JESHI la Polisi limewaonya vijana wanaoshawishiwa
kufanya fujo kwa kigezo cha kucheleweshwa matokeo, kuacha kufanya hivyo kwa
kuwa ni uvunjifu wa amani na sheria za nchi.
Pia, limesema limepata taarifa kuwa
kundi la vijana limetoka mikoa ya jirani kuja Dar es Salaam, kufanya vurugu
katika kipindi hiki cha uchaguzi na
kuonya kuwa watambue watakutana na mkono wa sheria.
Msimamo wa Polisi ulitolewa jana na
Kamishina wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Paulo Chagonja, katika mkutano
wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Chagonja alisema licha ya kuwepo kwa
vurugu kwenye maeneo mbalimbali, lakini Polisi inawapongeza wananchi kwa
kushiriki kwenye uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu mkubwa.
Alisema wanawapongeza sana wananchi,
lakini pia wanawatahadharisha vijana kuacha fujo kwa kigezo cha kucheleweshwa
matokeo, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo na Polisi.
"Tunawaonya vijana wanaoletwa na
viongozi wa vyama vya siasa kutoka mikoa ya jirani kuja Dar es Salaam kufanya
fujo. Tunawaonya na tunawataka vijana mbalimbali watulie na wafuate sheria,"
alisema.
Aliongeza kuwa vijana wote waliokamatwa
wakifanya fujo sehemu mbalimbali, watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria
za nchi na kuwataka kila mtu kutii sheria bila shurti.
No comments:
Post a Comment