 39,367 na mgombea wa CUF, Ntinga Julius akipigiwa kura 4,076.

No comments:

Post a Comment