Sunday, 11 October 2015

UVCCM YAWATAKA VIJANA KULINDA AMANI




Na Mwandishi Wetu
UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM), umewataka vijana nchini  kutambua umuhimu wa kuilinda, kuthamini na kuenzi  misingi ya utulivu na amani ya Taifa kwani, inapovunjika au  kuvurugika huwa ni vigumu kuirudisha na kujengeka tena.

Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, katika tamasha la amani, lililojumuisha makundi ya wanamichezo wilayani Temeke, Dar es Salaam.

Amesema kazi ya kuilinda na kuendeleza misingi hiyo inatakiwa kudumishwa na vijana wenyewe kwa sababu ndiyo wahitaji wa kuendelea kuishi huku wakifurahia maisha na maendeleo ya jamii. 

Shaka alisema amani, umoja na utulivu ukitetereka, hakutakuwa na kundi lolote, chama cha siasa wala timu za mipira zitakazopata nafasi ya kukutana na kufanya nazoezi au kujadili maendeleo ya michezo.

"Hivi sasa vijana wenzetu kule Libya, Syria au Somalia hawakutani kama tunavyokutana hapa na kufanya mazoezi, kujumuika, kufurahi pamoja, amani na utulivu kwao vimetoweka,” alisema Shaka.

Alisema hatua hiyo imewakumba kufuatia kupuuzia, kucheza na kutania kuenzi misingi ya umoja, amani, utulivu na wanasiasa kuendekeza tamaa ya kushika madaraka kwa pupa na kusahau umuhimu wa amani.

Aidha, aliwataka vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa wenye malengo hayo hapa nchini na ikibidi kuwasuta na kuwakwepa wanapohubiri hotuba za shari na mgawanyiko katika jamii.

Katibu mkuu huyo wa UVCCM aliwasisitiza vijana wote kutobaguana kwa sababu ya tofauti ya itikadi za kisiasa kwa kuwa kuna maisha mengine baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

"Najua hapa kila mmoja atakuwa ana mapenzi kwa chama chake, tushindane kwa hoja bila kuvutana, tusigawanywe na uchaguzi. Uchaguzi utapita ila Taifa letu litaendelea kubaki moja milele kizazi hadi kizazi,” alisema Shaka.

Alisema vyama vya siasa hujengwa na sera makini, historia yake,  Ilani za uchaguzi na mikakati ya maendeleo na kwamba kile kilichobora kinachoaminiwa na wengi, kifuatwe na kuungwa mkono. 

Shaka alisema ni jambo la aibu na fedheha kubwa ikiwa kuna vijana watakubaki kujitumbukiza wao wenyewe katika mivutano, ugomvi na mgawanyiko katika jamii kwa sababu za kisiasa au uchaguzi.

Shaka alisema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015 hadi 2020, masuala ya sanaa, muziki pamoja na michezo yamepewa  vipaumbele kwa maendelo ya vijana kama sehemu ya kukuza ajira na kujenga afya zao.

No comments:

Post a Comment