Wednesday, 28 October 2015

'VIJANA WA LOWASSA' WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA KUINGILIA MTANDAO WA NEC


 
Na Mwandishi Wetu
WATUHUMIWA wanane wakiwemo watatu raia wa kigeni kutoka nchi za Angola, Kenya na Korea, wanaodaiwa kutumiwa na CHADEMA kuingilia kazi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kukusanya na kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais, wamepandishwa kizimbani.
Mbali na shitaka hilo ambalo washitakiwa hao walisomewa jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, raia hao watatu wa kigeni, pia wanadaiwa kujiingiza katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya uchaguzi ya urais kwa chama cha CHADEMA, kinyume cha sheria.
Muda mfupi baada ya washitakiwa hao kufikishwa mahakamani hapo, viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA, akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zanzibar, Salum Mwalimu, walifika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ni Mashinda Mtei (49), mkazi wa Tengeru, Arusha, Julius Mwita (30), mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam na mtaalamu wa kompyuta Frederick Fussi (25), mkazi wa Mbezi Beach, Dar es Salaam.
Wengine ni  Julius Matei (45), mkazi wa Mwangazi-Kitui, Kenya, Mchungaji Meshack Mlawa (27), mkazi wa Keko, Dar es Salaam, Mhandisi Anisa Rulanyaga (41), mkazi wa Kawe, Dar es Salaam, raia wa Ufaransa, Jose Nimi (51), mkazi wa Paris, Ufaransa na mfanyabiashara Kim Hyunwook (42), mkazi wa Busan, Korea Kusini.
Washitakiwa hao walisomewa mashitaka matatu na Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi na Mawakili wa Serikali, Simon Wankyo na Paulo Kadushi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Katika shitaka la kwanza, ambalo linawakabili washitakiwa wote, wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Oktoba 25 na 26, mwaka huu, katika vituo mbalimbali Jijini Dar es Salaam, walisambaza kwa kupitia mtandao wa ‘National Election Management System’ wenye kichwa ‘M4C Election Results Management System’ na kwa kupitia mitandao ya kijamii, Facebook na Twitter, taarifa za uongo kuhusu matokeo ya urais.
Inadaiwa walifanya hivyo kwa lengo la kuudanganya umma wakati huu wa utangazwaji wa matokeo unaofanywa na NEC.
Shitaka la pili, Matei, Nimi na Hyunwook, wanadaiwa Oktoba 26, mwaka huu, kayika Hoteli ya King D, iliyoko wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, wakiwa raia wa Kenya, Angola na Korea na hati za kusafiria namba  A.1532119, 930879 na M 27687807 walijiingiza katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya urais kwa  CHADEMA, bila ya kuwa na vibali.
Mshitakiwa Matei anadaiwa pia siku hiyo, katika eneo lisilofahamika jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Kenya, alijiingiza katika shughuli za biashara kwa na niaba ya chama cha kuweka na kukopa WANAMA bila ya kuwa na kibali  halali.
Washitakiwa hao ambao wanatetewa na Wakili Peter Kibatala akishirikiana na Omary Msemo, walikana mashitaka hayo, ambapo Wakili wa Serikali Mkuu, Kakolaki aliieleza mahakama kwamba Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa washitakiwa.
Kakolaki alidai DPP amewasilisha hati hiyo kwa sababu za maslahi ya nchi na usalama wake, hivyo aliiomba mahakama washitakiwa hao wakae rumande wakati shauri hilo litakapokuwa likiendelea hadi pale Mkurugenzi wa Mashitaka atakapoamua kuiondoa.
Hata hivyo, Wakili Kibatala alipinga hati hiyo, kwa madai  kwamba haijasajiliwa mahakamani hapo, wakati hati hiyo inaanza kutumika pale inaposajiliwa.
Pia, alidai kifungu cha Sheria ya Makosa ya Mtandao, kilichotumika katika shitaka la kwanza, hakizalishi kosa hilo, hivyo hati hiyo ni batili. Aliiomba mahakama kuikataa hati hiyo na kutoa dhamana kwa washitakiwa.
Baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mwijage kusikiliza hoja za pande zote husika, aliahirisha shauri hilo hadi Ijumaa, ambapo atatoa uamuzi na washitakiwa walirudishwa rumande.
Juzi, mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, aliitisha mkutano na waandishi wa habari kulalamikia Jeshi la Polisi kuwakamata vijana hao waliokuwa wakifanya kazi ya kupokea na kujumlisha matokeo ya nchi nzima.
Alidai kuwa kazi iliyokuwa ikifanywa na vijana hao aliyowataja kwa idadi kuwa wapo 192, si kosa kisheria kwa sababu walikuwa na nia ya kufuatilia historia ya uchaguzi wa nchi yao.

No comments:

Post a Comment