Wednesday, 28 October 2015

LUBUVA: SITAKI MALUMBANO




MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema hataki malumbano na chama cha siasa au mgombea yeyote.
Pia, amesisitiza kwamba hakuna mgombea wala chama kinachopendelewa katika suala la kutangazwa kwa matokeo na mshindi atapatikana kwa kuwa na kura nyingi.
Amesema kinachofanywa na NEC ni kutangaza matokeo kama wanavyoyapata na hakuna mgombea anayependelewa.
Jaji Lubuva aliyasema hayo jana, baada ya kutokea kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama na wagombea waliodai NEC inapendelea katika kutoa matokeo.
“Hatupendi malumbano na chama wala mgombea, kama suala la kutumia busara sisi tuna busara sana na hatupangiwi kazi na yeyote, tunatangaza matokeo tuliyoyapokea na hakuna upendeleo,” alisema.
Aidha, Jaji Lubuva alizungumzia kuhusu suala la kutakiwa kutumia busara katika utangazaji wa matokeo, ambapo alisema wanatumia sana na wataendelea kutangaza matokeo kwa kadri wanavyoyapokea.
Mgombea wa urais kupitia CHADEMA, Edward Lowassa, juzi katika mkutano wake na vyombo vya habari aliilalamikia NEC kwa madai kuwa inatangaza matokeo kwa upendeleo.

No comments:

Post a Comment