Friday 9 October 2015

DK. SHEIN: HAKUNA MWENYE UBAVU WA KUVURUGA UCHAGUZI





NA SULEIMAN AME, ZANZIBAR

”UCHAGUZI mkuu wa Oktoba, mwaka huu, utakuwa huru na haki na hakuna mwenye ubavu wa kuvuruga zoezi hilo la kidemokrasia ambalo lipo kwa mujibu wa katiba,” ni kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein, aliyoitoa katika mkutano wa kampeni za uchaguzi huko Mkokotoni mkoa wa Kaskazini, Unguja.

Dk.Shein ambaye ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi katika kinyanganyiro cha urais wa Zanzibar, amelazimika kutoa kauli hiyo kufuatia kuwepo kwa matamshi yanayotolewa na baadhi ya wanasiasa kwamba uchaguzi utakuwa na vurugu kama chama fulani kitashindwa katika uchaguzi huo mkuu.

Dk.Shein amelazimika kuwatoa wananchi hofu na wasiwasi mkubwa uliotanda wakati taifa likielekea katika uchaguzi mkuu.

Anafafanua kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaongozwa kwa mujibu wa katiba na sheria na uchaguzi ni mfumo wa kidemokrasia wenye lengo la kupata viongozi watakaoongoza nchi baada ya kipindi cha miaka mitano baada ya kupata ridhaa kutoka kwa wananchi.

Amasema hafurahishwi na kauli zinazotolewa na viongozi wa kisiasa katika majukwaa ya mikutano, ambazo kwa kiasi kikubwa zinaashiria chuki na uhasama na mwelekeo wa kuhatarisha amani ya nchi.

“Zipo kauli zinatolewa na  viongozi wa kisiasa, zinatia mashaka makubwa. Wanasema CCM watake wasitake watatoa nchi au mwaka huu hatukubali kuporwa ushindi wetu, vijana jitayarisheni kuingia barabarani,”anasema kauli za namna hiyo ni za kichochezi.

Dk.Shein anasema hizo si kauli za kiungwana na kistaarabu, ambazo hazipaswi kutolewa na viongozi waliopo madarakani wanaounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Anawakumbusha viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kinaunda  Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kutambua kwamba serikali hiyo ilipatikana baada ya kuwepo kwa mivutano ya kisiasa.

Anaeleza kuwa uhasama huo ulisababisha kumwagika kwa damu kwa mara ya kwanza na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwepo kwa wakimbizi wa kisiasa waliokwenda kuishi uhamishoni Mombasa.

“Nawakumbusha wananchi madhara ya siasa za chuki na uhasama pamoja na matamshi yenye kulenga kusababisha vurugu.Zanzibar tunatoka mbali, wanasiasa msijaribu kusahau ukweli uliopo,”anaeleza.

Anasema lengo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kujenga mazingira mazuri ya kisiasa yatakayoviwezesha vyama kufanya siasa za kistaarabu kwa kujenga nguvu ya hoja mbele ya wananchi ambao ndiyo wenye uamuzi.

Anasema kwamba kauli za kujaribu kuwashawishi vijana kuingia barabarani kama hawatoridhika na maamuzi yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi kuhusu matokeo ya urais ni dhahiri kwamba yanalenga kuleta vurugu.

Anasema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndiyo yenye maamuzi ya mwisho ya kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu na hakuna taasisi nyingine itakayohoji matokeo hayo.

Anafafanua kwamba, kazi ya kulinda kura zlizopigwa katika uchaguzi mkuu si ya vijana kwani zipo taasisi zilizopewa uwezo wa kufanya kazi hiyo.

“Natoa wito kwa vijana kwamba msikubali kusikiliza kauli za wanasiasa wenye lengo la kuwaingiza katika matatizo na vurugu za kisiasa kwa malengo yao binafsi ikiwemo uchu wa madaraka,”anasema.

