Saturday, 24 October 2015

JK AFUNGUKA KASHFA YA RICHMOND, ASEMA MUHUSIKA MKUU NI LOWASSA, ASEMA CCM HAIENDESHWI KIBABE

Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli akiwapungia mkono wananchi waliofurika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, kusikiliza mkutano wake wa mwisho uliofanyika jana
Rais Jakaya Kikwete akiwapungia mkono wananchi baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jana
Rais Kikwete akimtambulisha Dk. Magufuli kwa wananchi
Rais Kikwete na Dk. Magufuli wakiserebuka jukwaani
Dk. Magufuli akiwahutubia wananchi wakati wa mkutano huo
Dk Magufuli akimwaga sera kwa wananchi

Na Rashid Zahor, Mwanza

WAKATI uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani unatarajiwa kufanyika kote nchini leo, hatimaye Rais Jakaya Kikwete ameamua kufichua ukweli kuhusu muhusika mkuu wa kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond.

Rais Kikwete amesema muhusika mkuu wa kashfa hiyo ni mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa, ambaye alilazimika kujiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2008.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kuzungumzia kashfa hiyo, tangu Lowassa alipojiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2008, baada ya kamati ya bunge iliyoundwa kuchunguza kashfa hiyo kumtia hatiani.

Aidha, Rais Kikwete amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakiendeshwi kibabe kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai, bali kinadendeshwa kwa kufuata taratibu na katiba ya Chama.

Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alisema hayo jana, alipohutubia mkutano wa kufunga kampeni za kuwania urais, uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini hapa na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Mkutano huo umeweka rekodi mpya ya mahudhurio katika mikutano yote ya kampeni, iliyofanywa na mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli, ambaye ametamba kuwa ana uhakika mkubwa wa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano wa serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa zaidi ya asilimia 90.

Akizungumzia kashfa ya Richmond,Rais Kikwete alisema ni kweli alikubali iletwe mitambo ya kuzalisha umeme ili kuongeza kiwango cha umeme wakati huo, lakini  hakushiriki katika uteuzi wa kampuni hiyo.

Rais Kikwete, aliyeanza kuhutubia mkutano huo saa 10.30 jioni, alisema wakati akitoa ruhusa ya kuletwa kwa mitambo hiyo, aliwasisitizia wahusika, akiwemo Lowassa kuwa ni lazima sheria ya manunuzi izingatiwe,  lakini hilo halikutekelezwa.

"Sheria za manunuzi hazikuzingatiwa. Waziri Mkuu aliteua kamati ya makatibu wakuu na wakawa wanaripoti kwake. Matokeo yake iliteuliwa kampuni, ambayo haikuwa na uwezo,"alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa kwa mayowe mengi ya wananchi.

Rais Kikwete alisema alimshangaa Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, alipomtaka aseme ukweli kuhusu muhusika mkuu wa kashfa hiyo, ambapo alimjibu kuwa mtu huyo amekuwa akisafiri naye kwenye mikutano ya kampeni ya chama hicho.

Kudhihirisha kwamba kampuni ya Richmond ilikuwa ya kitapeli, Rais Kikwete alisema aliiagiza Wizara ya Fedha isitoe fedha zilizoombwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Ibrahim Msabaha kwa ajili ya kuilipa kampuni hiyo kwa vile ilishatiliwa shaka.

"Msabaha alinifuata akanilalamikia kwamba wizara ya fedha imekataa kutoa fedha za kuilipa Richmond, mimi nikaipongeza wizara imefanya vizuri kwa kuwa kampuni ambayo ilikuwa ilipwe pesa hizo, ingeweza kuingia mitini bila kuleta mitambo hiyo. Nikaagiza walipwe baada ya kuleta mitambo,"alisema Rais Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa pia alipinga vikali madai yaliyotolewa na baadhi ya makada wa Chama waliohamia upinzani kwamba, amekuwa akikiendesha kibabe na kinyume cha katiba.

Alisema hakuna ubabe katika CCM na kusisitiza kwamba kimekuwa kikiendeshwa kwa kufuata katiba bila kumuonea mtu yeyote.

"Hakuna ubabe CCM. Kila mtu ataingia kwenye Chama kwa hiari yake na atatoka kwa hiari yake. Hatuna muda wa kumbembeleza mtu,"alisema.

