Wednesday 7 October 2015

DK. SHEIN AWATAKA WANANCHI KUICHAGUA CCM




MGOMBEA Urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi kuendelea kuichagua CCM, kwani ndio inayothamini na kutekeleza malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Akihutubia mkutano mkubwa wa aina yake wa kampeni uliofanyika Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Shein, alisema Chama kitaendelea kuyaenzi Mapinduzi pamoja na Muungano kwa kuweka misingi imara itakayowanufaisha wananchi wote.
Dk. Shein aliwaambia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa wanapaswa kuichagua CCM, kwani ndicho Chama chenye uwezo na kimeonyesha mfano wa utekelezaji wa malengo ya Mapinduzi na ahadi za Rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume.
“Mapinduzi ndiyo yaliyoweka msingi wa usawa na kuondoa ubaguzi ambao uliwanyima haki na kuwakandamiza wananchi walio wengi wa Zanzibar,” Dk. Shein.
Alisema Mapinduzi yalileta usawa na kujenga mazingira ya kuijenga nchi kwa ushirikiano na kwa umoja na kwa maslahi ya watu wote.
Mgombea huyo alisema Zanzibar ni maarufu ulimwenguni tangu karne zilizopita, lakini umaarufu huo hautakuwa na manufaa iwapo hawataweza kulinda na kuienzi amani na utulivu uliopo.
Katika kipindi kijacho, Dk. Shein aliahidi kuimarisha huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, umeme, maji pamoja na miundombinu ya barabara ili kukidhi mahitaji makubwa ya huduma hizo kutokana na mji huo kukua.
 “Tutaimarisha huduma za umeme kwa kuweka transfoma kubwa yenye KVA 200, katika mji mpya ulioko Ras Nungwi, itakayoweza kuhudumia wateja wengi na kwa uhakika zaidi,”alisema.
Dk.Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa biashara ya utalii ndio inayoipatia Zanzibar fedha nyingi za kigeni, hivyo lengo la serikali katika miaka mitano ijayo ni kuongeza idadi ya watalii wanoitembelea Zanzibar na kufika 500,000, ifikapo 2020, kutoka 300,000, hivi sasa.
Alisema Nungwi inaendelea kusonga mbele kwa kujenga majengo mengi na hoteli nyingi za kitalii.
Dk. Shein alisema akichaguliwa tena, serikali yake itawajengea uwezo wavuvi nchini kwa kuwapatia boti zenye ukubwa wa kati na kubwa ili waweze kuvua kwa uhakika na kupata mapato makubwa zaidi.
Kuhusu kilimo cha mwani, Dk. Shein alisema ataiamarisha soko la mwani kwa kutafuta masoko mapya ya zao hilo ili wakulima waweze kupata bei nzuri na kufaidi jasho lao.

No comments:

Post a Comment