Pia, amesema kuwa uamuzi wake wa kujiondoa ndani ya CCM baada ya miaka 61 ya kutumikia TANU na CCM, ni ishara ya mtu aliyepoteza mwelekeo na anayestahili kusaidiwa.
Aidha, amesema kuwa hoja zinazotolewa na Mzee Kingunge ni dhaifu na kwamba, hazina tofauti na mtu aliyepofushwa macho na rushwa hivyo, ni mtu wa kusikitisha na wa kuonewa huruma.
Makamba aliyasema hayo jana, wakati wa mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Tabora, ambapo alisema uamuzi wa Kingunge kujiunga na mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, hauna tija.
"Ngombale anadanganya Watanzania anapodai mabadiliko yamechelewa katika nchi yetu, wakati yeye ameshiriki katika kutengeneza sera zote za nchi hii kwa miongo mingi iliyopita," alisema.
Akieleza kwa ukali huku akionyesha hadharani vitabu vya sera na miongozo mbalimbali ya CCM na TANU, ambayo Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alishiriki kutengeneza, Makamba alisema:
"Muongozo wa mwaka 1971 wa CCM, Mzee Kingunge ameshiriki kutengeneza (anauonesha), muongozo wa mwaka 1981, Mzee Kingunge ameshiriki kuutengeneza, muelekeo wa sera za CCM miaka ya 1990, Mzee Kingunge ameshiriki kutengeneza, muelekeo wa sera za CCM miaka ya 2000 hadi 2010, Mzee Kingunge ameshiriki kutengeneza, leo hii anapata wapi ujasiri wa kubeza sera alizozitengeneza mwenyewe?"
Makamba alifafanua kuwa sera hizo ndizo zilizoongoza serikali za awamu zote katika kutekeleza mipango ya maendeleo.
"Sote tunafahamu kuwa sera na miongozo hii ndiyo ambayo serikali za awamu zote zimekua zikitekeleza. Sasa huyu Kingunge anawezaje kuzikana sera alizozitengeneza mwenyewe? Hawezi kukwepa kama kuna mapungufu yoyote, maana yeye ni sehemu yake,"
alisema Makamba.
Alisema Kingunge aliingia CCM akiwa kijana na amelelewa na kukulia ndani ya CCM, hivyo hatua yake ya kukashifu CCM na serikali yake ni kukosa shukurani.
"Mtu amekulia CCM, ameishi CCM maisha yake yote, leo amezeeka hana hata meno anasema CCM imeishiwa pumzi. Kwa kweli yeye ndiye atakuwa amechoka na kuishiwa pumzi, sio CCM," alisisitiza.
KUKATWA LOWASSA
Akijibu hoja ya Mzee Kingunge kuwa utaratibu wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka huu wa 2015, ulikiuka katiba, Makamba alisema kuwa hoja hiyo ni dhaifu na ya uongo.
Alisisitiza kuwa utaratibu uliotumika kumpata mgombea urais wa CCM mwaka 1995, ndio uliotumika mwaka huu.
"Mwaka 1995, mimi na Kingunge wote tulikuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), sababu zilizofanya jina la Lowassa likatwe ndio hizo hizo zilizofanya akatwe jina lake mwaka huu Dodoma.
Tena Kingunge anakumbuka mimi na yeye tulihoji ndani ya kikao, tukaambiwa uadilifu wa Lowassa unatiliwa shaka.
"Mimi nilitumwa kwenda kumuita nikamuuliza kuwa anatuhumiwa ana mali nyingi ambazo hazina maelezo yake, akashindwa kujibu," alisema.
KINGUNGE KAHONGWA?
Alisema hatua ya Kingunge kusema uongo bila aibu na kumtetea Lowassa, ni ishara kuwa bila shaka njaa inamsumbua na huenda kapewa chochote ili amtetee na hatimaye kuamua kumfuata UKAWA.
Huku akishangiliwa na wananchi wa Tabora, waliohudhuria mkutano huo, Makamba alinukuu vifungu vya biblia na kusema:
"Katika kitabu cha kutoka 23:6-8 , imeandikwa kuwa rushwa hupofusha macho ya waonao, kwa hiyo Kingunge kawa kipofu sababu ya kupewa chochote."
MSHAURI WA RAIS MKAPA, KIKWETE
Akiendelea kumchambua Mzee Kingunge na hatua yake ya kutaka mabadiliko, Makamba aliwaeleza wananchi kuwa mzee huyo alikuwa mshauri wa Rais katika vipindi tofauti, wakati wa Benjamin Mkapa na Rais Kikwete, hivyo ni sehemu ya mafanikio na changamoto zote zilizoko nchini kwa sasa.
"Alipokua mshauri wa Rais Mkapa na Kikwete, aliwashauri nini?Au anategemea Lowassa ashinde ili awe mshauri wake tena?"Alihoji.
GWAJIMA APIMWE AKILI
Katika hatua nyingine, Makamba alisema kuwa mshauri wa kiroho wa Lowassa, Askofu Josephat Gwajima, anatakiwa akapimwe akili mara moja kutokana na kauli yake ya kutaka kuchochea chuki za kidini nchini.
"Gwajima anasema ana ndoto ya kuona misikiti itakuwa Sunday Schools, na masheikh wanasujudia msalaba. Tafsiri ya hii ni kufuta uislamu. Huku ni kupandikiza chuki za kidini nchini. Nashauri akapimwe akili haraka," alisema.
RAGE AMNADI MAGUFULI
Naye Mbunge wa Tabora Mjini anayemaliza muda wake, Alhaji Ismail Aden Rage, alisimama jukwaani kwa mara ya kwanza katika mkutano wa kampeni na kuwaombea kura mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, mgombea ubunge Emmanuel Mwakasaka na madiwani wote wanagombea kupitia CCM.
Alhaji Rage alieleza mafanikio ya serikali ya CCM kwa wananchi wa Tabora, ikiwemo kuimarika kwa huduma za maji, miundombinu na afya.
No comments:
Post a Comment