Alisema uteuzi wa mgombea urais kupitia CCM ni suala nyeti na kwamba masuala mbalimbali muhimu yalijadiliwa na kuzingatiwa, ikiwa ni pamoja na afya ya mgombea, ambapo Dk. Magufuli alikuwa bora kuliko wengine.

"Wengine afya zao zilikuwa na mashaka na Chama kinajua. Si mmeona wenyewe? Mkutano umebaki dakika tatu kumalizika, ndipo mgombea anasimamishwa kuhutubia. Ndio sababu hakufika katika baadhi ya wilaya,"alisema Rais Kikwete na kuamsha mayowe ya kumshangilia kutoka kwa wananchi.

Alisema baadhi ya watu walikuwa na imani kwamba Chama kingefia Dodoma wakati wa vikao vya kumteua mgombea urais, lakini badala yake kimefanya mabadiliko makubwa na kuendelea kuwa imara.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, baadhi ya watu waliokuwa wakitaka CCM ife, walikuwa wakiendesha mikutano yao kwenye ukumbi wa St Gasper, ikiwa ni pamoja na kufanya vitendo vilivyokuwa na mwelekeo wa kumtisha, lakini alikuwa imara.

"Tulipoingia mkutanoni, badala ya kuonyesha imani kwa chama, watu wanaonyesha imani kwa mtu. Mzee mmoja aliwafundisha wapige kura ya kutokuwa na imani na mimi. Nilichofanya niliwapigia makofi na kusema haijapata kutokea kwa sababu haijawahi kutokea wanachama wanakuwa na imani na mtu badala ya chama kisha nikawaambia tukae tufanyekazi,"alisema.

Aliongeza kuwa wakati wa kikao hicho, aliwapa nafasi wajumbe waliokuwa wakimuunga mkono Lowassa ili wamtetee, lakini hoja zao zilizidiwa nguvu na wale waliokuwa wakipinga uteuzi wake na katika kupiga kura, Lowassa alimpigia Dk. Magufuli.

Alimwelezea Dk. Magufuli kuwa ni mchapakazi aliyefanya vizuri katika wizara zote alizomteua kuzisimamia na kwamba anaposema hapa ni kazi tu, anamaanisha kile kinachotoka moyoni mwake.

Alisema wagombea wa upinzani wanashindwa kumsema vibaya Dk. Magufuli kwa sababu hana chembe ya uchafu, tofauti na wagombea wengine wanaoshindwa kuzungumzia mikakati yao katika kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Awali, Rais Kikwete aliwapongeza wakazi wa Mwanza kwa kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano huo, hali iliyodhihirisha wazi kwamba wanavutiwa na Dk. Magufuli na watampigia kura nyingi leo.

Rais Kikwete alisema amewahi kufanya  mikutano kwenye uwanja huo mara nyingi, ikiwa ni pamoja na kwenye kampeni zake za kwanza mwaka 2005, lakini hakuwahi kupata idadi kubwa ya watu kama ilivyokuwa jana.

Hata hivyo, aliwataka wananchi hao wasiutafsiri wingi huo wa watu kuwa Dk. Magufuli ameshinda, badala yake wajitokeze kwa wingi kupigakura leo na kumchagua mgombea huyo na wengine waliosimamishwa na CCM.

Aliwaonya wafuasi wa vyama vya upinzani watakaothubutu kufanya vurugu leo kuwa watakiona cha mtema kuni. "Asiyejipenda afanye uhuni kesho,"alisema huku akishangiliwa.

Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Magufuli alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais, vipaumbele vyake vitakuwa ni kuwapelekea wananchi huduma za maji safi na salama katika maeneo yanayokabiliwa na uhaba wa huduma hiyo.

Aidha, aliahidi kufikisha umeme katika maeneo yote ambayo bado hayajapata huduma hiyo na kuongeza kuwa, kupatikana kwa huduma hiyo kutasaidia kupunguza uhaba wa maji.

Aliwataka watendaji katika serikali wenye tabia ya kula rushwa na kushindwa kusimamia maeneo yao inavyotakiwa, wakae mkao salama kwa vile Magufuli anakuja.

