Na Tito
Msemakweli
“NI kweli
nilimshawishi Namelock agombee ubunge kwa tiketi ya CCM, lakini mambo
yalipobadilika nilimshauri ajitoe. Kama CCM hainitaki kwqa nini yeye abaki?”
Hiyo ni kauli ya mgombea urais kwa tiketi ya Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa,
Edward Lowassa.
Ni kauli
aliyoitoa kwa wananchi wa Monduli alipowahutubia juzi akiwaomba kura ili apate
ridhaa ya kuingia Ikulu na kuwa rais wa tano wa Tanzania; akijieleza pia kwa
wana chi hao baada ya Namelock kumkatalia ombi lake hilo akimsifu kuwa ni binti
msikivu.
Namelock
ambaye ni binti wa Waziri Mkuu wa zamani, marehemu Edward Sokoine aliamua
kushikilia msimamo wake wa kutaka kumrithi Lowassa kwenye kiti cha ubunge wa
Monduli kwa tiketi ya CCM, ingawa kwa sasa Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu kwa
kashfa ya Richmond ameonekana kumkasirikia.
“Kama mtu
amebaki CCM mimi nifanye nini?” Alihoji na kusema sasa atamwombea kura Julius
Karanga ambaye anagombea nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema, chama kilichompokea
Lowassa na kumpachika kugombea urais bila kufuata utaratibu wa kidemokrasia.
Ni
dhahiri, kuwa Lowassa ameumbuka kwa Namelock, binti ambaye awali alimheshimu na
kumsikiliza kwa mambo mengi akiwa kada wa CCM na mbunge wa Monduli, Waziri na
Waziri Mkuu, lakini alipomwona mzee huyo amekengeuka akamwacha aende zake.
Lowassa
ambaye anajiona kuwa mlezi wa familia ya Sokoine, amekuwa akijipa madaraka
makubwa ya kutaka kuiendesha familia hiyo ikiwa ni pamoja na kuwachagulia
wanafamilia maisha ya kufuata, mojawapo likiwa hilo la Namelock ambaye
amemshitukia.
Inasikitisha
kuwa Waziri Mkuu mwingine mstaafu, Frederick Sumaye, anamuunga mkono mgombea
wake huyo ambaye anampigia debe usiku na mchana kwa kutoa kauli sawa na hiyo
iliyojaa ubaguzi kwamba:
“Wale
watu wa Monduli ambao walikuwa wanamfuata Lowassa na sasa hivi hawako naye,
hawawezi kuwa watu wake. Kama mtu amebaki CCM si mtu wa Lowassa hata kama
alikuwa anamsaidia kisiasa.”
Mpiga
debe huyu anafanya kila juhudi kuhakikisha Lowassa anakosana na hata ndugu zake
na wafadhili wake, kwa sababu tu hawako pamoja ndani ya Chadema au Ukawa, huku
akihanikiza kuwa walioko CCM wabaki na Magufuli (Dk John) kwa kuwa Lowassa hana
mtu CCM! Hivi ni kweli?
Ingekuwa
kweli mbona wanaendelea kurubuni watu kwa kauli za kimtaani za ‘Toroka Uje’
wakimtumia mwanasiasa mwingine mchovu, Hamis Mgeja ambaye anaamini kwamba CCM
ilikuwa mali ya ‘mkata pumzi’ Kingunge Ngombale-Mwiru ambaye ametoroka na
kwenda Chadema.
Wakati
Magufuli anahubiri kuwa atakuwa kiongozi wa watu wote bila kujali tofauti za
kiitikadi, kidini na kikabila, Lowassa na Sumaye wanaamini kwamba wasio Chadema
na Ukawa si watu wao na hivyo hawatawaongoza. Huku ni kufilisika kifikra na
kisiasa.
