Wednesday, 28 October 2015

WAANGALIZI WAPONGEZA MCHAKATO WA UCHAGUZI



WAANGALIZI wa uchaguzi kutoka  Jumuia ya Madola  na ya Maendeleo ya Nchi za Kusini kwa Afrika (SADC), Kamati ya Bunge la Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuia ya Umoja wa Nchi za Ulaya (EU),  wamepongeza kuwa uchaguzi mkuu wa Tanzania, umefanyika kwa amani, utulivu, huru na haki.

Wamesema ushindani katika uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki na kwamba, kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza zinaweza kurekebishwa kwenye chaguzi zijazo kwa kuwa hazina madhara.

Mkuu wa Wasimamizi wa Jumuia ya Madola, ambaye ni Rais Mstaafu wa Nigeria, Goodluck Jonathan,  amesema uchaguzi umekwenda vizuri kuanzia mchakato wa kampeni zake, upigaji kura na hatua ya kuhesabu na kutangaza matokeo.

Akizungumza mjini Dar es Salaa, jana, wakati wa kutoa tathimini kuhusiana na uchaguzi huo, aliipongeza serikali kwa kuandaa vizuri mazingira ya uchaguzi huo pamoja na matumizi ya mfumo wa uandikishaji wapigakura wa BVR, uliotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ZEC kwa upande wa Zanzibar.

"Tunaipongeza  Tanzania kwa kufanya uchaguzi huru, wazi na wa haki ambapo hatua zote zimefanyika kwa mujibu wa sheria. Tanzania inaonyesha kukomaa kidemokrasia na idadi kubwa ya Watanzania walijitokeza kushiriki kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.

"Licha ya kasoro chache, tunaipongeza NEC na ZEC kwa maandalizi na usimamizi makini na wa kitaalamu katika hatua zote hadi kutangaza matokeo," alisema Jonathan.

Alisema kasoro zilizojitokeza ni za kawaida na zinarekebishika katika uchaguzi ujao, ingawa zingine zilirekebishwa haraka ikiwemo baadhi  ya watu kutoona majina yao katika daftari la kudumu la mpigakura, lakini walijaza fomu maalumu na kupigakura.

Alitaja kasoro nyingine kuwa ni kutofunguliwa kwa kituo kimoja wilayani Kinondoni, baada ya wasimamizi wa uchaguzi kutoonekana na kuwa jana walishuhudia kura zikipigwa kituoni hapo.
"Maoni yetu ni kwamba uchaguzi umekwenda vizuri sana na kwa mpangilio, bado tupo hadi hatua ya mwisho ya kutangaza matokeo kamili…tunafuatilia hali halisi ya Zanzibar na tutatoa maoni yetu ya mwisho," alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa SADC, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Msumbiji, Oldemiro Baloi, alisema wameshuhudia uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa Sheria za Tanzania na za SADC uliozingatia demokrasia.

"Tunaipongeza Tanzania na Watanzania wote kwa kuendesha vizuri uchaguzi kwa zaidi ya asilimia 90. Hatua zote za uchaguzi zimefanyika katika hali ya utulivu na amani, uwazi na haki," alisema.

Alizitaka nchi nyingine kuiga mfano wa Tanzania kwa kudumisha amani na kuwa na uvumilivu katika hatua zote za uchaguzi, licha ya kasoro ndogo zilizojitokeza.

Alisifu wagombea kwa uvumilivu wa kisiasa wakati wa kampeni, kuvumiliana licha ya wakati mwingine kutoleana maneno  makali,  jambo ambalo halikuzua uvunjifu wa amani.

"Ni kweli tumeshuhudia wakati huu wa kutangaza matokeo katika baadhi ya maeneo vijana walianzisha vurugu, lakini pia tunalipongeza Jeshi la Polisi kwa kujipanga vema na kuwatuliza," alisema.

Mwenyekiti wa ICGLR, Injinia Peter Mosilet, aliisifu Tanzania kwa kuandaa uchaguzi huru na wa haki kwa kuzingatia utawala bora.

"Utangazaji matokeo umeonekana kwa kiasi kikubwa kukidhi matakwa ya wananchi ndio sababu hali ya amani inatawala hadi sasa," alisema.

Alivitaka vyombo vya habari kuendelea kuripoti vizuri wakati huu na baada  ya uchaguzi,  ili kudumisha amani.

Hata hivyo, miongoni mwa dosari walizoziona, alisema ICGLR, inaishauri Tanzania kwenye uchaguzi ujao, kuhakikisha inaandikisha wapigakura na kutangaza matokeo mapema ili kuondoa malalamiko.

Tathimini ya Ulaya
Kiongozi wa  waangalizi hao Judith Sargentini, ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Ulaya, alisema walihudhuria shughuli 139 za kampeni nchini kote ambapo, baadhi ya vyombo vya habari vilitoa habari bila upendeleo kwa wagombea wote.

Alisema EU EOM ilikuwa na waangalizi 141 nchi nzima ambao walikwenda mikoa yote ya Tanzania katika siku ya uchaguzi na kuwa Watanzania wengi wametumia haki yao katika kupiga kura wakionyesha dhamira yao ya kuunga mkono mchakato wa kidemokrasia.

"Uchaguzi umefanyika vizuri na NEC na ZEC zote kwa pamoja zilijiandaa vizuri, lakini kuna masuala kadhaa ambayo hayakufanyiwa kazi katika uchaguzi uliopita, ambapo ni kutokuruhusiwa kikatiba kwa wagombea binafsi na kutokuweza kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais ambayo hayaendani na misimamo ya kimataifa kwa chaguzi za kidemokrasia," alisema.

Sargantini alisema bado wanaendelea kufuatilia uorodheshwaji wa matokeo, lakini pia NEC na ZEC hazikuonyesha uwazi katika uendeshaji wa hatua tofauti.

Alisema wawakilishi wa vyama vya siasa walikuwepo katika vituo vyote walivyoangalia jambo ambalo lilichangia kuwepo kwa uwazi na imani juu ya mchakato wa kupiga kura wa upigaji kura.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Bunge la Ulaya, Ines Sender aliwahimiza Watanzania wote kufanya kazi kwa kushirikiana katika maisha ya kisiasa na ujengaji amani na utulivu na uimarishaji wa taaisisi zinazounga mkono demokrasia.

No comments:

Post a Comment