Dk. Magufuli aliwapongeza wakazi wa Mwanza kwa kuhudhuria kwa wingi katika mkutano huo na kwamba hivyo ndivyo imekuwa ikifanyika katika mikoa mingine, hali inayompa imani kubwa ya kuchaguliwa kuwa rais kwa kishindo.

Alisema mahudhuria hayo yanadhihirisha jinsi Watanzania walivyopania kuleta mabadiliko ya maana katika nchi yao na yaliyolenga kuwaletea maendeleo.

Mgombea huyo aliwaomba radhi wananchi wa majimbo matano, ambayo ameshindwa kwenda kufanya mikutano ya kampeni, lakini aliahidi kuyatembelea katika mikutano yake ya kuwashuruku wananchi.

Alisema kila alikokwenda amekuwa akipata mapokezi mazuri na uamuzi wake wa kusafiri kwa gari umbali wa kilometa 46, 892 umempa elimu ya shida za wananchi, hivyo atakapokuwa rais, atazipa kipaumbele katika kuzitatua.

Pia alisema amekuwa akipata ushauri wa aina mbalimbali kupitia kwenye mitandao ya kijamii, magazeti na mabango na kuongeza kuwa, atauzingatia ushauri huo na kuufanyiakazi.

"Nawashukuru wagombea wenzangu saba, lakini nawakumbusha asiyekubali kushindwa si mshindani. Wote wanafahamu kwamba rais wa awamu ya tano atakuwa Magufuli,"alisema mgombea huyo huku akishangiliwa.

Kwa upande wake, mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wananchi waendelee kuuenzi Muungano wa Tanzania na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.

Aidha, alisema si kweli kwamba vijana ni bomu linalosubiri kupasuka, bali ni rasilimali ya taifa, hasa iwapo itatumiwa vizuri katika kuleta maendeleo.

Aliwashukuru wanahabari aliosafiri nao wakati wa mikutano hiyo, madereva na wasanii, ambao walishiriki bega kwa bega na viongozi wa CCM kunadi sera za Chama kwa wananchi.

Hata hivyo, aliwataka vijana wasikubali kutumiwa na wanasiasa kufanya vitendo vya kihalifu, badala yake aliwataka wawe wajenzi wa taifa lao.

Dalili za wakazi wa Mwanza kuvunja rekodi ya mahudhurio katika mkutano wa jana, zilianza kuonekana mapema asubuhi, wakati misururu ya watu ilipoanza kwenda kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Hadi ilipotimia saa 6 mchana, sehemu zote za kukaa kwenye uwanja huo zilikuwa zimejaa na kusababisha idadi nyingine kubwa ya watu kusimama eneo la katikati ya uwanja.

Kabla ya mkutano kuanza na wakati ukiendelea, baadhi ya wananchi walijikuta wakipoteza fahamu kutokana na msongamano mkubwa wa watu na hivyo kukosa hewa.

Msafara wa Dk. Magufuli uliwasili uwanjani saa 8.59 na kupokewa na mayowe mengi. Mgombea huyo alilazimika kusimama juu ya gari kuwapungia mikono wananchi na kuzunguka uwanjani.

Wakati Dk. Magufuli akiwasili uwanjani, wimbo wa CCM mbele kwa mbele wa kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT), ulipigwa na kumfanya kila mtu aimbe na kucheza. Wananchi hao walipeperusha hewani kofia na mabango yenye nembo za CCM.

Rais Kikwete aliwasili uwanjani saa 9.06 na kupokelewa na Dk. Magufuli, mgombea mwenza, Samia, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo, Katibu wake, Miraji Mtaturu na viongozi wengine wa Chama.

Wakiwa jukwaani, Rais Kikwete alimshika mkono Dk. Magufuli na kuunyanyua juu mbele ya wananchi, ambao walilipuka mayowe ya kumshangilia.

Katika mikutano yao wa kampeni, Dk. Magufuli alitembea umbali  wa kilometa 46, 892 wakati Samia alitembea umbali wa kilometa 39,215. Magufuli alihutubia mikutano rasmi 470 wakati Samia alihutubia mikutano 405.

Aidha, Dk. Magufuli alihutubia mikutano isiyo rasmo 2,401 wakati Samia alihutubia mikutano 1,820.

No comments:

Post a Comment