NA SHAABAN MDOE, LONGIDO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani
Longido, kimepinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo yaliyompa ushindi mgombea wa
CHADEMA, Onesmo Nangole, kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika
zoezi zima la upigaji kura, kuhesa na kutangaza matokeo.
Akizungumza na vyombo vya habari
jana, katika ofisi za CCM mkoa wa Arusha, Katibu wa wilaya hiyo, Esupatu
Naikara, alisema zoezi la uchaguzi tangu upigajikura, halikuwa la haki na amani
kutokana na vurugu mbalimbali zilizokinzana na sheria za uchaguzi walizotia saini.
Aliitaja moja ya kasoro hizo kuwa ni
ukiukwaji wa sheria ya mawakala, ambayo inakitaka kila chama kuweka wakala
mmoja katika kila kituo, ambapo CHADEMA kiliweka mawakala zaidi ya 15 hadi 20 katika
kituo kimoja hali iliyozua vurugu vituoni.
Alisema hali hiyo ilionekana zaidi katika maeneo ya nje ya mji, ambapo mawakala hao walikuwa wakifanya fujo vituoni wakati wote wa upigaji kura, kuhesabu pamoja na utangazaji matokeo.
Katibu huyo alisema polisi na
msimamizi mkuu wa jimbo walipoelezwa kuhusu hali hiyo, hakukua na hatua zozote
zilizochukuliwa.
Naikara alisema kutokana na hali
hiyo, Chama kilijaribu kuongeza idadi ya mawakala ili kukabiliana na vurugu
zilizokuwa zikisababishwa na mawakala hao, lakini askari wa jeshi la polisi waliwazuia,
hali iliyoonyesha wazi kuwa kulikuwa na njama kati ya polisi na CHADEMA.
Alisema mapema jana asubuhi walipofika katika ofisi za halmashauri ili kusikiliza matokeo, walimkuta mgombea wa CHADEMA ndani ya chumba cha kujumlishia matokeo, lakini walipotaka kuingia, walizuiliwa hali iliyosababisha watumie nguvu.
Naikara alisema baada ya kuingia
kwenye chumba hicho kwa nguvu, mgombea huyo wa CHADEMA alianzisha fujo, ikiwa
ni pamoja na kuzimwagia maji karatasi za kura.
Kutokana na hali hiyo, msimamizi
mkuu wa uchaguzi, ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri, aliwataka wote kutoka
nje, ambapo walikubali, lakini walipokuwa wanaelekea nje ya eneo hilo, mgombea
huyo wa CHADEMA alibaki nyuma.
Katibu huyo alisema baadaye
walimpigia simu mkurugenzi huyo kutaka kujua hali inaendeleaje, lakini
aliwajibu kuwa watume wakala mmoja kwa ajili ya kujua kinachoendelea.
“Tulipojibiwa hivyo, tukaamua kwenda
pamoja na tulipofika tulimkuta mkurugenzi huyo mlangoni, ambapo alimkabidhi
mgombea wa CCM karatasi ya matokeo aliyoyatangaza bila sisi kuwepo,”alisema.
Alisema alishangazwa na kitendo
hicho na walipotaka kumuuliza sababu za kutangaza matokeo bila wao kuwepo,
alitokea mlango wa nyuma na kutokomea kusikojulikana.
Kufuatia hali hiyo, Naikara alisema Chama pamoja na mgombea wake, wamegomea matokeo hayo na kuamua kukata rufani kuyapinga kutokana na kukiukwa kwa baadhi ya taratibu muhimu.
Akizungumzia matokeo hayo, mgombea
wa CCM alisema hakubaliani nayo kutokana na ukweli kwamba ni ya kupikwa kwa
vile hayakuwa na saini yake.
Aliitaja sababu nyingine iliyomfanya
kuyakataa matokeo hayo kuwa ni idadi ya kura walizopata wagombea wote na zile
zilizoharibika zinazidi idadi ya wapiga kura halali.
Alitaja idadi ya wapigakura halali kuwa ni 40,606, kura halali zilikuwa 39,988 na zilizoharibika 767, wakati mgombea wa CCM alipata kura 19,352, CHADEMA kura 20,076, CUF 307 na ACT kura 253, ambazo zikijumlishwa zinazidi wapigakura halali.
Mapungufu mengine ni kuchelewa kwa masunduku ya kura hata kwa maeneo ya jirani, ambayo yalifika jana saa tano usiku juzi na saa moja asubuhi jana pasipo kuwepo na ulinzi wowote wa polisi.
Alisema masanduku hayo yalionekana yakibebwa na magari ya watu binafsi, ambao ni wafuasi wa CHADEMA na kwamba walitoa taarifa kwa mkurugenzi wa halmashauri, ambaye alipuuzia malalamiko hayo hali iliyoonyesha kuwepo kwa dalili za rushwa.
No comments:
Post a Comment