Na Anita Boma, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, amewaomba
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutofanya maandamano ya kumtaka
Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Ahmed Sawa, kurejesha kura alizozigawa kwa
mgombea ubunge wa CHADEMA.
Wanachama na wafuasi wa CCM, walianza kujikusanya
kuandamana kushinikiza Sawa kurejesha kura hizo alizoziongeza kwa Mchungaji
Peter Msigwa, ambazo walisema kuwa zimehujumiwa kutoka kwa mgombea wao,
Fredrick Mwakalebela.
Wameonya kuwa kamwe hawatakuwa tayari kuona msimamizi
wa uchaguzi huo akishindwa kutenda haki na kufanya vitendo vya hujuma.
Amina aliyasema hayo jana kwenye Ofisi za CCM Wilaya ya
Iringa Mjini, akiambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Richard Kasesera, baada
ya kundi kubwa la wanachama hao kutaka kuandamana kupinga kile walichokiita ni
hujuma dhidi ya mgombea wao.
"Nimekuja hapa kwa mambo mawili, la kwanza kuwaasa
tusiandamane kwa sababu mambo bado…tuache kwanza sheria ichukue mkondo wake na
jimbo litarudi kwa amani. Aliyehusika kuhujumu matokeo ya mgombea wenu, sheria
itafuatwa ," alisema.
Alisema kuandamana inavuta usikivu wa kila mmoja na
hawezi kujua wataweza kufanyiwa nini na wenzao wa upande wa pili, hivyo kila
jambo linalotakiwa kufanyika kisheria litafanyika na kuwa Katibu wa CCM Mkoa na
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, wanalifanyia kazi na hivyo wanatakiwa
kuwa watulivu.
Aliongeza kuwa kutokana na hilo lililojitokeza na
malalamiko yanayomtuhumu mkurugenzi wa uchaguzi wa jimbo hilo, aliwaomba wana-CCM
kuendelea kusubili kwani sheria itaamua.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari ofini kwake, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, alisema katika uchaguzi huo, mkurugenzi wa uchaguzi ndiye chanzo cha kuhujumu na anatakiwa achukuliwe hatua.
Alisema msimamizi huyo ameharibu uchaguzi na bado
anaendelea kuharibu kwa kukataa kukubaliana na mgombea wa CCM, Fredrick
Mwakalebela kuhesabiwa upya maboksi ya kura ili kujiridhisha.
Mtenga alisema kama chama kilimuandikia barua na juzi walikutana naye pamoja na Mchungaji Msigwa na kumtaka kurudia upya kuhesabu, lakini alikataa na kudai kitakachofanyika ni kurudia uchaguzi katika kituo kimoja ambacho kura zake ziliibwa.
"Sisi hatuhitaji vurugu na wala mkurugenzi
asituletee vurugu, tuliondoka juzi mchana tukisubiri majibu ya ombi letu,
lakini badala yake saa nn usiku tulipata taarifa kuwa mkurugenzi alikuwa ofisini
akiwa na watu wa CHADEMA.
“Tulifika kwa haraka na tulimkuta akiwa na watendaji wake pamoja na viongozi wa upinzani
ndani ya chumba cha kujumlishia kura huku maboksi matano ya kura zikiwa zimemwagwa.
“Tulimuuliza kuhusiana na hatua hiyo, lakini hakuwa na
jibu sahihi ndipo tulipotoa taarifa polisi ambao walifika na kumchukua kwa
ajili ya mahojiano,” alisema Mtenga.
Alisema kutokana na matukio hayo na sintofahamu hiyo, CCM imekosa imani na msimamizi huyo kwa kuwa anaonekana kuegemea upande mmoja dhahiri.
Aidha, aliongeza kuwa msimamizi huyo amekuwa karibu na
Mchungaji Msigwa kila wakati na amediriki hata kumuacha akijitangazia ushindi
licha ya kura kutokamilika kuhesabiwa na kugubikwa na utata.
Tayari wagombea wa vyama vyote wameomba kuhesabiwa upya
kwa matokeo hayo, lakini msimamizi huyo amekuwa akiweka ngumu bila sababu za
msingi, jambo linalozidi kujenga hofu.
Alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, alikiri kuwepo
kwenye chumba cha kuhifadhi matokeo juzi usiku, lakini akadai walikuwa
wakijumlisha matokeo ya urais na si ubunge kama inavyodaiwa.
Pia, alidai kuwa hawezi kukubali kurudiwa kuhesabiwa
kwa maboksi ya kura kwa kuwa matokeo bado hayajatangazwa na kueleza kuwa
yaliyotangazwa na Mchungaji Msigwa si ya NEC bali ni ya kwake binafsi.
"Sijatoa matokeo bado ,
hivyo hawana sababu ya kutaka au kuomba kuhesabiwa upya. Jana usiku (juzi)
walikuja na ni kweli nilikuwa ndani na watumishi wa usimamizi wa ndani na nje
na nilikuwa tunajumlisha matokeo ya rais na ubunge bado hivyo, yale ya Msigwa ni yake mwenyewe,"
alisema na kukiri kuitwa na kuhojiwa polisi.
No comments:
Post a Comment