Aidha anawataka wazazi kuwa macho kwa kutokubali kuwashawishi watoto wao kuingia barabarani kwa ajili ya kufanya vurugu za kisiasa kwani vyombo vya ulinzi vipo na vitapambana na aina yoyote ya vurugu.

Anavitaka vyama vya siasa pamoja na viongozi wake kufahamu majukumu makubwa waliyokabidhiwa na wananchi ya kulinda amani na utulivu wa nchi.

Anasema huu ni wakati wa kufanya kampeni za kistaarabu zenye kujenga nguvu ya hoja na kuwaachia wananchi kupima nani mwenye sifa za kuchaguliwa na kukabidhiwa jahazi la kuongoza nchi.

Anawakumbusha wananchi na viongozi kwa ujumla kwamba, nchi nyingi za Bara la Afrika zinaingia katika machafuko ya kisiasa katika kipindi hiki kutokana na kauli tata na za kichonganishi kutoka kwa wanasiasa.
 
“Sitaki kuzitaja nchi za Bara la Afrika ambazo zimeingia katika vurugu za kisiasa kwa sababu ya uchaguzi mkuu uliosababishwa na viongozi kushindwa kuheshimu maamuzi ya kidemokrasia ya wapiga kura,”anasema Dk.Shein.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim, akizungumza na wahariri waliohudhuria mkutano uliotayarishwa na ZEC alisema kwamba taasisi hiyo ipo huru katika kutekeleza majukumu yake na kamwe haipokei ushauri au maagizo kutoka kwa mtu yeyote.

“Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inafanya kazi zake kwa mujibu wa katiba ya nchi na haipokei maagizo au amri kutoka kwa kiongozi yeyote au taasisi,”anaeleza.

Anasema Tume ya Uchaguzi imejiandaa vizuri kusimamia zoezi kubwa la Uchaguzi Mkuu na kuona kwamba unafanyika katika mazingira ya uhuru na uwazi zaidi na aliyeshinda ndiye atakayetangazwa.

Akifafanua zaidi anasema wapo watu wanaoitilia shaka taasisi hiyo kwamba ipo kwa ajili ya kupokea maagizo kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu serikalini na kusema si kweli.

Anasema Tume imejipanga vizuri kusimamia zoezi la uchaguzi mkuu ikiwemo katika suala la vifaa vya kupigia kura hadi utaratibu mzima wa kutangaza matokeo kuanzia ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani hadi wa urais.

“Tume ya uchaguzi ipo tayari kwa ajili ya kusimamia uchaguzi mkuu huku ikiwa imejipanga vizuri katika maeneo yote muhimu hadi kutangaza matokeo ikiwemo ya urais,”anasema.

Shekhe Norman Jongo ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Amani yenye malengo ya kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani, anawataka viongozi wa vyama vya siasa kuachana na jazba ambazo matokeo yake ni kujenga chuki.


Anasema vitendo vya vurugu za kisiasa athari zake ni kubwa huku akiwakumbusha wazazi kufahamu mambo yaliyopita miaka ya nyuma ambapo wananchi walipotea maisha kwa fujo za kisiasa zilizopelekea  kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Tunawaomba viongozi wa dini pamoja na maimamu kuliombea dua taifa la Tanzania ambalo linapita katika kipindi kigumu cha ushindani wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu,”anaeleza.

Naibu Inspekta Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Abrahmani Kaniki, wakati akizungumza na Makamanda wa Jeshi la Polisi kisiwani Pemba,anawakumbusha majukumu yao makubwa yaliyomo katika katiba katika kuimarisha amani na utulivu wa nchi.

Kaniki anawataka Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa kuzingatia katiba na sheria za jeshi hilo na kuepuka ushabiki wa kisiasa unaoweza kuiingiza nchi katika vurugu za kisiasa.

“Majukumu ya Jeshi la Polisi katika kusimamia amani ya nchi ni makubwa kwa hivyo mnatakiwa kutekeleza majukumu yenu kwa kufuata katiba ya nchi na sheria zinazoliongoza jeshi hili,”anasema.

No comments:

Post a Comment