Namelock
ambaye alikuwa karibu sana na familia ya Lowassa, ameonesha msimamo wa marehemu
baba yake wa kukataa kurubuniwa na kushawishiwa kwa ‘Big G za kuazima’ na
kuamua kubaki ndani ya chama kilichomlea baba yake mpaka akapoteza maisha kwa
ajali ya gari akiwa mtu maarufu ndani na nje ya nchi.
Heshima
kama hiyo wameikataa akina Kingunge, Lowassa na Sumaye, ambao wameamua kujitoa
mhanga kutafuta madaraka kwa njia yoyote ile, ili mradi wahakikishe mwisho wa
siku wanaingia Ikulu kuendeleza ufisadi waliokuwa wakiufanya.
Namelock
amekataa kuingia kwenye tandabui la makandokando yasiyoeleweka yaliyogubikwa na
uporaji ardhi za wakulima, uingizaji nchini kampuni hewa za kuzalisha umeme,
uporaji zabuni za maeneo ya maegesho na stendi Dar es Salaam na kujinasibu
kusaidia wananchi kuondokana na umasikini huku wakiwaibia.
Wapo
wengi wanaorubuniwa na wapambe wa Lowassa na Ukawa kwa jumla ili wavihame vyama
vyao na kujiunga na Ukawa, ili eti wasaidie kuing’oa CCM madarakani kama
ambavyo amekuwa akijinasibu Sumaye katika mikutano ya hadhara ya kumzungumzia
Lowassa ambaye anaonekana kuanza kupoteza kauli.
Sumaye
ambaye amekuwa kama fisi anayenyemelea mkono wa binadamu udondoke aukwapue,
anafanya jitihada za makusudi za kuhakikisha walioko karibu na Lowassa
hawaendelei kuwa pale, ili likitokea la kutokea hata kama ni baada ya miaka
mitano neema iwe kwake.
Ndiyo
maana ya kauli ya : “Kama mtu amebaki CCM si mtu wa Lowassa hata kama alikuwa
anamsaidia kisiasa,” ambayo ilipaswa kutolewa na Lowassa mwenyewe na si mpambe,
mpiga debe au mshenga awayeyote.
Lowassa
alitaka kumfanya Namelock awe kama Fred mwanawe ambaye alimwamuru siku ya
kwanza alipojiunga anChadema naye apewe kadi sambamba na wanawe wengine na
mkewe ambaye inasemekana alimkubalia kwa shingo upande.
Wapo wana
CCM wengi ambao walifuatwa na kundi la Lowassa kushauriwa kumfuata, lakini
wengi wao walikataa baada ya kumeona Lowassa wa sasa si yule aliyekuwa CCM,
ambaye alikuwa na fikra na uamuzi binafsi tofauti na sasa ambapo fikra na
uamuzi anaazima kutoka kwa akina Sumaye na Freeman Mbowe.
Kutokana
na hali hiyo, si rahisi kwa mtu timamu anayejitambua na kuelewa analolifanya,
kukubali kurubuniwa au kushawishiwa kujiunga na kambi ya mtu ambaye hana
mwelekeo wa kisiasa, achilia nmbali uwezo wa kuongoza Taifa kutokana na udhaifu
alionao kiafya.
Wengi
wanaojiunga kwa Lowassa ni wanaokumbwa na upepo na mawimbi bila kujua
yanawafikisha wapi, lakini ni hao ambao hata wanapoondoka CCM hawaachi
pengo na hata huko waendako hawasaidii chochote na ndiyo sababu wamebaki kuwa
maboya na mavuvuzela wa mgombea.
Wako wapi
akina John Guninita, Lawrence Masha, Mgana Msindai, Tambwe Hiza, Makongoro
Mahanga, James Lembeli, Goodluck ole Medeye? Wameongeza nini kwenye
Ukawa? Walirubuniwa na kuahidiwa nafasi lakini hakuna lolote ingawa baadhi yao
wanawania ubunge ambao hawataupata kwa ridhaa ya wananchi.
Walidhani wanafuata
nyuki kupata asali lakini wataambulia manundu.
No comments:
Post a Comment