Wednesday, 28 October 2015

HAKI ZA BINADAMU YAONYA WANASIASA




TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB),
imeeleza kusikitishwa na hatua ya baadhi ya wanasiasa kuingilia majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kwa kujitangazia matokeo kinyume cha taratibu na sheria za uchaguzi.

Pia, imesema imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vurugu zinazotokea katika maeneo mbalimbali nchini wakati wa kusubiri kutangazwa rasmi kwa matokeo ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani, uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Hayo yalisemwa jana na Makamu Mwenyekiti wa THBUB, Bahame Nyanduga, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ambapo alitumia fursa hiyo kukemea vitendo hivyo vinavyofanywa na wanasiasa na wafuasi wao.

“Vitendo hivi siyo tu vinaashiria uvunjifu wa sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi, pia vinaweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu, haki za binadamu na vitendo vinavyokwenda kinyume na misingi ya utawala bora,” alisema.

Alisema vurugu zinazotokea katika maeneo machache ya Tanzania Bara na Zanzibar, zimelilazimu Jeshi la Polisi kutumia nguvu  ili kuhakikisha utulivu na amani  unaendelea kuwepo nchini.

“Kwa kuwa nchi yetu inaongozwa na utawala wa sheria, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inawataka wadau wote wa uchaguzi waongozwe na sheria za nchi na ZEC na NEC ndizo zenye mamlaka ya kutangaza washindi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi,” alisema.

Alisema tume inawaomba wananchi watakaobaini uvunjifu wowote wa haki za binadamu, au uvunjifu wa sheria ya uchaguzi, kuzijulisha mamlaka husika na pia wanaweza kutoa taarifa kwao kwa kutuma ujumbe mfupi  kwenda namba 0754 460 259.

No comments:

Post a Comment